Soka ni sayansi, sio figisufigisu zenu

Muktasari:

Zaidi ya yote, soka inahitaji uelewa wa kutosha kuhusu mchezo wenyewe (misingi yake, ufundi na mbinu), utaalamu wa elimu ya viungo (physical education), saikolojia yake na sosholoj

SOKA ni sayansi, taaluma na ni elimu yenye mchanganyiko wa fani mbali mbali ambazo zinalenga kumuwezesha mchezaji aliye na kipaji cha hali ya juu,cha kati na cha kawaida aweze kutimiza majukumu yake vizuri na kwa uhakika wakati anacheza kiwanjani.

Zaidi ya yote, soka inahitaji uelewa wa kutosha kuhusu mchezo wenyewe (misingi yake, ufundi na mbinu), utaalamu wa elimu ya viungo (physical education), saikolojia yake na sosholojia.

Pia inahusisha falsafa, sayansi ya mwili wa binadamu (anatomy and physiology), tiba katika michezo (sports medicine), kanuni za mijongeo/miondoko ya mchezaji (biomechanics and kinesiology).

Vilevile upimaji na tathmini na mengine ili kupata ufanisi, matokeo tarajiwa na yenye maana kwa mwalimu, viongozi, wachezaji na mashabiki wa timu husika.

Nadharia mbalimbali za kitaalamu zinaonyesha kwamba, soka ni mchezo unaotegemea sana wachezaji kuwa na mbinu nyingi na ufundi mwingi, lakini pia matumizi ya akili na nguvu ni muhimu sana hivyo kuufanya mchezo huu kupendwa zaidi na watu wengi.

Tafsiri yake ni kwamba ni mchezo unaohitaji utaalamu ili kuufanya uongezeke thamani, mvuto na uchezwe katika kiwango bora zaidi kulingana na ngazi ya timu na kariba ya wachezaji (level) popote pale licha ya tofauti za mazingira, jiografia, utamaduni wa nchi au jamii sambamba na mfumo wa usimamizi na uendeshaji wa mchezo huu.

Wachezaji katika ngazi yoyote ile hususani vijana wadogo kuanzia miaka mitano na kuendelea wanategemea mambo miwili makubwa ili wawe mahiri kiwanjani kadiri wanavyoendelea kushiriki mchezo huu; utayari na utashi na pili kipaji.

Kazi ya kufundisha soka kwa mwalimu yeyote ina hatua nyingi muhimu, ya kwanza ni kumuelewa mchezaji hususani hulka na haiba yake, kipaji na uzoefu wake nje na ndani ya uwanja, mapungufu yake kiufundi na matatizo mengine yanayoweza kuathiri uwezo wake wa kujifunza kutoka kwa mwalimu au wachezaji wenzake na hatimaye kazi ya msingi na ngumu zaidi ni kuwaunganisha wachezaji kwa kutumia mifumo mbalimbali ya kucheza soka uwanjani.

Mchakato huu unamsaidia mwalimu kuelewa na kuchagua mbinu na njia sahihi atakazozitumia kuwafundisha wachezaji/ mchezaji stadi na mbinu kutoka hatua moja kwenda nyingine nzuri zaidi. Kwa kuwa tendo la kujifunza ni mchakato maalumu, ni wazi kufundisha soka kunahitaji stadi maalumu ili kuibua, kufundisha, kuendeleza na kulinda vipaji vya wachezaji kwa kuandaa program zenye kuzingatia sayansi ya mchezo.

Kwa msingi huu sio kila mtu anaweza kuwa kocha wa soka hata kama aliwahi kucheza soka kwa kiwango cha juu, mpenzi, shabiki wa kupindukia, anatazama kila mechi au anafuatilia sana mchezo huu, ni lazima apite katika darasa angalau ngazi ya awali ili ajifunze namna ya kufundisha soka na afaulu.

Mwalimu ni mtu muhimu katika kuleta mabadiliko chanya ya kitabia na uwezo wa kutenda kwa mchezaji, tena mabadiliko haya ni lazima yawe ya kudumu (permanent change of behavior).

Katika soka uwezo unaonekana ni kucheza kiufundi na kwa kutumia mbinu mbali, utimamu wa mwili, kujituma, kujali muda, uwezo wa kuwasiliana kwa sauti na ishara sambamba na kuheshimiana, kushirikiana na kuthubutu.

Ili haya yote yaonekane kwa mchezaji, lazima kocha apate muda wa kutosha wa kukaa na wachezaji wake ili wapate mabadiliko ya kudumu yanayotarajiwa. Kwa kawaida kukua na kukomaa kimchezo kwa mchezaji kunategemea programu iliyoandaliwa na kocha katika mazoezi (periodisation) kwa kuzingatia kiwango cha uchezaji kinachokusudiwa kukifikiwa.

Kwa muda mrefu sasa soka la Tanzania limekumbwa na tatizo la mfumo mzuri na utaratibu thabiti wa kulinda ajira za makocha wa soka kwa mapana yake. Inaeleweka kuwa, kila timu ina uhuru wa kutosha wa kutafuta mwalimu kwa njia na mbinu zake ilimradi akidhi vigezo husika kwa mujibu wa kanuni na taratibu za Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) kwa upande mmoja na timu kwa upande mwingine, hii ikiwahusu makocha wote wa ndani na nje ya nchi.

Kwa miaka takribani 15 sasa kumekuwa na tabia au mazoea katika timu zetu ya kuwaajiri walimu (mameneja) na kuwatimua/kusitisha mikataba yao baada ya muda mfupi, hata kabla hawajazoea mazingira ya kazi kwa maana ya utamaduni wa timu, wachezaji mmoja mmoja, mashabiki na tabia zao, viongozi na mfumo mzima unaosimamia na kuendesha timu lakini pia wakati mwingine hata kuyaelewa vizuri malengo ya timu.

Hali hii imesababisha kukosa huduma ya wataalamu wazuri wa kigeni na wa ndani kwa sababu asilimia kubwa ya wapenda soka Tanzania wanataka kupata matokeo mazuri ndani ya kipindi kifupi baada ya mwalimu kukabidhiwa timu, ingawa ni kweli kuna asilimia ndogo sana ya walimu wachache sio wazuri kwa kiwango kilichotegemewa.

Kuna ushahidi wa kutosha kwamba walimu wengi hubebwa na historia nzuri ya mafanikio ya walikopita (profile) ambayo mara nyingi hutumika kama kigezo cha kocha kupata ajira na inaonekana kwenye wasifu wao wakati wa kuomba kazi, lakini kwetu imekuwa ni ajabu hakuna mwalimu anayefaa. Wapenda soka walio wengi wanatumia kigezo cha nadharia ya “walimu wanaajiriwa ili wafukuzwe” (coaches are hired to be fired)”. Ukocha ni kazi za kitaalamu hazifanyiwi uamuzi wa kutumia hisia na ushabiki. Kimsingi kuna maswali mengi ambayo hayajapata majibu mazuri miongoni mwa wapenda soka, kwa mfano; ni utaratibu gani unaotumika kuwatambua walimu wanaostahili kukabidhiwa timu? Nani anahusika kwa karibu katika mchakato huu wa kuwatafuta?, Lakini pia kwa muda gani na kwa kutumia vigezo gani? Maswali haya na mengine mengi yanatokana na ukweli kwamba makocha wengi pamoja na sifa nzuri walizonazo wanaonekana hawana sifa ya kufundisha soka katika klabu zetu ndani ya muda mfupi sana.

Ipo mifano mingi, mmojawapo ni msimu uliopita Azam FC iliwafukuza kazi wataalamu wake wote watano wa benchi la ufundi kutoka Hispania baada ya kuiongoza katika mechi 17 tu. Nini kinatuongoza kufanya uamuzi huu nyeti na wa kiufundi usiyohitaji jazba?

Tabia hii na utamaduni huu umekuwa ni kama jambo la kawaida kwa timu kongwe za Simba na Yanga, ndiyo maana maendeleo ya soka katika klabu hizi kongwe nchini ni ya kubahatisha sana nje na ndani ya uwanja. Katika hali ya kushangaza klabu kubwa na kongwe Yanga ilimfukuza kazi mwalimu wake wa kigeni wakati timu ikiwa inacheza soka lenye ubora na imeshikilia vikombe, mpaka leo hakuna anayejua sababu za msingi na za kitaalamu za uamuzi ule. Tunapaswa kufahamu kuwa athari za mabadiliko ya mara kwa mara za benchi la ufundi linawaathiri wachezaji kisaikolojia, hivyo kugusa moja kwa kwa moja kiwango cha umakini uwanjani na uwezo wa utendaji na utekelezaji wa majukumu nje na ndani ya uwanja. .

Kiufundi ufundishaji wa soka ni sanaa (football coaching is an art) ambayo inategemea sana mwalimu mwenye mambo matatu makuu karama (charisma), kujituma na kujitoa(passion),kuupenda na kuufurahia mchezo wenyewe (humor). Hivi vyote vinasaidiwa sana na mazingira rafiki ya kufanyia kazi. Kwa hapa kwetu, walimu wengi wana bahati mbaya ya kukutana na misukosuko mingi katika ajira zao. Wastani wa makocha 7 kati ya 10 hawadumu kwenye ajira zaidi ya msimu mmoja, tunashuhudia kwenye msimu huu 2017/18 tayari aliyekuwa Kocha wa Njombe Mji, Hassan Banyai ametangaza kuachia ngazi baada ya kuiongoza timu katika michezo mitatu tu na baada ya siku 17 tangu ligi ianze. Unatarajia nini kwa timu hii iliyopanda Ligi Kuu?