Sitaki nataka ya Ajib, Niyonzima Simba na Yanga

Muktasari:

  • Lakini sote tunafahamu kuwa kabla hata TFF haijatangaza rasmi kufunguliwa kwa dirisha hilo jana, tayari kurasa za magazeti zilikuwa zimeshaanza kupambwa na picha za wachezaji mbalimbali wa ndani na nje ya nchi wakitajwa kuingia mikataba ama wanawaniwa na timu mbalimbali kwa lengo la kuimarisha vikosi vyao.

BAADA ya kusubiriwa kwa hamu, hatimaye dirisha la usajili kwa timu za Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza sambamba na Daraja la Pili kwa Tanzania Bara limefunguliwa ambapo kuanzia jana Alhamisi hadi Agosti Sita timu zinaruhusiwa kuacha na kuingiza wachezaji, hii ni kwa mujibu wa kalenda ya mashindano ya Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF).

Lakini sote tunafahamu kuwa kabla hata TFF haijatangaza rasmi kufunguliwa kwa dirisha hilo jana, tayari kurasa za magazeti zilikuwa zimeshaanza kupambwa na picha za wachezaji mbalimbali wa ndani na nje ya nchi wakitajwa kuingia mikataba ama wanawaniwa na timu mbalimbali kwa lengo la kuimarisha vikosi vyao.

Sio tu wale waliosajiliwa au kuhitajika kwenye mipango ya usajili, bali pia hata wale wachezaji ambao wanaachwa na klabu zao kutokana na sababu mbalimbali kama kushuka kiwango, utovu wa nidhamu au kuwa majeruhi wa muda mrefu, majina yao yameanza kuwekwa hadharani.

Presha imekuwa kubwa kwa wachezaji, viongozi, mashabiki na hata vyombo vya habari katika kufahamu sura gani zinaondoka na zipi zinaingia kwenye vikosi vya timu kulingana na jinsi ripoti za makocha zilivyoainisha baada ya msimu uliopita kukamilika.

Kwa wachezaji na makocha ambao walifanikiwa kutamba msimu uliomalizika, ni wazi kuwa hiki ndicho kipindi chao cha mavuno kwa kuchota fedha za timu zinazowahitaji au kwa kuongeza mikataba katika timu zao. Ifahamike kwamba fedha za usajili zimekuwa zikitolewa na klabu husika au matajiri wenye mapenzi na timu hizo.

Miongoni mwa majina ambayo yanaonekana kuteka vyombo vya habari katika kipindi hiki ni lile la kiungo wa Yanga na Timu ya Taifa ya Rwanda, Haruna Niyonzima sambamba na jina la mshambuliaji wa Simba na Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Ibrahim Ajib ambao wanaelekea kumaliza mikataba kwenye klabu zao za sasa, jambo linalowapa fursa ya kuendelea kubaki au kuzungumza na timu nyingine.

Kwa kufahamu kuwa mkataba wa Ajib unamalizika, Simba imekuwa ikihaha kuhakikisha mshambuliaji huyo anaongeza mkataba wa kuendelea kuitumikia siku za usoni kutokana na kiwango kikubwa ambacho amekuwa akikionyesha ndani ya timu hiyo.

Hata hivyo, inaonekana wazi kuwa juhudi za Simba katika kumbakiza Ajib, zimeongezeka hasa pale waliposikia kuwa watani wao Yanga wanamwania kwa udi na uvumba nyota huyo sambamba na Singida United na Azam.

Kama ilivyo kwa Simba, ndivyo inavyotokea kwa Yanga ambapo vigogo wa timu hiyo wanahaha usiku na mchana kuhakikisha Niyonzima anaongeza mkataba wa kuitumikia klabu yao, lakini juhudi hizo zote zimechagizwa na tetesi ambazo zimekuwa zikienea kwa kasi kuwa Niyonzima yuko mbioni kujiunga na Simba.

Huu ni utamaduni wa kawaida kwa timu za Simba na Yanga pindi usajili unapofika, ni kama mwiko kwa mchezaji wa upande mmoja kutimkia kwingine hasa wale ambao huwa na nafasi kwenye kikosi cha kwanza kama ilivyo kwa Ajib na Niyonzima.

Simba na Yanga zipo tayari kutumia pesa ya aina yoyote ile kuhakikisha kuwa upande wa pili haumchukui mchezaji wake hata pale mchezaji huyo anapokuwa hahitajiki na benchi la ufundi la timu husika.

Ninapoona jinsi Simba na Yanga zinavyotumia nguvu kubwa kifedha na muda katika kuwashawishi Ajib na Niyonzima wabakie, najikuta nikicheka tu hasa pale ninapokumbuka maisha ya wachezaji hawa wakati ligi inapokuwa ikiendelea.

Ni wachezaji ambao tumeshuhudia mara kwa mara wakipokea matusi na kila aina ya kashfa kutoka kwa mashabiki wa timu zao wakiwatuhumu kuwa wanacheza chini ya kiwango ili kuzihujumu timu hizo.

Ilifika hatua mashabiki, wanachama na baadhi ya viongozi wa Yanga walitamba hadharani kuwa hawamhitaji Niyonzima kwenye timu yao kwa sababu anatumiwa na Simba ili acheze chini ya kiwango ili klabu yao ifanye vibaya.

Kama ilivyo kwa Haruna, ndivyo ilivyokuwa inamtokea Ajib ambaye kundi kubwa la Wanasimba limekuwa likimshambulia kila wakati hasa timu inapopoteza pointi kwa madai kuwa mjeuri, dharau na kuleta mgawanyiko kwenye kikosi jambo linaloigharimu Simba.

Leo hii, walewale waliokuwa maadui wa Ajib na Niyonzima kwenye klabu hizo mbili ndio wanaotokwa mapovu na kupambana kwa hali na mali ili kuhakikisha nyota hao hawaendi upande wa pili.