NJE YA BOKSI: Saa nyingine kujifunga raha

Peter Kisaranga

Muktasari:

Chuki hizi za kishabiki ni za mbali sana na hubadilika kadri matokeo ya mpira uwanjani yanavyozidi kuwa bora.

KUNA msemo unaodai haki ya shabiki ni kushangilia ama kuzomea timu anayotaka. Mashabiki hasa wa klabu kuna wakati tumekuwa tukitamani timu zetu zipoteze pambano ili pengine mmoja wa wachezaji ama kocha awajibishwe.

Chuki hizi za kishabiki ni za mbali sana na hubadilika kadri matokeo ya mpira uwanjani yanavyozidi kuwa bora.

Mastori leo yanayotueleza pale hali inapokuwa ngumu kiasi mchezaji pia anataka apoteze mechi husika.

Januari 27, 1994 huko Barbados kulikuwa na michuano ya Caribbean Cup. Masharti ya michuano hiyo ilikuwa lazima kila mechi iwe na mshindi (hamna sare ya aina yoyote na kama pambano litaenda kwa dakika 30 za nyongeza goli litakalofungwa katika dakika hizo litamaliza pambano (sheria ya zamani ya sudden death ama ‘golden goal’).

Kama haitoshi bao hilo litahesabika kama mabao mawili kwa mfano sare ya bao 1-1 ikienda dakika za nyongeza yule atakayefunga bao la ushindi atahesabika kashinda kwa jumla ya mabao 3-1.

Pambano la hatua ya makundi lilikuwa kati ya wenyeji Barbados na Grenada, Barbados waliingia uwanjani katika mechi hiyo wakihitaji ushindi wa mabao mawili ama zaidi.

Mpaka dakika ya 83 Barbados walikuwa wakiongoza 2-0 hivyo kila kitu kilikuwa sawa kwa upande wao. Dakika moja baadaye sasa, yaani dakika ya 84 Grenada walipata bao, hivyo kufanya matokeo kuwa 2-1.

Kwa kutumia sheria ya michuano na kuona dakika hazitoshi beki wa Barbados aliamua kujifunga dakika ya 87 na kufanya matokeo kusomeka 2-2. Alifanya hivyo ili kubahatisha kupata bao katika muda wa dakika 30 za nyongeza ambalo lingewapa ushindi wa 4-2.

Grenada kwa kuwa na matokeo bora zaidi katika mechi za awali, hata kama wangepoteza kwa tofauti ya bao moja tu ingewatosha kufuzu hatua inayofuata.

Katika dakika tatu zilizosalia kabla ya mchezo huo kumaliza dakika 90, Grenada walicharuka na kujaribu kusaka bao kufunga ama kujifunga kadri nafasi itakapotokea. Huku Barbados wao wakizuia mabao yote mawili langoni yasiingie ili wapate sare ya kucheza dakika za nyongeza. Hatimaye mchezo ulimalizika kwa matokeo ya 2-2 na zikaongezwa 30 na kweli bwana Barbados wakafunga bao na matokeo kusomeka 4-2 na kusonga mbele wakiwaacha wapinzani wao wakishangaa.

Hakuna kokote ambapo mchezaji huwa anataka kufungwa langoni mwake, lakini katika michuano hiyo bwana Barbados waliitamani. Sijajua ikitokea kwa Simba na Yanga wachezaji waamue kujifunga uone moto wake. Tchao!

twitter: @PixiDeHaya