STRAIKA WA MWANASPOTI: Hivi Afrika Mashariki kulikoni Kombe la Dunia?

Tuesday November 14 2017Boniface Ambani

Boniface Ambani 

By Boniface Ambani, Nairobi

MBIO za kuwania nafasi kuiwakilisha Afrika katika fainali za Kombe la Dunia mwakani zitakazofanyika Urusi, zilifikia ukingoni wikiendi iliyopita tena kwa mshangao wa hali ya juu.

Kulikuwa na vita kali Afrika nzima wakati nchi tano zikikata tiketi ya kwenda kusimama kwa niaba ya bara zima la Afrika.

Kikosi cha Nigeria maarufu kwa jina la Super Eagles, kilifuzu kuwakilisha bara la Afrika Kwa mara ya pili mfululizo. Tunisia imefuzu kwa mara nyingine baada ya kufanya hivyo mwaka wa 2006.

Misri wamerejea katika mashindano hayo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1990. Nao Senegal wanarejea kwa mara ya kwanza pia tangu mwaka 2002. Msimu huu umerejesha timu ambazo zilikuwa zikisubiriwa kwa hamu kubwa.

Morocco wanarejea katika mashindano hayo tangu waliposhiriki mwaka wa 1998. Morocco walikuwa na kibarua kigumu sana kwani walihitaji ushindi ama sare katika mechi yao ya mwisho ambayo walikwenda ugenini dhidi ya Ivory Coast. Kipute kilipigwa jijini Abidjan.

Ilikuwa ni mechi ambayo walihitaji tu sare na juhudi zao zilizaa matunda kwani waliweza kuishinda Ivory Coast kwa mabao 2-0 ugenini. Ivory Coast wakiwa nyumbani kwao walihitaji ushindi wowote ule, lakini mambo yaliwaendea vibaya.

Walipata nafasi nzuri tu za kuweza kushinda hiyo mechi, lakini hawakuweza kuzitumia kwa ustadi. Walipoteza nafasi nyingi jambo ambalo mwishowe liliwagharimu pakubwa.

Gervinho na Wilfred Zaha walipoteza nafasi ambazo kwa kweli wangezitumia katika dakika za mwanzoni za mchezo huo, basi wangefuzu kwa mara ya nne mfululizo.

Morocco walipata nafasi na wakazitumia. Ilikuwa ni huzuni kubwa sana ndani ya Abidjan na nchi nzima kupokea kipigo cha mabao 2-0 nyumbani kwao.

Wakati hayo yakitendeka, Afrika Kusini pia walikosa nafasi ya kufuzu baada ya mechi ya marudio dhidi ya Senegal kumalizika kwa kipigo cha 2-0 nyumbani kwao.

Awali Afrika Kusini ilikuwa imeshinda, lakini Shirikisho la Soka la Kimataifa, Fifa, liliamua mechi hiyo iruduwe baada ya kuonekana mwamuzi alikuwa ameipendelea Afrika Kusini.

Alipatikana na makosa ya kuchukua hongo na hatimaye aliondolewa kwa orodha ya waamuzi wa mechi na kupigwa marufuku kabisa ya kushiriki katika shughuli ya uamuzi milele.

Mechi ilirudiwa na Senegal ikaibuka kuwa washindi na kufuzu. Kwa mantiki hiyo Senegal, Tunisia, Misri, Nigeria na Morocco ndizo zinakwenda Urusi zikiliwakilisha bara letu la Afrika.

Kinachoshangaza ni kwamba nchi zote hizo tano zinatoka Kaskazini na Magharibhi mwa Afrika. Ukanda wetu wa Afrika Mashariki tumeendelea kuwa kichwa cha mwendawazimu. Ni kitu gani kinafanya hatuwezi piga hatua? Uganda ‘The Cranes’ nusura watuwakilishe kabla ya hesabu zao kuwagomea dakika za mwishoni. Ndugu zanguni tutakuwa tunasindikiza wenzetu hadi lini? Shida yetu imeendelea kuwa ile ile kwani tuna matayarisho duni sana. Kwa sasa tunatakiwa kuanza kuweka mipangilio ya kuona vile tunafuzu Kombe la Dunia 2022 kwa 2022 ambalo litafanyikia Qatar.

Bahati mbaya sisi huanza matayarisho kwa kuchelewa halafu tunataka kutumia njia za mikato kufuzu.

Matayarisho yanafaa kuanza saa hizi. Vikosi ambavyo tunatarajia kutuwakilisha tunafaa kuwa tunaviunda saa hizi. Wacheze pamoja, mazoezi wafanye pamoja kwa wingi, tuangalie ni umri gani tunahitaji, na wakati 2022 utafika hicho kikosi kitakuwa tayari kuwajibika?

Shida yetu kubwa ni hiyo. Matayarisho yanafaa kuanza sasa hivi. Bila hivyo yatakuwa yale yale ya abunuwasi.

Kanda hili letu ni lazima iamke. Hakuna vile tutafikiria kufuzu Kombe la Dunia, ilihali hata kufuzu katika Kombe la Afrika hatuwezi. Itakuwa ni ndoto kubwa sana.

Mikakati inafaa ianze sasa. Uganda, Kenya, Tanzania, Rwanda, Burundi, sote tunafaa kufikiria. Tutafute shida iko wapi ili tuifanyie kazi. Mara ya Mwisho Kenya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ilikuwa kitambo sana.

Vile vile Tanzania. Juzi tu tukapewa Chan (fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani), bado hata hatukuwa tayari kuandaa mashindano hayo.