INAWEZEKANA: Real Madrid, nguvu zote kuzielekeza Ulaya

Tuesday March 13 2018Olle Bergdahl Mjengwa

Olle Bergdahl Mjengwa 

MSOMAJI, wiki iliyopita Real Madrid walionyesha tena kwa nini wao ni klabu ambayo imeshinda Ligi ya Mabingwa mara nyingi zaidi katika historia ya soka.

Kama ilivyo katika mashindano mengi, Madrid walionyesha kwamba uzoefu ni kitu muhimu sana katika soka na si jambo la kushangaza kwamba Real Madrid wameweza kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa na kuwatoa Paris Saint Germain.

Hakika, Real Madrid wamekuwa na msimu ambao wangependa kuusahau katika Ligi Kuu ya Hispania na hali yao mbaya kimpira imesababisha wengi kutokuamini kwamba mabingwa hao wa Ulaya wana uwezo wa kufika mbali katika Ligi ya Mabingwa msimu huu.

Lakini, ni muhimu kukumbuka kwamba Real Madrid walipoteza pointi nyingi sana mwanzoni mwa msimu huu na nafasi yao ya tatu katika Ligi Kuu huenda si kipimo kizuri cha kiwango cha timu hiyo.

Real Madrid wana kati ya wachezaji bora zaidi duniani katika kila nafasi lakini msimu uliopita nyota wao, Cristiano Ronaldo ndiye aliyeibeba timu hiyo mpaka fainali alipofunga magoli katika mechi nne mfululizo kuanzia robo fainali.

Msimu huu, fomu kali ya Ronaldo katika Ligi ya Mabingwa imeendelea na mchezaji huyu amefunga magoli mengi zaidi katika Ligi ya Mabingwa mpaka sasa akiwa na magoli kumi na mbili.

Bila shaka Ronaldo hivi sasa yupo katika hali nzuri sana kimpira na ana uwezo wa kuwapeleka Real Madrid fainali nyingine katika Ligi ya Mabingwa kwa juhudi zake mwenyewe.

Pia, kutokana na kuona hali halisi kwamba Real Madrid hawana uwezo wa kushinda Ligi Kuu ya Hispania,

Kocha wa timu hiyo, Zinedine Zidane atakuwa na uwezo wa kuwapumzisha wachezaji wake tegemeo katika Ligi Kuu kabla mechi za Ligi ya Mabingwa.

Yumkini, baadhi ya wachezaji katika kikosi cha Real Madrid hawapo katika ubora wao kama zamani msimu huu, mathalan Benzema na Gareth Bale.

Lakini, msimu huu vilabu vingi vikubwa barani Ulaya hawana vikosi vyenye kutisha sana na kwa kuwatoa Paris Saint Germain, Real Madrid sasa wameonyesha kwamba wana uwezo wa kuifunga timu yoyote iliyobaki katika michuano hii.

Kutokana na kushinda Ligi ya Mabingwa msimu uliopita, Real Madrid ni timu ya kwanza kushinda michuano hii mara mbili mfululizo.

Hakika sitashangaa kama wanavunja rekodi yao na kushinda Ligi ya Mabingwa kwa mara ya tatu mfululizo.