Ramsey amekuwa yatima Emirates

YATIMA Aaron Ramsey. Huna namna nyingine zaidi ya kumwita hivyo. Wakati wa uhai wa baba yake huko Emirates, Ramsey asingekuwa mtu wa kuchagua moja, ama kusaini au kuondoka.

Chini ya Arsene Wenger, Ramsey asingekuwa na huo msamiati wa kuchagua. Angesaini tu. Hakuna, asiyelifahamu hilo, Ramsey alikuwa kipenzi cha Kocha Wenger huko Emirates. Lakini, ndio hivyo, maisha yamebadilika na yanaonekana kwenda kasi kweli kweli kwa upande wa Ramsey.

Hivi unavyosoma hapa, Ramsey si mchezaji muhimu tena huko Arsenal. Kwa sasa huko Arsenal, kuna kocha mpya, kuna sura mpya. Kuna ari mpya. Kuna nguvu mpya na kasi mpya. Hakuna tena kung’ang’ania yale ya zamani yasiyokuwa na faida.

Hivyo ndivyo maisha yanavyokwenda kasi kwa Ramsey. Kocha mpya, Unai Emery ameonyesha kuziamini sura mpya alizozileta. Amemleta Stephan Lichtsteiner. Amemleta pia Sokratis Papastathopoulos. Amekuja na kipa Bernd Leno na kiungo Lucas Torreira. Utamaduni wa Arsenal sasa unakuwa mpya. Hakutakuwa na ile desturi ya kupigapicha vipicha kwenye vyumba vya kubadilishia kisa umeshinda mechi kubwa. Watu wazima na akili zao kama Sokratis na Lichtsteiner watasimamia zaidi mataji na si kufurahia kushinda mechi kama umebeba ubingwa. Emery ni wa mtazamo mwingine. Kama amethubutu kumfungia mlango, Jack Wilshere, hawezi kuona ugumu wa kufanya hivyo kwa Aaron Ramsey. Maisha yamebadilika. Ramsey anapaswa kufahamu nyakati si zile tena. Arsenal ya Emery haiogopi kufanya usajili.

Kwa sasa wanahusishwa na usajili wa pesa nyingi kumnasa Ousmane Dembele kutoka Barcelona.

Dembele akija Emirates, Ramsey hatakuwa na la kufanya zaidi ya kufahamu tu, atakuwa rafiki wa benchi msimu ujao. Hizi ni zama za Emery. Huku nyuma chini ya Wenger, maisha ya Arsenal yalikuwa yenye kutabirika. Ramsey lazima acheze labda kama atakuwa mgonjwa. Emery si hakubali Ramsey, la anamkubali na ndio maana mara mbili nzima, alimpa kitambaa cha unahodha kwenye mechi za kujiandaa na msimu mpya.

Lakini tofauti Emery na Wenger ni moja, ipo kwenye mabadiliko. Emery hana kawaida ya kukariri, si kama Wenger. Ndiyo maana hakitakuwa kitu kigumu kwa Mhispaniola huyo kufungua milango ya kumwaachia kiungo huyo. Emery aliwafikiria zaidi Adrien Rabiot na Steven Nzonzi, akitaka kuungana na viungo wake hao wa zamani aliowahi kuwanoa PSG na Sevilla. Kwa Emery hakuna kurudi nyuma tena. Ramsey ana jambo moja, kusaini au kuondoka kufuata njia waliyopita wenzake, Jack, Ox na Theo.