Ni muda mwafaka kwa viongozi wa TFF kujitathimini

Muktasari:

  • Hata hivyo, jambo pekee la msingi ambalo binadamu aliyekamilika anapaswa kulifanya pindi anapofanya makosa ni kuomba radhi na kujirekebisha na kuhakikisha hafanyi tena kosa kama hilo au linalofanana nalo.

HAKUNA mwanadamu aliyekamilika, hivyo ufanyaji wa makosa ni jambo la kawaida katika maisha yetu ya kila siku tunayoishi hapa duniani

Hata hivyo, jambo pekee la msingi ambalo binadamu aliyekamilika anapaswa kulifanya pindi anapofanya makosa ni kuomba radhi na kujirekebisha na kuhakikisha hafanyi tena kosa kama hilo au linalofanana nalo.

Kujirekebisha huko kunaweza kuwa ni kwa kuwashughulikia wale waliosababisha makosa hayo au kujiweka pembeni na kuwapisha wengine kama unahisi uwezo wako wa kusimamia kitu umeisha.

Inapotoke mtu anafanya makosa yaleyale kila siku bila kuonyesha kutobadilika au kuchukua hatua stahiki kwa makosa yanayojitokeza kama ya upangaji wa matokeo kwenye michezo ya mwisho ya Kundi C la Ligi Daraja la Kwanza (FDL), sakata ambalo lilizihusisha timu za JKT Oljoro, Kanembwa JKT, Geita Gold na Polisi Tabora anatakiwa kuachia ngazi.

Licha ya TFF kuchukua uamuzi wa kuzishusha timu hizo nne, huku pia ikitoa adhabu kali kwa wote waliothibitika kushiriki kwenye suala hilo la upangaji matokeo, baadhi ya viongozi wa klabu hizo zilizokutana na rungu waliibuka hadharani na kudai kuwa wapo viongozi wa juu kabisa wa shirikisho ambao walishiriki moja kwa moja katika upangaji matokeo.

Sakata hilo lilikolezwa na kusambaa kwa sauti iliyorekodiwa ya watu inaodhaniwa kuwa maofisa wa TFF, wakipanga mikakati ya kupanga matokeo huku shirikisho likikanusha suala hilo. Wakati hilo halijapoa, TFF iliingia tena lawamani kwa kuingilia mchakato wa uchaguzi wa klabu ya Yanga baada ya kamati yake ya uchaguzi kujipa mamlaka ya kuendesha zoezi hilo badala ya kusimamia kama walivyoagizwa na Wizara ya Michezo kupitia Baraza la Michezo Tanzania (BMT).

Ikumbukwe kuwa hilo lilisababisha Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji aliyefanikiwa kutetea nafasi hiyo kwa mara nyingine, kushusha tuhuma nzito kuwa ndani ya TFF kuna njama za kumhujumu huku akipeleka vithibitisho mbele ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) .

Upepo huo wa uchaguzi wa Yanga ulipita na kumbukumbu inaonyesha kuwa, uongozi wa TFF ulikutana na ule wa Yanga kwa ajili ya kuweka mambo sawa.

Kabla hilo halijapoa, TFF tena wiki moja iliyopita, ililaumiwa kwa kuingilia mchakato wa uchaguzi kwenye timu ya Stand United pamoja na ule wa Chama cha Soka Wilaya ya Kinondoni (Kifa).

Juzijuzi tu tulisikia viongozi wa timu za Makumbusho FC na Stand Bagamoyo zikilitupia lawama shirikisho kwa kushindwa kushughulikia rufaa zao walizokata kwenye Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL).

Na juzi kumeibuka malalamiko mengine kutoka kwa klabu ya Yanga ikilituhumu shirikisho kwa kutowalipa fedha zao za ubingwa wa Kombe la Shirikisho (FA) ambalo waliibuka mabingwa baada ya kuifunga Azam FC mabao 3-1.

Nimekuwa muumini mkubwa wa kutohukumu kwa kusikiliza kauli za upande mmoja. Ni lazima pande zote zilizopo kwenye mzozo zisikilizwe ili hukumu inayotoka iwe ya haki.

Baada ya kufanya tathmini yangu juu ya mizozo yote hiyo inayoihusu TFF, nikubaliane na mawazo na mitazamo ya kundi kubwa la wapenzi wa soka nchini kuwa TFF ya sasa imepoteza dira na hata mwelekeo.

Hakuna namna yoyote ambayo TFF inaweza kutuaminisha kuwa hizo kashfa na tuhuma zote ni za kusingiziwa na kulipaka matope shirikisho hilo.

Ukichunguza kwa umakini, utakubaliana nami kuwa, TFF haiwezi kukwepa kwa namna yoyote ile kuingia kwenye lawama kwani kuna ishara za wazi za jinsi watendaji wake walivyohusika nazo.

Hata pale ambako watendaji wake hawakuhusika, TFF haikuchukua hatua stahiki za kuzuia matatizo hayo yasitokee.

Kwenye haya malalamiko ya Yanga kutopewa fedha zao za ubingwa, sikutegemea majibu mepesi kutoka kwa TFF kuwa eti Yanga na timu zinazodai zote, ziende makao makuu ya shirikisho hilo kudai pesa zao badala ya kulalamika kwenye vyombo vya habari.

Ni jambo la kushangaza kwa sababu wadhamini ambao ni Kampuni ya Azam Media ilishakabidhi fedha zote za udhamini mapema, hivyo ilipaswa siku ya mchezo wa fainali, washindi wote wakabidhiwe zawadi zao palepale uwanjani.

Umefika wakati sasa kwa watendaji wa TFF, kujitazama wao wenyewe na kuona kuwa wanawajibika kwa madudu yanayotokea kila kukicha ndani ya shirikisho hilo.

Kama kuna kirusi ambacho wanahisi ndicho chanzo cha uozo wote unaotokea kila siku, ni muhimu sasa wakakishughulikia kwa kukiondoa ndani ya shirikisho na kama wakishindwa basi wawapishe wale ambao wataweza kurudisha hadhi ya mpira wetu.

Kwa haya yanayotokea hivi sasa, ni wazi kuwa yanakatisha tamaa wadhamini ambao wamekuwa wakitoa fungu kubwa la pesa kwa ajili ya kuendeleza soka letu.

Kitakachotokea siku za usoni ni wadhamini na wadau wa soka kuamua kukaa pembeni ili kunusuru fedha zao kwa sababu ya upuuzi wa watu wachache wasiojitambua, jambo litakalosababisha soka letu kuzidi kudorora.

Kama kweli shirikisho linachoshwa na kashfa zinazoibuka kila kukicha dhidi yake, imefika wakati sasa kwa kuchukua uamuzi mgumu wa kuondoa magugu yote ili liweze kurudisha imani ya wapenzi wa soka.

Kama hilo litashindikana, basi ni ishara tosha kuwa viongozi wake wameshindwa kutimiza jukumu la kusimamia soka letu na wote wakae pembeni kupisha wenye nia ya dhati ya kutimiza hilo.

0713 923276