NJE YA BOKSI: Utamu wa soka upo kwenye namba

Muktasari:

Hii ni kwa sababu ubingwa huenda sawia na matokeo mazuri uwanjani yaani soka bwana yanaenda sambamba na mambo ya namba.

LEO ikitokea mchambuzi yeyote wa soka akasimama na kusema kuwa, matokeo mazuri katika soka sio ya muhimu sana kama ubingwa, sidhani kama haitakuwa rahisi kwake kueleweka mbele za wadau wa mchezo huo.

Hii ni kwa sababu ubingwa huenda sawia na matokeo mazuri uwanjani yaani soka bwana yanaenda sambamba na mambo ya namba.

Lakini pia hakuna shabiki atakayejali sana kama timu yake itatwaa ubingwa, licha ya kuwa na matokeo yasioridhisha. Kwa sababu ubingwa ni mtamu kivyovyote.

Mfano wa karibu ni klabu ya Huddersfield Town iliyofanikiwa kupanda Ligi Kuu England (EPL), licha ya kuwa na tofauti ya mabao mawili hasi (-2).

Mastori ya leo yanatupeleka sehemu mbalimbali ambapo tunaweza kusema ubingwa umepatikana bila matokeo chanya kama mashabiki tunavyopenda.

Katika Ligi Kuu huko Ghana msimu wa mwaka 2009/10, bingwa Aduana Stars alishinda taji la ligi hio kwa kufunga jumla ya mabao 19 tu katika michezo 30 waliocheza. Yaani walikuwa na wastani wa goli 0.63 katika kila mechi. Timu ya karibu zaidi katika kufunga mabao machache msimu huo ilikua ni Bechem Chelsea waliofunga mabao 26 ambayo hayakuiokoa kushuka daraja. Kama haitoshi Aduana Stars walikuwa wakishiriki Ligi Kuu Ghana kwa mara ya kwanza.

Nchini Uturuki Ligi Kuu mwaka 1979/80, bingwa Trabzonspor alifunga magoli 25 kwenye mechi 30 walizocheza, yaani wastani wa mabao 0.83 katika kila mechi.

Ubingwa wa kihistoria walioupata Klabu AIK ya nchini Sweden mwaka 1998. AIK walishinda michezo 11 na kutoa suluhu michezo 13 (kati ya michezo 26 ya ligi hiyo).

Walifanikiwa kufunga magoli 25 tu na kufungwa jumla ya magoli 15, hivyo kutwaa ubingwa wakiwa na wastani wa magoli 0.92. AIK ndio timu iliyofunga mabao machache zaidi msimu huo licha ya kutwaa ubingwa.

Bingwa wa Ligi Kuu nchini Brazil mwaka 1985, FC Coritiba alishinda michuano hiyo akiwa na tofauti ya mabao hasi 2. Baada ya kufunga mabao 25 na kuruhusu kufungwa mabao 27 katika michezo 30 sawa na wastani wa goli 0.86. Hiyo pekee inaonyesha kuwa soka ni mchezo wa namba.

Peter kisiraga

twitter: @PixiDeHaya

instagram: peter_kisiraga

phone; 0626919015