ROHO NYEUPE: Msuva ameipuuza sauti ya shetani na kwenda mbele

NI nani awezaye kuipuuza sauti ya shetani? Ni wachache sana. Winga Simon Msuva amefanikiwa kuipuuza sauti ya shetani na kukubali kwenda kuanza maisha mapya kwenye klabu ya Difaa EL Jadida ya Morocco. Inahitaji ujasiri sana.

Sauti ya shetani ina nguvu usiambiwe na mtu. Umewahi kujiuliza inakuwaje msichana aliyekuwa anakusumbua kwa muda mrefu, anakupigia simu wakati ukiwa na hela? Unabaki ukijiuliza amefahamu vipi kuwa nina hela? Sasa fahamu huyo hupewa mtonyo na sauti ya shetani.

Sauti ya shetani ina kawaida ya kukatisha tamaa na kutia hasara. Ukitaka kuondoka sehemu ili kwenda kuanza maisha mengine sauti hiyo hukujia na kukujaza hofu kubwa. Ndivyo ilivyokuwa kwa Msuva ambaye ameacha fahari kubwa ya kucheza Yanga na kwenda kujaribu maisha nchi za watu.

Asikwambie mtu, kufanya uamuzi kama wa Msuva inahitaji moyo wa chuma. Kwanza ni kupambana na hofu ndani yako. Kuna hofu kubwa zimewajaa wachezaji wa Simba na Yanga, wanafikiria sana ugumu wa kupata ufalme kwingineko kama walivyofanikiwa hapa.

Msuva anaondoka Yanga akiwa shujaa mkubwa. Mashabiki wa Yanga roho zinawauma. Viongozi wa Yanga roho zinawadunda, kila mmoja alitamani abaki. Shabiki mmoja wa Yanga aliniambia anatamani Msuva afeli vipimo vya afya huko anakokwenda ili arudi kuichezea timu yao. Nikamwambia pepo lako na lishindwe.

Msuva mwenyewe amejipambanua kuwa mchezaji mahiri ndani ya Yanga na alikuwa na maisha mazuri klabuni hapo. Yanga ilimlipa vizuri na mashabiki walimpa zawadi za kutosha. Alipotembea mtaani jina lake liliimbwa kila kona.

Mwanadamu anahitaji sifa gani zaidi ya hii? Hakuna maisha matamu kama ya kusifiwa na kutukuzwa. Ni maisha fulani ya kiungu ambayo siyo rahisi kwa mtu kuyaacha na kwenda kuanza upya kwingineko.

Ukitaka kwenda shetani anakupa hofu kali. Anakuonyesha tena ufahari wako hapo ulipo ili tu ukate tamaa ya kusonga mbele. Msuva ameipuuza sauti hii na kujivika moyo wa ujasiri ili aweze kusogea mbele kidogo.

Wakati fulani baada ya mchezo dhidi ya Zanaco nilimuuliza Msuva juu ya nia yake ya kwenda kucheza nje. Nilimuuliza haoni huu ni wakati mwafaka kwake kuondoka? Alichonijibu ndicho alichofanya sasa. Mwanaume wa kweli huishi kwa ndoto zake.

Kwenda kuanza maisha sehemu nyingine kunahitaji kujipanga pia. Msuva alikuwa na nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza cha Yanga lakini sasa anakwenda kupambania nafasi katika timu mpya.

Timu hiyo ya Al Jadida licha ya kwamba imemsaini, lakini bado inataka kuona uwezo wake uwanjani ili kujiridhisha upya. Msuva ataanza upya kujihakikishia nafasi katika kikosi cha kwanza, siyo kazi rahisi.

Ni kazi inayomkabili mchezaji yeyote mpya. Mbwana Samatta alipotoka TP Mazembe alikuwa mchezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza lakini baada ya kufika KRC Genk alilazimika kuanza kupambana kujihakikishia nafasi katika kikosi cha kwanza.

Ni wachezaji wachache sana wanaokwenda na kuingia moja kwa moja katika kikosi cha kwanza. Wengi wanalazimika kupambana kwanza kuthibitisha uwezo wao.

Pamoja na changamoto zote hizo, nina imani kubwa na Msuva. Nina imani hizi changamoto kwake ni za kawaida na ataweza kuzivuka na kufanya vizuri. Silaha yake kubwa itaendelea kuwa kasi yake pamoja na uwezo wake mkubwa wa kufunga.

Msuva hajawahi kuniangusha na sina mashaka kamaataniangusha huko Morocco. Mabao yake matamu aliyokuwa akifunga pale Uwanja wa Taifa yatahamia pale Morocco sasa. Lile soka lake la kujitolea kwa moyo wote litahamia pia huko.

Ninachotamani kwa Msuva aweze kuvuka hatua moja zaidi. Morocco ipo karibu sana na Hispania. Kuna baadhi ya maeneo ya Morocco ni kama yapo Hispania, hivyo Msuva ni kama amekaa nje ya lango la kuingia Ulaya.

Hii ndiyo njia anayotakiwa kuiendea pindi akitoka Morocco. Kutoka Morocco kwenda Ulaya ni karibu kama kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro. Nisingependa kuona anarudi nyuma na kushindwa kupata hata timu za daraja la kwanza Ulaya.

Mwisho wa yote pia nimpongeze na Abdi Banda pia kwa kuipuuza sauti ya shetani. Banda alipanga kwenda Afrika Kusini lakini sauti ya shetani ilitaka kumbakisha Simba.

Alipata ushawishi mkubwa na vikwazo vingi lakini mwisho wa siku amevipuuza vyote na kujiunga na Baroka FC.

Hakuna ujasiri mkubwa kama huu. Hakuna ujasiri mkubwa kwa mwanaume kama kuipuuza sauti ya shetani. Kama unabisha, jiulize ukiwa na hela halafu msichana mrembo unayemtamani akikuomba utamnyima? Majibu unayo lakini nakusihi usipende kusikiliza sauti ya shetani.