Mastaa 10 wamepiga pesa ndefu England

WANASEMA wajinga ndio waliwao! Usibishe nakwambia.

Ni hivi, unaambiwa usajili wa mastaa 10 ambao unaonekana kuwa na nguvu zaidi kwenye Ligi Kuu England, hakuna hata mchezaji mmoja aliyewahi kusajiliwa kwa walau Pauni 13 milioni tu wakati waliponaswa na timu zao za zamani, walipotua England, mkwanja uliotumika kuwanasa ni kufuru.

Karibu Pauni 500 milioni zimetumika kuwasajili wachezaji hao kwenye dili zao za kutua kwenye Ligi Kuu England, wengine wakiweka rekodi kwenye usajili, kitu ambacho hakikuwa huko nyuma, kwani walinaswa kwa pesa kidichu sana.

Wachezaji hao10, kabla ya kuhamishwa kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi huko Ulaya, thamani yao kwa jumla ilikuwa Pauni 72.6 milioni, lakini hivi unavyosoma hapa, thamani yao imekuwa zaidi ya Pauni 500 milioni, ikiwa ni zaidi ya mara saba ya thamani ya awali.

Chelsea ilimnasa kipa Kepa Arrizabalaga kwa pesa iliyovunja rekodi ya uhamisho kwa makipa baada ya kuilipa Athletic Bilbao, Pauni 71 milioni, wakati Mhispaniola huyo anatua Bilbao, alinaswa bure kabisa.

Manchester City ilikwenda Leicester City kuinasa huduma ya supastaa, Riyad Mahrez kwa Pauni 60 milioni, wakati ada yake ya awali wakati anatua King Power, staa huyo wa Algeria alisajili kwa Pauni 400,000 tu.

Wababe wa Anfield, Liverpool walifanya usajili wa mastaa watatu katika dirisha hili la majira ya kiangazi, wakimnasa kiraka Fabinho, kipa Alisson Becker na kiungo Naby Keita, ambao kwa ujumla wake wamewagharimu vijana hao wa Jurgen Klopp mkwanja wa Pauni 154 milioni, wakati ada ya jumla ambayo walilipiwa wachezaji hao kabla ya kutua Anfield ilikuwa Pauni 23.3 milioni.

Fabinho amenaswa kwa Pauni 39 milioni na Liverpool, lakini huko Monaco alikotokea alisajiliwa kwa Pauni 4.3 milioni. Alisson amenaswa kwa Pauni 65 milioni, lakini AS Roma ilipomsajili ililipa Pauni 6.7 milioni na Keita ametua Anfield kwa Pauni 50 milioni, wakati RB Leipzig yenyewe ilimnasa kwa Pauni 12.3 milioni tu.

West Ham United imemsajili Felipe Anderson kutoka Lazio kwa Pauni 36 milioni, lakini staa huyo, uhamisho wake alionaswa huko nyuma kabla ya kujiunga na wababe hao wa Ligi Kuu England ilikuwa Pauni 6.7 milioni.

Chelsea ilifanya uhamisho mwingine kwenye dirisha hilo la majira ya kiangazi na ilimnasa kiungo Jorginho kwa Pauni 57 milioni, lakini staa huko akiwa Napoli alikotokea, alisajiliwa kwa Pauni 8 milioni tu.

Everton yenyewe ilitumia Pauni 87 milioni kuwanasa wakali Yerry Mina na Richarlison kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi, ikilipa Pauni 27 milioni kwenye usajili wa Mina na Pauni 50 milioni.

Lakini huko alikotoka Mina ambako ni Barcelona alilipiwa Pauni 10.4 milioni na Richarlison huko alikotokea Watford, alisajiliwa kwa Pauni 11 milioni tu.

Usajili mwingine wa pesa nyingi kwa mchezaji ambaye huko nyuma ada yake ya usajili wakati ananaswa haikufika hata Pauni 13 milioni ni kiungo wa Kibrazili, Fred, aliyenaswa na Shakhtar Donetsk kwa Pauni 12.8 milioni na kuuzwa Man United kwa Pauni 47 milioni.