Mapengo ya kila timu Top Six

DIRISHA la usajili kwenye Ligi Kuu England litafungwa leo Alhamisi. Lakini kuna timu kibao hazikamilisha bado kufanya marekebisho kwenye vikosi vyao, ikiwamo vigogo wa Top Six kwenye ligi hiyo.

Wakati dirisha likifungwa haya hapa maeneo ambayo kila klabu ya Top Six katika Ligi Kuu England inapaswa kuyafanyia kazi na kusajili kabla ya dirisha kufungwa rasmi usiku wa leo.

Arsenal - beki wa kushoto

Arsenal imefanya usajili wa akili tu kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi ambapo kocha mpya Unai Emery amesajili kisomi. Lakini, shida bado imebaki kwenye jambo moja tu, inahitaji beki wa kushoto.

Nacho Monreal kwa sasa umri wake unazidi kuwa mkubwa na Sead Kolasinac, aliyeanza vizuri bado ameonekana kuwa na shida kwenye baadhi ya mechi. Eneo jingine ambalo Emery atahitaji kulirekebisha ni kwenye kiungo mkabaji, ambapo hapo anapiga hesabu za kumnasa Steven Nzonzi.

Lakini hilo la Nzozi kuja Arsenal haliwezi kutimia kama haijampiga bei Aaron Ramsey.

Wachezaji ambao Emery hadi sasa ameshawanasa ni Stephan Lichtsteiner, Bernd Leno, Sokratis Papastathopoulos, Lucas Torreira na Matteo Guendouzi.

Chelsea - beki wa kati, kiungo na straika

Kuchelewa kumfukuza Antonio Conte na kuteua mrithi wake, Maurizio Sarri kumeifanya Chelsea kuwa na mapengo mengi ya kujaziba wakati dirisha lenyewe la usajili likifika tamati hii leo.

Msimu uliopita, Chelsea ilimaliza kwenye nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu England, hivyo itahitaji kucheza kwa kiwango bora sana msimu huu ili kurudi kwenye Top Four na kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Kocha Sarri anahitaji beki wa kati, kiungo mmoja matata na straika. Kwenye kiungo ilimnasa Jorginho, lakini bado kuna shida kwenye straika, ambapo inamsaka Robert Lewandowski na beki ya kati kuna pengo inalopaswa kuliziba pia.

Liverpool - Namba 10

Jurgen Klopp amemwaga pesa za kutosha kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi kuboresha kikosi chake cha Liverpool, ambapo aliwanasa viungo wawili wa kati, mshambuliaji mmoja na kipa.

Lakini kama kuna eneo ambalo Klopp anapaswa kulitafutia suluhisho la haraka kabla ya dirisha la usajili kufungwa basi ni la kiungo mshambuliaji mwenye uwezo wa kucheza Namba 10. Liverpool ilihitaji huduma ya Nabil Fekir kuja kucheza kwenye eneo hilo, lakini mambo yaligoma, ikashindwa kumnasa.

Tangu Philippe Coutinho alipoondoka, Liverpool bado haijapata namba 10 wa maana na matokeo yake imekuwa tu ikimchezesha Alex Oxlade-Chamberlain.

Wachezaji iliowanasa kwenye dirisha hili ni Naby Keita, Fabinho, Xherdan Shaqiri na Alisson Becker.

Man City - kiungo mkabaji

Pep Guardiola amemnasa mchezaji wake aliyekuwa akimhitaji kwenye kikosi cha Manchester City, Riyad Mahrez, lakini ameshindwa kumnasa staa mwingine aliyekuwa akimsaka, kiungo wa kukaba Jorginho, ambaye ameamua kujiunga na Chelsea.

Kutokana na hilo, Man City bado ina pengo kwenye sehemu hiyo ya kiungo, hivyo inahitaji kusajili mchezaji wa kushindania namba na Fernandinho, ambaye alionekana kuwa na uchovu kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018 huko Russia.

Mchezaji inayemsaka ni Mateo Kovacic wa Real Madrid. Kwenye dirisha hili imeshawanasa Riyad Mahrez, Claudio Gomes na Philippe Sandler.

Man United - winga na beki wa kati

Jose Mourinho anahitaji wachezaji wawili kwenye kikosi chake kukifanya kuwa imara zaidi. Anahitaji beki wa kati na winga wa kulia na hilo likifanyika kabla ya dirisha hili kufungwa leo Alhamisi, basi atakuwa amefanikiwa kwa kiwasi kikubwa.

Mastaa Juan Mata, Jesse Lingard na Marcus Rashford wanaweza kucheza upande huo wa kulia, lakini ukweli anahitaji winga wa kiwango cha dunia.

Nafasi nyingi inayohitaji marekebisho ni kwenye beki ya kati na ndiyo maana timu hiyo imekuwa ikihusishwa na wakali Yerry Mina, Harry Maguire na Toby Alderweireld.

Tottenham - kiungo wa kati

Kocha Mauricio Pochettino anahitaji kiungo mmoja wa kati matata sana ambaye atamhakikishia ufiti na si kuwategemea Victor Wanyama, Mousa Dembele na Harry Winks ambao mara kwa mara wamekuwa kwenye wodi ya wagonjwa. Lakini pia kikosi hicho kinahitaji beki wa kati kuchukua nafasi ya Toby Alderweireld kama atakwenda Manchester United. Viungo inawasaka ni Jack Grealish, Abdoulaye Doucoure na Lewis Cook huku inaweza kuingia sokoni kumnasa winga Anthony Martial.