Mambo 5 kumbeba Pluijm pale Azam

Hans Van Pluijm

Muktasari:

  • Kocha mpya wa Azam FC, Hans Van Pluijm bado yuko safarini. Safari ya soka aliyoianza miaka zaidi ya 40 iliyopita hadi sasa akiwa anakwenda kuifundisha Azam.

SAFARI yoyote ya mafanikio huanzia mwanzo kabisa, kujipanga. Japokuwa hakuna safari isiyo na mwisho, lakini kila safari ina changamoto zake na mafanikio.

Kocha mpya wa Azam FC, Hans Van Pluijm bado yuko safarini. Safari ya soka aliyoianza miaka zaidi ya 40 iliyopita hadi sasa akiwa anakwenda kuifundisha Azam.

Kwa kifupi tu, safari yake imekuwa na changamoto pamoja na mafanikio kutokana na alikopitia.

Kazi ya ukocha alianza akiwa na klabu ya FC Den Bosch, Excelsior, Obuasi Goldfields, Heart of Lions, Ashanti Gold, Young Africans, Singida United na sasa Azam FC.

Kocha huyu alitua nchini akianzia Yanga msimu wa 2014 hadi 2016 akiipa mafanikio kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara mbili. Akaifikisha hatua ya Makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mara moja na Ngao ya Hisani mara moja.

Baada ya hapo, alitua Singida United alikoipa mafanikio kiasi ikiwa ndio imepanda daraja kutoka Ligi Daraja la Kwanza. Aliifikisha fainali ya Kombe la FA msimu uliopita ikiwa ni msimu wake wa kwanza akiisaidia pia kubaki Ligi Kuu ikimaliza katika nafasi tano bora.

Ni wazi timu anayokwenda kocha huyu wa kwanza wa kigeni aliyepata mafanikio na mwenye uzoefu na ligi ya Tanzania kuliko wengine ni sahihi. Azam ni klabu ambayo ina kila kitu ambacho sio kocha tu hata wachezaji vinaweza kuwasaidia katika kuyapata mafanikio.

Mwanaspoti linakuletea mambo matano ambayo kocha huyu atayakuta Azam na hakika kama mambo yakienda kama atakavyo, mafanikio Azam ni lazima.

Miundombinu wapo vizuri

Unataka nini zaidi ukifika pale Azam. Miundombinu? Hapo usiulize. Kocha Pluijm hatakuwa na shaka juu ya miundombinu kwani Azam imekamilika kwenye idara hii.

Azam ina viwanja vya mazoezi, gym ya kisasa, pamoja na bwawa la kuogelea katika kuwafanya wachezaji wawe fiti.

Tofauti na Yanga na Singida United ambazo zinakosa mambo muhimu kama hayo, Pluijm ambaye ni muumini mkubwa wa mazoezi hawezi kuwa na kisingizio hili. Akiwa Yanga na Singida, timu zilikuwa zikifanya mazoezi katika viwanja ambavyo alishawahi kukiri haviendani na aina ya wachezaji wake kutokana na ubovu.

Uwezo wa kifedha

Hakuna asiyejua Azam ndio klabu tajiri zaidi katika ukanda huu wa Afrika Mashariki. Inamilikiwa na bilionea, Said Salim Bakhresa mmiliki wa Kampuni ya Azam. Sasa jiulize, Azam FC inakosaje pesa?

Ukiwa Azam huwezi ukawa na tamaa ya pesa, ni vigumu kusikia mchezaji wa Azam amehongwa au kuuza mechi kisa pesa. Azam pesa ipo. Pluijm anaenda Azam akijua wazi atafanikiwa kutokana na pesa iliyo nayo klabu na wenyewe wanataka mafanikio.

Wachezaji wengi hujikuta wakishindwa kufika mazoezini sababu kubwa ikiwa ni kutokulipwa mishahara na hivyo kuwafanya makocha kushindwa kuendana na hali hiyo na kuamua kukimbia, mfano ni Kocha Mzambia, George Lwandamina ambaye aliamua kukimbia kutokana na timu kukosa pesa ya kumwezesha yeye pamoja na wachezaji kuwa na ari ya kujituma.

Usajili

Imezoeleka kwa timu kubwa hasa za Simba na Yanga suala la usajili husimamiwa na Kamati za Usajili pamoja na viongozi. Wao ndio huamua wachezaji wa kuwasajili jambo ambalo ni kinyume na timu nyingine kubwa, makocha ndio wenye jukumu zima la kutafuta na kusajili wachezaji.

Pluijm anatarajiwa kuanza kibarua chake msimu ujao na tayari Azam imeshaanza huku usajili huku kazi hiyo akiifanya yeye mwenyewe kwa kupendekeza ni wachezaji gani wasajiliwe watakaomsaidia kuipa mafanikio klabu.

Uongozi wa Azam umempa uhuru kocha huyo kuhakikisha anakisuka kikosi chake mwenyewe ili asiwe na sababu kwa nini amefanya vibaya.

Uongozi imara

Pluijm anaenda kukutana na viongozi wanaosimamia vyema klabu. Sio tu suala la fedha za kuendesha klabu, bali viongozi wa Azam wanajali wachezaji pamoja na mambo mengine kama kuwafanya wachezaji wawe na nidhamu na uvumilivu na hivyo wachezaji wengi kudumu ndani ya Azam.

Katika suala la afya za wachezaji, Azam kupitia viongozi wake wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha mchezaji anapata matibabu ikiwezekana nje ya nchi pale inapohitajika ili tu kumrudisha mchezaji katika hali yake na kiwango chake.

Azam ndio timu pekee ambayo imekuwa ikiwasaidia wachezaji wao kuhakikisha wanapata matibabu pale wanapopata matatizo bila kujali ukubwa wa tatizo hasa pale wanapopata matatizo wakiwa chini ya uongozi wao, mfano Shomari Kapombe wakati akiichezea klabu hii kabla ya kuhamia Simba, Joseph Kimwaga na sasa Donald Ngoma ambaye alipelekwa nchini Afrika ya Kusini kwa ajili ya matibabu kabla hata ya usajili wake Azam.

Mfumo bora wa timu za vijana

Yahaya Zayd, Shaaban Idd Chilunda ni mfano msuri wa jinsi Azam FC imekuwa waumini wa soka la vijana. Wachezaji hawa kwa sasa wamepandishwa timu kubwa huku pia nyota zao zikizidi kung’ara kutokana na kuwepo katika kipengele cha wachezaji wanaowania tuzo ya mchezaji bora chipukizi zitakazotolewa na TFF.

Azam ni zaidi ya akademi ya kukuzia wachezaji kutokana na inavyojiendesha, kwani imekuwa ikiwasaidia chipukizi kupandisha viwango vyao kwa kuwapa malezi bora wawapo kambini.

Pluijm sio muumini sana wa vijana kutokana na kutegemea zaidi wale wenye uzoefu. Akiwa Yanga na hata Singida United amekuwa akiwatumia zaidi wazoefu kutokana na kutokuwaamini vijana.

Pale Azam sidhani kama Pluijm atashindwa kuwatumia vijana na hasa hawa waliopandishwa msimu uliopita kutokana na ukomavu wao kwenye Ligi Kuu.