MAONI: Kikosi hiki cha Taifa Stars kina uwezo wa kufanya vizuri zaidi

Muktasari:

Stars ilitoka suluhu ugenini na Benin juzi Jumapili na kufikisha mechi 14 chini ya Mayanga ambapo ameshinda mara sita na kupoteza mara moja tu.

TIMU ya taifa ya soka ya wanaume, Taifa Stars, imeendelea kuwa na rekodi nzuri chini ya kocha Salum Mayanga, licha ya kuwepo kwa hisia tofauti juu ya uwezo wa kocha huyo mzawa na namna timu hiyo inavyocheza.

Stars ilitoka suluhu ugenini na Benin juzi Jumapili na kufikisha mechi 14 chini ya Mayanga ambapo ameshinda mara sita na kupoteza mara moja tu.

Rekodi hiyo inaonekana kuwa nzuri kwa Mayanga licha ya kwamba bado hajaweza kupata ushindi katika mechi ya mashindano makubwa ambayo Stars inawania kushiriki.

Ikumbukwe kuwa Stars ililazimishwa sare ya bao 1-1 na Lesotho katika mchezo wa kwanza wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka 2019.

Stars pia iliondoshwa na Rwanda katika kuwania kufuzu mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan). Stars iliondoshwa kwa faida ya bao la ugenini baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani na kisha kutoka suluhu nchini Rwanda.

Kwa minajili hiyo, ni kwamba Mayanga pamoja na kuwa na rekodi nzuri, bado ana changamoto ya kufanya vizuri zaidi katika mechi za mashindano. Pia baadhi ya wadau wa michezo wamekuwa hawaridhishwi na kiwango halisi cha timu hiyo.

Ni imani yetu kwamba Taifa Stars inaweza kufanya vizuri zaidi, hasa baada ya kutazama kiwango ilichoonyesha ugenini nchini Benin, hasa katika kipindi cha pili.

Kikosi cha Stars ya sasa kinaundwa na wachezaji wengi wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi, tofauti na kipindi kingine chochote.

Kwa sasa kuna wachezaji Abdi Banda, Hamis Abdallah, Abdul Hilal, Farid Mussa, Elius Maguli, Simon Msuva na nahodha Mbwana Samatta ambao wanatoka nje. Licha ya kwamba Samatta ni majeruhi kwa sasa, bado ni mchezaji wa timu hiyo ya Taifa.

Pia wachezaji wanaocheza Ligi Kuu Bara ambao wanaitwa Stars, wapo katika viwango vya juu.

Mfano, mabeki Gadiel Michael na Erasto Nyoni, viungo Mudathir Yahya na Himid Mao pamoja na winga, Shiza Kichuya wamekuwa na viwango vya juu msimu huu.

Hili linampa kocha chaguo pana katika kikosi chake. Imekuwa kawaida sasa kuona wachezaji wa viwango vya juu kama Mzamiru Yassin na Jonas Mkude wakianzia benchi katika kikosi cha Stars.

Kutokana na uhalisia huo, ni wazi kwamba Stars inaweza kufanya vizuri zaidi ya inavyofanya sasa kama kocha wa timu hiyo ataendelea kuingiza mabadiliko.

Muda mwingi ambao Stars inacheza nyumbani imekuwa ikijilinda badala ya kushambulia, tofauti na zinavyofanya timu nyingi pindi zikicheza kwao.

Ni wazi kwamba mbinu ya kujilinda hutumiwa zaidi ugenini ama pindi ambapo timu imeshapata ushindi, ili kuhakikisha inaondoka na alama zote tatu.

Kama Mayanga ataendelea kufanya marekebisho ndani ya timu na kubadili mfumo hasa akicheza nyumbani, ni wazi Stars itafanya vizuri zaidi.

Pia Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), linatakiwa kutazama upya namna ya kuifanya Stars irejee katika mioyo ya Watanzania kama ilivyokuwa miaka mitano nyuma.

Ipo haja ya TFF kuandaa ajenda maalumu ya kuisapoti Taifa Stars na kuwa na mikakati ya kuifanya iwe timu inayouzika mitaani.

Hili linaweza kufanyika kwa ushirikiano mkubwa na wadhamini wa timu hiyo, bia ya Serengeti, ambao pamoja na yote wanataka kujiuza sokoni.

Kama kutakuwa na kampeni za mtaa kwa mtaa, katika masoko na maeneo mengine, kuhamasisha watu kwenda uwanjani kuitazama Taifa Stars, itakuwa ni jambo jema.

Pia, TFF inaweza kufanya tathmini ya ubora wa benchi la ufundi na kuangalia kama ipo haja ya kuliongezea nguvu ili liweze kuifanya Stars iwe timu ya ushindani zaidi.

Wakati huu ambapo tuna miezi minne kabla ya kuendelea na mechi za kufuzu Afcon ambapo tutacheza na Uganda na Cape Verde, ni vyema tukawa na mikakati madhubuti ya kuibeba Stars.

TFF iweke mpango kabambe wa kuhakikisha tunafanya vizuri katika mechi hizo.

Ni matumaini yetu TFF inaitazama Stars kama bidhaa muhimu na itaisambaza kwa Watanzania wote.