ROHO NYEUPE: Kwa hatima ya soka letu, tumchagueni huyu kuwa Rais TFF

Friday August 11 2017Gift  Macha

Gift  Macha 

By GIFT MACHA

MPAKA sasa ni ngumu kutabiri nani atakuwa Rais mpya wa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) katika uchaguzi utakaofanyika kesho Jumamosi mjini Dodoma.

Ni vigumu vivyo hivyo kutabiri nani atakuwa Makamu wa Rais, kwa kuwa ushindani ni mkali sana. Uchaguzi huu unaonekana kushika hatamu hasa kutokana na wagombea kujitokeza kwa wingi, zaidi ya miaka ya nyuma.

Wapo baadhi ya wapigakura ambao mpaka sasa hawajafanya maamuzi kuwa wamchague nani. Wapo wengine ambao walipanga kumrejesha madarakani Rais wa sasa, Jamal Malinzi na bado hawajafahamu mtu mwingine wa kumchagua baada ya kipenzi chao kukatwa.

Ni wazi sasa baada ya Malinzi kufeli kwa kiwango kikubwa, tunahitaji kiongozi shupavu na mwenye weledi. Tunahitaji kiongozi ambaye si tu anasema atafanya kitu fulani, bali ambaye anasema atakifanya vipi. Kiongozi, ambaye anasema atatufikisha sehemu na kutuonyesha njia ya kwenda hiyo sehemu sio maneno tu.

Ni vyema wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF wakahoji zaidi juu ya namna ambavyo wagombea wamejipanga kufanya. Tusichague Rais wala Makamu, ambaye hajajibu swali ATAFANYAJE? Mgombea asiishie kusema tu atafanya, aseme na atatumia njia gani kufanya.

Kama mgombea anasema atahakikisha Ligi Kuu Bara inakuwa ya ushindani zaidi, aseme ni kivipi atalifanya hilo. Kusema tu ni rahisi, lakini kiongozi bora lazima ataonyesha njia, anafanyaje. Hawa ndio tunaowataka.

Kama mgombea anasema ataimarisha uwezo wa waamuzi wa Ligi Kuu Bara, aseme kabisa atalifanya vipi hilo? Je ni kwa kutoa elimu? Kuboresha maslahi ya waamuzi? Kuongeza adhabu ama kwa vipi? Lazima ajibu swali la KIVIPI?

Tusichague wagombea wenye hoja nyepesi. Tusichague wagombea wenye historia chafu. Tusichague wagombea ambao, wamekuwa TFF kwa miaka nenda rudi na hawana cha kujivunia.

Tujikite katika hoja za msingi. Lazima kiongozi anayekuja atueleze amejipanga vipi kuleta maendeleo ya soka nchini. Ana mipango gani ya kuisaidia Taifa Stars na kusaidia soka la vijana. Nimeona wagombea wanatoa hoja nyepesi tu bila kujibu swali la kivipi watatekeleza hoja zao.

Mgombea anayefaa ni yule, ambaye anasema katika soka la vijana ataanzisha programu fulani ili kulinyanyua. Mfano mgombea wa nafasi ya Makamu wa Rais, Mulamu Ng’ambi amesema wazi kwamba ataanzisha timu za vijana chini ya miaka 13 kila mkoa na baadaye kila wilaya.

Ameweka wazi atafanya hilo kwa kushirikiana na Shule za Msingi katika maeneo hayo. Angalau katika hili amejitahidi kuweka mpango kazi unaoleta taswira chanya.

Wagombea wengine wameishia kusema wataboresha soka la vijana, lakini hawajasema wataboreshaje. Kwanini wagombea wa nafasi kubwa kama hizi wanashindwa kujibu maswali ya msingi? Kwa nini wanashindwa kusema watafanyaje ili wajenge taswira ya wadau wa soka?

Miongoni mwa mambo ambayo yalimfelisha Malinzi ndiyo haya. Malinzi alisema atafanya hiki na kile, lakini hakusema atafanyaje. Hapa ndipo alipofeli. Ilipofikia hatua ya kufanya alishindwa kujua anafanyaje na kuonekana anavuruga.

Matokeo yake akaanza kuja na programu za ajabu kama Taifa Stars Maboresho na kampeni za Changia Taifa Stars. Alitamani kuona Taifa Stars inafanya vizuri, lakini hakujua njia sahihi ya kuisaidia ifanye vizuri, matokeo yake akaharibu.

Sitaki kuona tunarejea huko. Mgombea akisema atalisaidia soka la wanawake, aseme wazi kwamba atafanya vitu gani kulisaidia. Ni kwa vipi atalisaidia? Amepanga kufanya nini na nini kusaidia soka hilo? Tusiache tu mgombea aseme atasaidia bila kuonyesha njia.

Kama mgombea atasema tu kwa wepesi kuwa atasaidia kuboresha utendaji wa TFF bila kusema ni kwa njia gani, ana tofauti gani na mimi ama wewe? Mgombea wa urais ama makamu lazima awe na hoja nzito na siyo nyepesi nyepesi tu kama pamba.

Tunataka wagombea waonyeshe mikakati yao.

Kama tutachagua wagombea ambao hawana mikakati imara, basi tutaishia hapa hapa ama tutarudi nyuma zaidi. Tusikubali haya. Maamuzi tunayofanya sasa yatadumu kwa miaka minne, siyo jambo dogo.