Kwa Simba ile, ni Manula, Kapombe tu wanaanza

Tuesday June 12 2018Gift  Macha

Gift  Macha 

SIMBA imefungwa na Gor Mahia kwenye pambano la fainali ya SportPesa Super Cup. Imefungwa 2-0 ndani ya dakika 90. Nani anashangazwa na matokeo hayo? Simba ilishafungwa kabla na baada ya mchezo huo.

Gor Mahia ni habari nyingine. Imekamilika kila idara. Wachezaji wake wako fiti na wameiva kiufundi. Timu yao iko imara nyuma, katikati na mbele. Imekamilika.

Haikushangaza kuona Simba ikizidiwa kila idara kwenye mchezo wa fainali. Simba ilipotea katikati ya uwanja, mbele na nyuma. Ilizidiwa.

Kwa kifupi tunasema ilipata kipigo halali. Mechi ilichezeshwa kwa haki. Waamuzi walifanya kazi yao kwa weledi. Wachezji walikuwa huru kufanya lolote uwanjani lakini hawakuweza.

Wakati wachezaji wa Simba wakionekana kuwa fiti kwa dakika 90, wale wa Gor Mahia walionekana kuwa fiti kwa dakika 120. Kila kitu walikuwa wanaizidi Simba.

Waliizidi Simba kwa umakini, utayari wa kucheza michuano hiyo pamoja na kiwango cha msisitizo wa ushindi. Baada ya hapo wakaizidi Simba uwezo na mbinu uwanjani. Haikushangaza sana.

Ilikuwa ni mechi ya bingwa wa Ligi Kuu ya Kenya na wa Ligi ya Tanzania. Hata hivyo, uwanjani haikuonekana hivyo. Ilionekana kama timu kubwa kutoka Kenya inacheza na timu ya kawaida kutoka Tanzania.

Simba haikuwa kwenye uzani wa kupambana na Gor Mahia. Mechi yao hata ingechezwa kwa dakika 90 nyingine bado wasingeweza kusawazisha. Uwezo wa

Simba kufunga mabao ya kusawazisha ulikua mdogo kuliko wao kuongezewa bao la tatu.

Nini kimetokea? Ni jambo la kutafakari. Hebu tuanze kwanza na tathmini ya vikosi vilivyoanza pambano hilo la fainali. Ni wachezaji wangapi wa Simba wanaweza kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha Gor Mahia?

Labda wawili tu. Ni kipa Aishi Manula pamoja na beki wa kulia, Shomary Kapombe. Wengine wote wataanzia benchi. Pengine na Erasto Nyoni angeweza kufikiriwa kidogo kama anaweza kuanza kwenye kikosi hicho cha Gor. Labda kwa uzoefu wake.

Hiki ndicho kilicholeta tofauti kubwa ya mchezo wa Jumapili jioni. Kwa uwezo wa mchezaji mmoja mmoja, Gor Mahia imeiacha Simba mbali sana. Haishangazi kuona

wako hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Unafikiri ni straika gani wa Simba aliyeanza kwenye pambano hilo la fainali ambaye angeweza kuwaweka benchi Jacques Tuyisenge na Meddie Kagere? Ni Adam Salamba?

Ni Mohammed Rashid? Hapana, labda Emmanuel Okwi kama angekuwepo. Mastraika wa Simba walizidiwa uwezo mbali sana na wale wa Gor Mahia. Hakuna straika wa Simba aliyeweza kufunga bao kwenye mashindano ya mwaka huu, wakati Kagere peke yake amefunga manne. Yaani mastraika wote wa Simba hawana uwezo hata unaomkaribia Kagere.

Ni kiungo gani wa Simba angeanza mbele ya Wendo Ernest ama Kahata Francis? Hakuna. Jonas Mkude na Mzamiru Yassin wote wangesugua benchi. Wendo ni mwanaume wa shoka. Anakaba mtu kwa mtu na nafasi. Anaipa uhuru timu yake.

Kahata ndiyo habari nyingine kabisa. Anaufanya mpira kuwa kitu rahisi. Ana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira na kufungua timu. Anapiga pasi ndefu zinazofika. Ana uwezo wa kupunguza wachezaji wa timu pinzani kama anavyojisikia. Ni kiungo gani wa Simba anaweza kufanya hivyo? Hakuna.

Mabeki wa Gor Mahia ndio wamekamilika zaidi. Haikushangaza kuona wamemaliza mashindano ya mwaka huu bila kuruhusu bao. Wako vizuri kwenye mipira ya juu na chini. Wako fiti kweli kweli.

Mwisho wa yote tofauti ya ubora wa Simba na Gor Mahia ilionekana mapema sana. Gor imetawala mechi zote za michuano hiyo. Gor Ilikuwa bora kwenye kila hatua. Ilistahili ubingwa.

Tuna kitu cha kujifunza kutoka kwa Gor Mahia. Simba, Yanga, Azam na Singida United zinatakiwa kuwekeza kwenye wachezaji wa viwango vya juu. Baada ya hapo kazi ya kocha yeyote itakuwa nyepesi.

Tuache kufanya kazi kwa mazoea. Timu zetu zifanye usajili wa maana. Yaani Gor Mahia ya mwaka huu ni kama ile Yanga ya mwaka 2016 aliyokuwa nayo Hans Van Pluijm. Kwa sasa hawana mpizani Afrika Mashariki.

Kwa namna Gor Mahia ilivyocheza kwenye michuano hii ya SportPesa Super Cup, ni wazi kuwa Yanga ina kazi kubwa kwenye mechi yao ya Kombe la Shirikisho mwezi ujao. Isipokuwa makini, Yanga itachezea nyingi ndani na nje.