MAONI: Kuna kila sababu kwa BMT, TFF kukaa kitako na Yanga

Muktasari:

Yanga imeutema ubingwa wa Ligi Kuu Bara mbele ya Simba, ambayo kesho Jumamosi itakabidhiwa kikombe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli.

KINACHOENDELEA ndani ya Yanga kwa sasa kinasikitisha, lakini hakipaswi kuachwa hadi kufikia mambo kuharibika kabisa, kwa mustakabali wa maendeleo ya soka la Tanzania.

Yanga imeutema ubingwa wa Ligi Kuu Bara mbele ya Simba, ambayo kesho Jumamosi itakabidhiwa kikombe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli.

Yanga imeondolewa Ligi ya Mabingwa Afrika na kuangukia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho, lakini nako imeanza kwa kusuasua.

Kwa sasa Yanga ina matatizo ndani na nje ya uwanja kwani tangu imeondokewa na kocha wake, Mzambia George Lwandamina, imeshindwa kupata ushindi kwenye mechi nane mfululizo ambazo ni sawa na kucheza dakika 720 bila ushindi.

Katika michezo hiyo ambayo Yanga imecheza kwenye mashindano yote, imeambulia pointi tatu tu na zote zimepatikana kwenye sare. Yanga ambao ndio wawakilishi pekee kwenye michuano ya kimataifa, imeshindwa kupata ushindi katika mechi tatu mfululizo za kimataifa, ikianza na ile ya Welayta Dicha ya Ethiopia, USM Alger na Rayon Sport uliopigwa juzi usiku Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika Ligi Kuu Bara, Yanga imepoteza mbele ya Simba, Mtibwa na kulazimishwa sare na Mbeya City na Prisons na sasa inapambana kumaliza ligi kwenye nafasi ya pili. Yanga ya sasa inatia huruma kwani, si ile ya miaka mitatu iliyopita ilipokuwa chini ya Mwenyekiti wake, Yusuf Manji.

Uwanjani inaonekana Yanga ambayo wachezaji wake ni kama wamekata tamaa huku mastaa wengine wakiwa kwenye mgomo baridi.

Wachezaji wanalalamika kutolipwa mishahara kwa wakati huku baadhi wakiendelea kuonyesha uzalendo kwa timu kwa kuendelea kucheza, japo wanaonekana kutokuwa na morali.

Katika kutuliza hali ya mambo uwanjani, Yanga imemleta kocha mpya, Mkongomani Mwinyi Zahera kujaribu kurejesha makali ya kikosi, lakini pamoja na jitihada hizo bado hajafanikiwa kutokana na uongozi kuonekana kuwa na tofauti za ndani.

Mwanaspoti linaamini mambo ndani ya Yanga kwa sasa hayapo sawa huku viongozi wakionekana kutozungumza lugha moja japo, wanapambana kuficha hali halisi klabuni hapo.

Tangu Zahera amewasili klabuni hapo, Yanga imeshashuka dimbani mara tano huku kocha huyo akikiangalia kikosi chake kutokea jukwaani kwa kile kinachoelezwa hana kibali cha kufanyia kazi nchini. Ni jambo linaloshangaza, iweje Yanga imlete kusimamia benchi la ufundi halafu afanye kazi kwa kujificha ficha?

Utendaji wa Zahera ni ishara tosha kuwa mambo ndani ya Yanga hayako sawa ama viongozi wake hawafahamu wamemleta nchini kwa ajili ya kazi gani. Kwa sasa Kocha Msaidizi, Shadrack Nsajigwa na Mzambia Noel Mwandila ndio wanaosimama kwenye benchi la Yanga wakati wa mechi.

Lakini, mbali ya hayo Yanga inawakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa na hapa ndipo Mwanaspoti linadhani kuna kila sababu kwa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), kuona umuhimu wa kufahamu kinachoendelea ndani ya Yanga.

Huenda ikawa ni kinyume, lakini kwa nia njema na yenye lengo la kulinda heshima ya soka la Tanzania kimataifa, vyombo hivyo vinaweza kuzungumza na viongozi wa Yanga ili kuangalia namna bora ya kuwasaidia.

Inafahamika kuwa timu yetu iwe ya soka, kuogelewa ama riadha inaposhiriki michuano ya kimataifa huwakilisha nchi, hivyo kuepukana na aibu ya Yanga kumaliza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho ikiwa mkiani tena, ni lazima matatizo yake yafahamike na ikiwezekana isaidiwe.

Matokeo inayoyapata Yanga kwa sasa yamekuwa yakiwasononesha wengi bila kujali ushabiki kwa kuwa, inawakilisha nchi na Mwanaspoti inachelea kusema kwamba, huenda wachezaji wameingia kwenye matatizo ya nje ya uwanja klabuni hapo badala ya kutimiza jukumu lao la kucheza mpira.

Tunashauri kama TFF ilivyojikita wakati Yanga ilipokwenda Ethiopia kuikabili Dicha kwenye mchezo wa pili, juhudi hizo zitumike na sasa badala ya kusubiri mambo yaharibike.

Kwa msimamo ulivyo, Yanga inahitaji kushinda mechi zilizobaki ili kujiweka pazuri, lakini hilo litawezekana tu kama mambo yatawekwa sawa vinginevyo ni maumivu tena Kombe la Shirikisho.