Klabu zionyeshe heshima kwa wadhamini

USAJILI wa wachezaji wapya bado ni habari kubwa inayoendelea nchini hasa kwa klabu za Ligi Kuu Bara. Zipo timu zinazosajili majina makubwa wakati nyingine zinatoa nafasi kwa vijana kutokana na malengo yao kwenye Ligi.

Licha ya kwamba usajili unafanyika ikiwa ni makubaliano baina ya timu na mchezaji husika, kumetokea tatizo la kuheshimu wadhamini wa klabu husika jambo ambalo linakatisha tamaa.

Timu kadhaa za Ligi Kuu kama Simba, Yanga, Azam, Singida United, Mbeya City, Ruvu Shooting na Mbeya City zimebahatika kuwa na wadhamini wanaowasaidia kulipa mishahara pamoja na gharama nyingine za klabu.

Simba, Yanga na Singida United zinapokea udhamini mkuu kutoka kwa kampuni ya Bahati Nasibu ya SportPesa. Azam inapata udhamini kutoka NMB wakati Mbeya City inapata udhamini wa BinSlum, huku Ruvu Shooting ikiwa na udhamini wa Cowbell. Hao ni wadhamini wakuu tu. Zipo timu nyingine zenye wadhamini wawili ama zaidi. Mfano Mbeya City mbali na udhamini wa BinSlum, Coca-Cola na Sport Master.

Singida United ina udhamini wa NMB, Halotel, RSS na Puma. Ni bahati kwa timu hizo kuwa na wadhamini wengi.

Mikataba mingi ya wadhamini hawa inategemea matangazo kutoka upande wa klabu. Kampuni inapolipa mamilioni ya fedha kwa klabu, inatarajia kutangazwa ndani na hata nje ya nchi ili kuweza kuwafikia wateja wao.

Kwa kampuni kutoa Sh100 milioni ama zaidi ili kupata matangazo kutoka wa klabu husika, sio jambo dogo kwani ni kampuni chache zenye uwezo wa kufanya hivyo.

Moja ya makubaliano yanayokuwepo baina ya klabu na kampuni hizi, ni kuvaa jezi zenye nembo ya mdhamini mazoezini pamoja na kwenye mechi. Kuweka mabango ya wadhamini katika matangazo ya klabu na pia kuweka nembo hizo kwenye tovuti na shughuli nyingine za klabu. Mfano wachezaji wanaposajiliwa, wadhamini hutaka kuwepo kwa picha za matangazo nyuma ya shughuli hiyo ili kuwatangaza. Mfano kwenye mkataba wa SportPesa na klabu za Simba na Yanga, unazitaka klabu hizo kuweka mabango yao nyuma ya shughuli ya usajili ili kuwatangaza.

Wadhamini wengi wanaamini kwamba mashabiki wanavutika zaidi na habari za usajili, hivyo kwa kuweka matangazo yao nyuma itasaidia kuwafikia watu wengi zaidi.  Hii ndiyo sababu wanaweka kipengele hicho katika mikataba yao.

Habari mbaya kwa wadhamini wetu ni kwamba klabu zimekuwa haziheshimu kipengele hicho na katika shughuli yote ya usajili wamekuwa hawaweki mabango ya wadhamini nyuma, jambo ambalo linaonekana kama siyo heshima kwa watu wanaowapatia pesa. Ni klabu chache ambazo zimekuwa zikitekeleza kipengele hicho japo bado siyo kwa asilimia zote. Mfano Singida imekuwa ikiweka mabango katika baadhi ya usajili wao, lakini wakati mwingine wanasahau.

Klabu ya Simba ndiyo imekuwa nyuma zaidi katika zoezi hilo kwani mara zote inawasainisha wachezaji bila kuzingatia matakwa ya wadhamini hao jambo ambalo linaonyesha kwamba hawathamini mkataba wao.

Simba imekuwa ikiweka nembo ya Simba APP katika picha za wachezaji inaowasajili na kusahau kabisa kwamba pesa hata za usajili huo zinatoka kwa wadhamini wao SportPesa.

Usajili mwingi umekuwa ukifanyika bila kuwepo kwa nembo ya mdhamini kwa nyuma jambo ambalo ni kinyume na makubaliano ya mkataba.

Tumeona wachezaji kama Ibrahim Ajib na Youthe Rostand wakisaini Yanga lakini hakuna mabango ya SportPesa.

Tunawapongezi Mbeya City ambayo imekuwa mstari wa mbele katika kuheshimu vipengele vya mikataba hiyo, kwani hata wanaosajiliwa husajili wakiwa mbele ya mabango ya wadhamini.