MAONI: Klabu, wachezaji tumieni mitandao kujitangaza

Muktasari:

Hii ni tofauti na miaka mingi iliyopita, teknolojia hasa ya mawasiliano ilikuwa chini, kiasi mtu kupata habari ama kuwasiliana na mwingine ilichukua muda mrefu.

DUNIA ya sasa inaenda kwa kasi mno. Kila kitu kimebadilika na mambo yamerahishwa, kiasi dunia imekuwa kama kijiji kimoja tu.

Hii ni tofauti na miaka mingi iliyopita, teknolojia hasa ya mawasiliano ilikuwa chini, kiasi mtu kupata habari ama kuwasiliana na mwingine ilichukua muda mrefu.

Hata hivyo, katika ukuaji wa maendeleo na hasa sayansi ya mawasiliano kwa sasa, mtu humchukua sekunde chache tu kupata taarifa ama kuwasiliana na aliye mbali. Nyenzo zimerahisha mambo.

Ukiacha mawasiliano ya simu za mkononi, kuna mitandao ya kijamii, tovuti, blog na nyenzo nyingine ambazo zinamruhusu mtu kuwasiliana, kutunza rekodi zake na hata kupakua chochote akitakacho ndani ya muda mfupi.

Kitu kizuri ni kwamba vitu hivyo kwa sasa havihitaji kwenda mgahawani (internet Cafe), kupitia simu tu mtu anafanya kila kitu kwa sababu zimeboreshwa kwa kiwango cha hali ya juu na hata bei zinaruhusu watu wa kada tofauti kumiliki.

Tanzania kama mataifa mengine imepokea mabadiliko hayo kwa kishindo na kuifanya jamii karibu yote kukumbwa na upepo wa teknolojia wakiwamo nyota wetu wa michezo, sanaa na burudani kwa jumla.

Mastaa wetu wamekuwa wakimiliki simu za kisasa zinazorahisisha kazi, pia wakimiliki kurasa zao kwenye mitandao ya kijamii.

Hata hivyo, sio wote wanaojua kama nyenzo hizo zinaweza kuwasaidia katika kuwatoa mahali walipo na kuwapeleka mbali zaidi kimaendeleo. Angalau kidogo wasanii wa muziki na waigizaji wameshtuka na kutumia kurasa zao kujitengenezea jina, lakini kwa wachezaji wetu ni wachache wanaoitumia kwa manufaa zaidi ya kutumia picha za kula bata ama kufanya manunuzi tu.

Ni wachezaji wachache ambao wanajitangaza kupitia kurasa zao ama kwa kuweka wasifu wao sahihi wa kile anachokifanya, namna ambavyo kazi yake uwanjani huwa na mifano kama hiyo.

Jaribu kupitia kurasa za mastaa wetu ndio utaelewa Mwanaspoti linamaanisha nini? Inawezekana wengi hawajajua mitandao na nyenzo hizo za mawasiliano kama ni sehemu ya kujitangaza badala ya kuonyesha upuuzi tu.

Kwa mfano ni wachezaji wangapi wanaotumia mtandao wa Youtube kuonyesha namna wanavyofanya kazi zao uwanjani ambazo zingeweza kuwarahisishia kazi mawakala wa nje ya nchi kuwafuatilia kupitia huko?

Inawezekana haya yanashindikana kwa sababu ya wachezaji wetu kutokuwa na menejimenti zinazowasimamia, hivyo kushindwa kuifanya kazi hiyo ya kurekodi anapokuwa uwanjani kisha kutupia mtandaoni ili watu wamwone.

Hata matukio yao yanayonaswa na kurushwa na mitandao, vituo vya runinga nchini wala hawashughuliki navyo. Jambo hilo lipo hata kwa tovuti ama kurasa zinazomilikiwa na klabu za soka nchini.

Hazina utamaduni wa kutunza kumbukumbu ama kuweka wasifu hata wa vikosi vyao. Hivyo Mwanaspoti linawakumbusha wachezaji na mastaa wengine waitumie mitandao kujitangaza badala ya kuendekeza mambo ya ovyo.

Baadhi ya wasanii wamekuwa wakiitumia mitandao kuendesha mipasho, vijembe na kutukanana, wachezaji wasiige mfano huo wafuate njia sahihi kwa manufaa yao.

Sio kwa wachezaji tu hata viongozi wa klabu nao wajaribu kuzifanya klabu zao kuwa za kisasa zaidi kupitia mitandao ya kijamii na tovuti wanazomiliki.

Ni aibu tovuti ya klabu ama kurasa za klabu hazina taarifa ama rekodi za nyota wa vikosi vyao, haziwezi kutoa taarifa hata ya mechi wanazocheza ama kile ambacho kinafanyika ndani ya klabu yao mpaka maofisa habari watafutwe kwa simu.

Tumekuwa tunaona kurasa na tovuti za klabu za nje na hata za wachezaji jinsi zinavyokuwa ‘hai’ muda wote wakiweka kila kinachoendelea kuhusu wao, tofauti na tovuti ama kurasa za klabu zetu na hata nyota wetu.

Nyingine zipo zipo, hii sio sawa kwa sababu dunia ya leo sio ile ya zamani. Imebadilika na inaenda kasi.

Mawakala na hata klabu za nje haziwezi kuwa na kiu ya kutaka kumsajili mchezaji kutoka Tanzania ama katika klabu zetu wakati hawawajui wasifu wao kisoka na hata mambo mengine yanayomhusu.

Klabu na wachezaji wetu wabadilike sasa, wapite kule walikopita nyota wenzao wa mataifa ya nje walivyo wajanja.