Kim Poulsen kawakosea nini Wabongo?

Muktasari:

  • Baada ya kupita kipindi kigumu kisoka tangu alipoondoka kocha kipenzi, Marcio Maximo, Poulsen alionyesha dalili za kujaribu kuuvunja mfupa wa unyonge wa muda mrefu wa Stars kwenye mashindano ya kimataifa.

MIONGONI mwa zawadi muhimu na za kipekee ambazo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) chini ya Leodgar Tenga uliwapa Watanzania ni kocha Kim Poulsen.

Baada ya kupita kipindi kigumu kisoka tangu alipoondoka kocha kipenzi, Marcio Maximo, Poulsen alionyesha dalili za kujaribu kuuvunja mfupa wa unyonge wa muda mrefu wa Stars kwenye mashindano ya kimataifa.

Kwanza alitengeneza kizazi fulani cha vijana ambao walionekana wazi wangekuja kuwa msaada kwa timu ya taifa siku za usoni pindi alipoanza kufundisha soka nchini kama kocha mkuu wa timu za taifa za vijana.

Ni huyu Poulsen ndiye alitutengenezea akina Saimon Msuva, Frank Domayo, Mbwana Samatta, Salum Telela, Aishi Manula, Himid Mao, Juma Abdul na Hassan Kessy kwa kuwapa misingi imara ya soka iliyowafanya wawe wanasoka mahiri na tunaowategemea.

Baada ya kupandishwa na kuanza kuifundisha Taifa Stars, Poulsen alitengeneza kikosi chenye muunganiko bora baina ya vijana wadogo na wazoefu na kuifanya timu hiyo kuwa imara na tishio kwa vigogo vya soka Afrika.

Hata hivyo pamoja na mipango na mikakati yake inayoonekana kuwa na faida chanya kwa soka la Tanzania, Kim Poulsen ni kama amekuwa na damu ya kunguni pale kwenye TFF.

Kazi kubwa aliyoifanya katika awamu yake ya kwanza nchini haikuonekana haina maana yoyote na uongozi ulioingia madarakani kwenye shirikisho hilo baada ya Tenga na alijikuta akitimuliwa na nafasi yake kupewa Mart Nooij.

Inasemekana alitimuliwa kama mkakati wa kuondoa masalia yote yaliyoachwa na Tenga katika mpira wa Tanzania. Hata hivyo, baada ya kelele za muda mrefu za wadau wa soka nchini, Poulsen alirudishwa tena Tanzania ambapo safari hii alikuja kama mkurugenzi wa timu za taifa za vijana.

Ndani ya muda mfupi baada ya kupewa nafasi hiyo, Poulsen kwa kushirikiana na Bakari Shime walitengeneza timu bora ya vijana wenye umri chini ya miaka 17

‘Serengeti Boys’ ambayo ilifuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri huo zilizofanyika Gabon mwaka jana.

Mafanikio hayo yalianza kuwapa matumaini Watanzania kuwa kutakuwa na muendelezo mzuri wa timu zetu za taifa za vijana kwenye mashindano mbalimbali.

Tayari dalili za hili lilishaanza kutokea baada ya vijana hao wakiwa chini ya Poulsen na Kocha Oscar Milambo kuchukua ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati kwenye mashindano yanayohusisha vijana wa umri huo wakiwa hawajapoteza mchezo hata mmoja.

Hata hivyo, wakati mchakato wa maandalizi ya Serengeti Boys kwa ajili ya kushiriki mashindano ya Afrika mwakani ukianza kupamba moto, Kim Poulsen ametangaza kujiuzulu kwenye nafasi yake kwa madai ya kutolipwa mshahara.

Hili ni pigo kubwa kwa Serengeti Boys kuelekea fainali za Afrika mwakani kwani Kim tayari alikuwa ameshaandaa programu kabambe za kuhakikisha tunafanya vizuri.

Lakini wakati Watanzania wakionyesha kutofurahishwa na kujiuzulu kwa Poulsen, hadi sasa shirikisho liko kimya na ni kama hawajaguswa na jambo hilo.

Ukimya wao unaashiria kuwa wamefurahia Kim aondoke na walikuwa wanatafuta sababu tu ya kuachana naye vinginevyo wangeonyesha kuguswa na hilo lililotokea.

Pengine kuna kitu ambacho Poulsen amewakosea lakini ikumbukwe kazi anayotufanyia kisoka. Lazima tujirudi katika hili.