Kilio kiwe cha Ally Yanga siyo Niyonzima

Muktasari:

Hakuna mtu yeyote anayeweza kuwa na furaha pindi anapopita kwenye matatizo, kwa nyakati hizo unahitajika uvumilivu wa hali ya juu kukabiliana na changamoto anazopitia, vinginevyo anaweza kupata shida zaidi.

NI kawaida kwa mwanadamu wakati fulani kupita katika nyakati ngumu kwenye maisha yake. Ni kama vile anavyoweza kupita katika kipindi cha neema ambacho humfanya asahau shida zote alizokutana nazo awali. Ndio maisha yalivyo.

Hakuna mtu yeyote anayeweza kuwa na furaha pindi anapopita kwenye matatizo, kwa nyakati hizo unahitajika uvumilivu wa hali ya juu kukabiliana na changamoto anazopitia, vinginevyo anaweza kupata shida zaidi.

Wiki hii inayomalizika, imekuwa ngumu kwa wanachama, wapenzi na mashabiki wa klabu ya Yanga. Wamekutana na matukio mawili yaliyowasababishia simanzi kubwa.

Tukio la kwanza ni la kumpoteza kiungo mahiri, Haruna Niyonzima, ambaye juzi uongozi wa Yanga kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Boniface Mkwasa, ulithibitisha kuwa hatoongeza mkataba wa kuichezea timu hiyo baada ya kushindwa kufikia makubaliano baina yao na kiungo huyo. Inavyosemekana, Niyonzima tayari ameshamalizana na Simba kwa ajili ya kuitumikia msimu ujao ingawa hakuna upande uliothibitisha taarifa hizo kuwa ni za kweli au la.

Lakini wakati suala la Niyonzima likipamba moto, Yanga ilipata pigo jingine la kumpoteza mwanachama na shabiki wake, Ally Mohammed, anayejulikana kwa jina maarufu la Ally Yanga.

Ally Yanga alifariki dunia mkoani Dodoma Jumanne mchana kwa ajali ya gari iliyotokea wilayani Mpwapwa ambako alikwenda kuhamasisha kampeni ijulikanayo kwa jina la Faidika.

Shabiki huyo alizikwa jana Alhamisi mkoani Shinyanga. Kwa wanaomfahamu Ally Yanga, alikuwa ni shabiki hasa wa Yanga ambaye alikubali kupoteza fedha na muda wake kuzunguka sehemu mbalimbali ambako timu hiyo ilicheza ili aiunge mkono.

Kwa jinsi inavyoonekana, suala la Niyonzima kutoendelea kuitumikia Yanga limeteka hisia za kundi kubwa la mashabiki na wapenzi wa timu hiyo kuliko msiba wa Ally Yanga ambaye alikuwa mshabiki kindakindaki wa Yanga.

Katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, tumeshuhudia mashabiki wa Yanga wakiendelea kutoa hisia zao juu ya kuondoka kwa Haruna na kuupa uzito mdogo msiba wa Ally Yanga.

Wengi wameonyesha hasira zao kwa Niyonzima, wakimchukulia kama msaliti kwao kwa kitendo chake cha kugoma kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia timu yao huku akihusishwa kwa ukaribu na Simba inayotajwa kuwa imeshamalizana naye.

Pia kuna wachache ambao wanaonekana kukubaliana na uamuzi wa klabu yao kumpa mkono wa kwaheri Niyonzima, hao wamekuwa wakisimamia hoja kuwa alishaitumikia na kujitolea kuichezea timu hiyo kwa kipindi cha misimu sita mfululizo huku pia wakiamini kuwa yeye kwa ajira yake ya uchezaji aliyoamua kuitumia kuendeshea maisha yake, kitu cha kwanza anachokipigania ni fedha na si mapenzi kwa timu.

Ni hisia na utashi binafsi wa mashabiki wengi wa Yanga kulipa msukumo suala la Niyonzima, lakini kiuhalisia msiba wa Ally Yanga ulipaswa kupewa kipaumbele cha kwanza kuliko habari ya kumpoteza kiungo wao anayeelekea upande wa pili.

Maisha ya mwanasoka hayana mahali maalumu na muda wowote anaweza kuhama kulingana na maslahi anayoyapata. Ni tofauti na shabiki ambaye anakuwa na mapenzi ya kudumu kwa klabu bila ya kupata malipo au stahiki zozote zile. Huu ni wakati mwafaka kuonyesha heshima kwa Ally Yanga kwa jinsi alivyojitolea sehemu ya maisha yake kuisapoti timu hiyo bila kulipwa chochote, ni kutokana na mapenzi tu ambayo alikuwa nayo pengine tangu alipozaliwa. Haipaswi kupoteza muda kumfikiria mtu ambaye ni mpitanjia tu kwenye klabu.

Hata kama Niyonzima angekubali kuendelea kuitumikia Yanga, watu wanapaswa kufahamu kwamba siku moja angeachana na klabu hiyo na kurudi kwao Rwanda, lakini bado wao mashabiki wangeendelea kuipenda Yanga katika nyakati za shida na raha, kama ambavyo Ally Yanga alikuwa anafanya enzi za uhai wake.

Leo hii wakati mwili wa shabiki huyo ukiawa katika siku ya pili kaburini, mashabiki na wanachama wa Yanga wanapaswa kumuona Ally Yanga kama shujaa wao wakiimba sifa zake na kumsifu kwa kila hali kwa jinsi alivyoitumikia timu yao kwa uaminifu na mapenzi makubwa bila malipo yoyote. Mtu aliyekubali kupigwa na jua, kunyeshewa na mvua na kupoteza fedha zake kusafiri maili nyingi kwa ajili ya kuisapoti Yanga. Ukweli alikuwa shabiki wa kweli.