Karia, Wambura achaneni na wapiga debe TFF

Muktasari:

  • Nchi kama Tanzania suala la ajira ni tatizo kubwa na linaendelea kuwa kubwa kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele, ni kwa sababu kila mwaka vijana wanahitimu elimu za vyuo.

 AJIRA inaweza kuwa tatizo kubwa katika nchi za dunia ya tatu, zikiwamo za barani mwetu Afrika.

Nchi kama Tanzania suala la ajira ni tatizo kubwa na linaendelea kuwa kubwa kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele, ni kwa sababu kila mwaka vijana wanahitimu elimu za vyuo.

Kwa hiyo kila fursa inapotokea watu huichukulia kuwa ni ajira, ndio maana usishangae kuona watu wanatumia fedha nyingi katika chaguzi.

Jumamosi tuliuona uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) ukifanyika mjini Dodoma. Hiyo ni ajira kwa baadhi ya walioshinda.

Wallace Karia amechaguliwa kuwa Rais wa TFF huku Michael Wambura akiwa Makamu wa Rais.

Ni uchaguzi ambao umemuweka madarakani Karia aliyekuwa Makamu Rais wa Jamal Malinzi na pia umemrejesha Wambura ambaye amewahi kuwa Katibu Mkuu wa shirikisho hilo enzi hizo likiitwa FAT (Chama cha Soka Tanzania).

Waliochaguliwa si watu wapya katika shirikisho hilo au katika soka, wanazijua fitina zote za soka nchini, hawawezi kubabaishwa na soka letu.

Wanayo kazi kubwa moja; kuhakikisha kuwa wanajenga taasisi ndani ya shirikisho hilo. Wateue wajumbe wa kamati mbalimbali wenye uwezo na weledi.

Ni ukweli usiofichika kuwa ili kushinda katika uchaguzi huo, Karia na Wambura walikuwa na wapiga debe nyuma yao.

Wapiga debe hao ndio walizunguka nchi nzima kupiga kampeni, hao ndio waliwasiliana na wajumbe mpaka usiku wa manane kule Dodoma kuomba kura.

Kwa bahati mbaya sana, wapiga debe wengi katika uchaguzi wowote huwa watu wa aina fulani, wengi hawana kazi.

Huamua kujitosa kupigia watu kampeni wakiwa na malengo ya kupata kazi ama kupata fadhila kwa kipindi ambacho muhusika atakuwa madarakani.

Kuna ambao hutaka kupata kazi baada ya uongozi mpya kuteuliwa, wakitaka wateuliwe katika nafasi mbalimbali za ujumbe au hata kuwa washauri.

Lakini kuna wengine ambao hutaka kupata tenda mbalimbali za biashara, pengine kutengeneza tiketi za kuingilia viwanjani au kufanya biashara nyingine yoyote.

Kwa bahati mbaya huwa hawana sifa za ama kufanya kazi au biashara, hivyo wanavyopewa kazi hiyo hujikuta wakiharibu na kuvuruga taswira nzima ya taasisi.

Na ndio maana ninasisitiza kuwa Karia na Wambura ni binadamu kama walivyo wengine, sijui wataweza vipi kuwaacha watu ambao walishiriki kwa namna mmoja au nyingine kuwapigia debe katika kampeni hizo.

Kwa sasa, hawapaswi kuwa na mambo mengi vichwani mwao.

Wakifanikiwa kuwaweka watu hao pembeni watakuwa wamepiga hatua kubwa sana kufikia malengo.

Wakifanya kosa na kuwateua watu walioshiriki katika kampeni zao, litakuwa ni kosa la mwaka na watakuja kujuta kwa sababu wataaangushwa.

Sababu kubwa ambayo iliufanya uongozi wa TFF uliomaliza muda wake kuyumba ni kujaribu kulipa fadhila kwa kuwateua wapiga debe kuingia katika nafasi mbalimbali za uongozi wa shirikisho hilo.

Kama Karia na Wambura wanataka kuwa salama, wawaache wapiga debe wao pembeni, kama wanataka kulipa fadhila, wawape fedha mambo yaishie hapo.

Kinachotakiwa kwa dhamana yao, kuutengeneza mpira wa Tanzania na kuondokana na sura za kibabaishaji ndani ya TFF.