MAONI: Hongereni Simba, lakini acheni kuwatimua makocha kila kukicha

Muktasari:

  • Kabla ya ujio wa kocha huyu ambaye Mwanaspoti ndio lilikuwa gazeti la kwanza kufichua mpango mzima ambao uliratibiwa kwa weledi mkubwa na mabosi wa Simba, kikosi cha mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita kilikuwa chini ya Kocha Msaidizi, Masoud Djuma.

BAADA kutingisha kwenye usajili kwa kunasa mastaa wa maana, Simba imeingia anga zingine kwa kumshusha Kocha Patrick Aussmes, raia wa Ubelgiji.

Kabla ya ujio wa kocha huyu ambaye Mwanaspoti ndio lilikuwa gazeti la kwanza kufichua mpango mzima ambao uliratibiwa kwa weledi mkubwa na mabosi wa Simba, kikosi cha mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita kilikuwa chini ya Kocha Msaidizi, Masoud Djuma.

Mwanaspoti ambalo lilikuwa na mkanda mzima kuhusiana na mchakato wa Simba kumkabidhi mikoba ya Mfaransa Pierre Lechantre, lilimnasa Aussmes akifuatilia mechi ya Simba dhidi ya Rayon Sport pale Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mwanaspoti linapenda kuipongeza Simba kwa kunasa huduma ya Mbelegiji huyo ambaye rekodi zake kwenye soka sio za kitoto hata kidogo.

Mbali na kuucheza mpira, Aussmes pia amezifundisha timu kibao kwa mafanikio makubwa hivyo, ujio wake ndani ya Wekundu wa Msimbazi utakuwa na maana kubwa uwanjani.

Kama ilivyo kwa Lechantre, Mbelgiji huyu analifahamu vyema soka la Afrika kwani, amezifundisha timu kadhaa kubwa na kubeba mataji hivyo, Simba wamelamba dume. Kwa ufupi tu, rekodi za Aussmes ambazo kwa mara ya kwanza zilichapishwa kwenye gazeti hili la Mwanaspoti, zinaashiria kuwa Simba imejipanga na haitaki utani kabisa msimu ujao.

Rekodi za Aussmes zinaonyesha kuwa, alikipiga katika klabu ya Standard Liege (1981-88), kisha kutua K.A.A Gent (1988-19), R.F.C Seraing (1989-90) na ES Troyes AC (1990-93).

Baada ya kustaafu mwaka 1993 kama Kocha Mchezaji wa Troyes inayoshikili Ligue 1, alijitosa jumla kuwa kocha ndani ya klabu hiyo hadi 1995 alipotua Saint Lousienne ya Re Union.

Klabu nyingine alizofundisha ni Capricorne Saint-Pierre, Stade Beaucairois, Stade de Reims, KSA Cameroon, SCO Angers, Evian Thonon Gaillard F.C, Shenzhen Ruby, Chengdu Blades na kutua kwa waliokuwa Mabingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika 2012 AC Léopards akimpokea Joseph Omog aliyekuwa ameletwa nchini kuinoa Azam FC. Alianza kuinoa timu hiyo tangu mwaka 2013-15 ambapo chini yake aliisaidia Leopards kubeba taji la Ligi Kuu ya Congo msimu wa 2014 bila upoteza mechi na iliruhusu kufungwa bao moja tu na kuifikisha timu hiyo katika Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho ikipoteza mbele ya Sewe Sports ya Ivory Coast hiyo ikiwa imeng’oka Raundi ya Pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huo. Alipotoka AC Leopard alichukuliwa El Hilal ya Sudan kabla ya kutemwa miezi michache baada ya timu kupata matokeo mabaya na kutua timu ya taifa ya Nepal aliyoinoa kati ya 2015-16.

Hizo sio rekodi za mchezo mchezo hata kidogo kwa kocha, ambaye anakuja kuiongoza klabu kama Simba yenye historia tamu barani Afrika. Hata hivyo, Mwanaspoti linapenda kutoa angalizo kwa mabosi wa Simba kubadilika kwani klabu hiyo imekuwa na rekodi mbovu za kutimua makocha kila inapojisikia. Mashabiki wa soka duniani wanaifahamu klabu ya Chelsea ya England, inayomilikiwa na bilionea wa Russia, Roman Abramovich kuwa ndio kinara wa kutimua makocha.

Chelsea imekuwa ikibadili makocha karibu kila msimu hivyo, kuwafanya wachezaji kushindwa kutuliza akili kutokana na kubadilishiwa walimu kila wakati.

Kwa mfano katika kipindi cha miaka miwili tu, Simba imewatimua kazi makocha wake zaidi ya wanne.

Ilianza na Dylan Kerr, ambaye kwa sasa anafanya vizuri kwenye kikosi cha Gor Mahia ya Kenya, kisha ikaachana na Jackson Mayanja, Joseph Omog na Lechantre ambaye amedumu klabuni hapo kwa miezi sita tu.

Tabia ya kutimua makocha kila kukicha mbali ya kuwavuruga wachezaji na kuwashusha viwango, pia inasababisha hasara kwa klabu kulipa fidia kwa kuvunja mikataba pamoja na kuwatishia wengine kuja kuomba ajira kutokana na udhalilishaji huo. Hata hivyo, Mwanaspoti linaamini kuwa mabosi wa Simba ya sasa ambayo ina uongozi mpya, tabia hii ya kuwatimua makocha itapungua ama kukomeshwa kabisa, labda kama atakwenda kinyume na taratibu za klabu ama kuzalisha matokeo ya hovyo.

Kama alivyosema kwenye mkutano wake na waandishi wa habari, Aussems anataka kutengeneza Simba ya Afrika na si ya Tanzania tu, hivyo apewe ushirikiano ili kweli azma hiyo iweze kutimia na kama akishindwa kusiwe na visingizio.