STRAIKA WA MWANASPOTI: Hata miaka ya nyuma, City walipigwa hivi hivi

Tuesday April 10 2018Boniface Ambani

Boniface Ambani 

SOKA ni mchezo wa kufurahisha sana. Ndio mchezo ambao huleta huzuni na furaha dakika yeyote Ile. Kwa kweli wahenga walisema usitabiri matokeo ya mechi kabla mwamuzi apige kipenga cha mwisho ndugu yangu.

Hayo ndio mambo yalifanyika kwenye Uwanja wa Emirates juzi wakati wababe wa soka England walipokutana katika mechi ya Ligi Kuu England wikendi iliyopita. Sio wengine bali ni Manchester Utd na Manchester City. Usitake pima.

Ni mechi ambayo ilikuwa ya kukata na shoka ndugu zangu. Mechi ambayo hakuna shabiki alitaka kuamka alikokuwa ameketi. Kwa balaa lake.

Leo nagusia baadhi ya mechi ambazo Manchester United ilitoka nyuma na kushinda.

Mechi ambazo kila shabiki alikuwa alijua United kashaa poteza. Juzi tuu Manchester City wanaojiita the Citizens mahasimu wa tangu jadi wa Man United walikuwa wanaongoza Kwa mabao 2-0 kufikia mapumziko.

Kipindi cha pili kilipoanza ndugu zanguni, Paul Pogba alipiga mabao mawili ya haraka na kuweza kufanya mambo yawe sawa. Dakika chache baadaye, Chris Smalling alipiga bao la tatu na kuipa Man Utd ushindi, ushindi mkubwa kwenye Uwanja wa Etihad.

Huzuni ilitanda ndani ya uwanja wa Etihad. Iwapo Man City wangeshinda hiyo mechi ndugu zanguni walikuwa wanatawazwa kuwa washindi wa Ligi Kuu England. Sherehe hizo zilikatwa.

Kuna mechi kadhaa tuu ambazo Man Utd washashangaza wengi. Sio mara ya kwanza Utd kumfunga Man City pale kwake.

Mwaka wa 93/94 Manchester United walitoka nyuma pia na wakaifunga Manchester City kwa mabao 3-2 mabao yaliyowekwa kimiani na Eric Cantona (2) kabla Roy Keane kupachika bao la tatu dakika ya 86.

Mwaka wa 2012 Chelsea wakiwa wanaongoza mabao 3-0, United waliamka kipindi cha pili na kusawazisha. Mambo yakawa sare ya 3-3.

Msimu wa 1992, Sheffield Wednesday wakiwa wanaongoza 1-0 hadi dakika ya 86, Steve Bruce alipiga bao la kusawazisha na namo dakika ya mwisho aliongeza bao la pili hatimaye kuipa United ushindi ambao uliwawezesha kushinda taji hilo.

2008/9 Tottenham walichukua uongozi katika mechi ya Ligi Kuu England mapema kweli. Hadi dakika ya 52 walikuwa kifua mbele.

Lakini kilichojiri baadaye ndugu yangu.

Hawakuamini. Mechi iliishia 5-2 mabao yaliyowekwa na Cristiano Ronaldo, Wayne Rooney na Dimitri Berbatov yalisambaratisha Tottenham.

West Bromwich msimu wa 2010/11 United kufikia mapumzikoni walikuwa wamefungwa 2-0.

Lakini juhudi za Wayne Rooney aliyepiga mabao matatu na bao la Javier Hernandez ilikuwa tosha kuiangamiza West Bromwich.

Msimu huu tuu, Man United walipigwa soka dhidi ya Crystal Palace katika kipindi cha pili.

Crystal Palace walikuwa kifua mbele kwa mabao 2-0, lakini Chris Smalling, Lukaku na bao la Nemanja Matic dakika ya mwisho wa mechi hiyo yalihakikishia United alama zote tatu.

Ndugu zanguni, si rahisi kwa klabu kutoka nyuma na kushinda mechi haswa kila mtu alikuwa anajua umeipoteza.

Kwa Man United imekuwa ni Jambo la kawaida tu kwa sababu mara nyingi tuu wamekuwa wakishinda mechi ambazo Kwa kweli kila mtu alikuwa anaona hiyo ushaenda. Jambo kama hilo linahitaji ushirikiano mkubwa haswa kutoka kwa wachezaji kupata matokeo kama hayo. Ushindi wao dhidi ya Manchester City kwa kweli umeonyesha ukomavu wa klabu hiyo.

Kilichobakia kwa Jose Mourinho sasa ni msimu ujao kufanya juu chini kushinda taji hilo.

Taji la huu msimu lishakimbia na Man City.

Wanahitaji kushinda mechi mbili tu wanyakue taji hilo. Kwangu nawapongeza. Sina la ziada Kwa leo. Nawatakia wiki njema.