Digrii zimelala kichwani

Friday December 1 2017

 

LONDON, ENGLAND

WANASOKA wanafahamika zaidi duniani kutokana na uwezo wao wa kucheza mpira.

Hata hivyo, wapo baadhi yao ambao wamekuwa na kitu kingine kinachowafanya wafahamike zaidi nje ya uwanja. Wakati baadhi ya wachezaji wakijitolea nyakati zao zote kwenye soka, wengine wamekuwa wakitumia pia muda wanaopata kujiendeleza kielimu.

Hawa hapa mastaa sita wa sasa na wa zamani ambao, wamekwenda shule na hakika digrii zimelala vichwani mwao.

Edwin Van der Sar

Kipa huyo wa zamani wa Ajax na Manchester United, amelifanya jina lake kuwa maarufu duniani kutokana na uhodari aliokuwa akiufanya anapokuwa kwenye ile milingoti mitatu uwanjani.

Mlinda mlango huyo wa zamani wa kimataifa wa Uholanzi, aliwahi kushinda pia ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na mataji mengine muhimu yaliyompa heshima kubwa katika maisha yake ya soka.

Lakini, hilo halikumfanya Van der Sar kufanya kweli kwenye mambo ya kielimu kwa kuongeza taaluma yake. Baada ya kustaafu soka kwa sasa Van der Sar ni Mkurugenzi wa Masoko wa Ajax Amsterdam na yupo kwenye hatua za mwishoni  kabisa za kupata Shahada ya Uzamili ya Uongozi wa Kimataifa wa Michezo.

Giorgio Chiellini

Mtaliano huyu shughuli yake ni pevu anapokuwa ndani ya uwanja, ni miongoni mwa mabeki mahiri kabisa katika soka la dunia. Ndani ya uwanja, Chiellini, ambaye aliwahi kumweka kwenye matatizo makubwa straika, Luis Suarez, hadi kufikia hatua ya kufungiwa kutokana na kumng’ata kwenye fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2014, amebeba mataji sita ya Serie A na amekuwa akicheza soka lake kwa kutumia akili nyingi.

Umakini wake wa ndani ya uwanja umeendana hadi kichwani pia kutokana na Chiellini kuwa na Shahada ya Uzamili ya Utawala wa Biashara.

Hivyo basi, kwa Chiellini unaweza kumpa ajira awe mchezaji wa kuimarisha safu ya ulinzi, lakini kama hutopenda kufanya hivyo unaweza kumhamishia kwenye masuala ya kibiashara bado akafanya mambo makubwa kabisa.

Frank Lampard

Kwenye soka, Lampard, ameweka jina lake kwenye kumbukumbu za kudumu huko Chelsea baada ya kuwa mfungaji bora wa muda wote katika kikosi cha miamba hiyo ya Stamford Bridge.

Ukiweka kando umahiri wa kucheza soka, Lampard, yupo vizuri kichwani pia kutokana na kuwa na elimu ya ngazi ya shahada.

Kiungo huyo wa zamani wa Manchester City ana shahada ya Latin, somo ambalo alilimudu kwa ufasaha mkubwa na kupata alama A. Lampard siyo kichwa maji, zinachaji na ndiyo maana pengine amekuwa mahiri uwanjani kiasi cha kumfanya kuwa kinara wa mabao huko Stamford Bridge. Licha ya kuwa kiungo, amewazidi washambuliaji waliowahi kuwa kwenye timu hiyo akiwamo Didier Drogba.

Juan Mata

Kwa sasa anacheza soka lake kwenye kikosi cha Manchester United chini ya kocha Mreno, Jose Mourinho. Juan Mata kwa Mourinho amekuwa chini yake mara mbili baada ya awali kuwa naye pamoja walipokuwa Chelsea kabla ya kwenda kukutana tena huko Old Trafford.

Ndani ya uwanja, Mata, ambaye ni Mhispaniola amewahi kushinda Kombe la Dunia, Kombe la Ulaya, Ligi ya Mabingwa Ulaya na mengine kibao yanayofanya kabati lake la mataji kupendeza kweli kweli. Lakini, uwezo wa staa huyo umekwenda hadi nje ya uwanja, baada ya kuwa vizuri kishule kutokana na kwamba kichwani ana Shahada ya Sayansi ya Michezo pamoja na Fedha ikiwa imelala bila ya wasiwasi wowote. Mata alipata shahada yake katika Chuo Kikuu cha Camilo Jose Cela huko Madrid.

Vincent Kompany

Nahodha wa Manchester City huyu. Hakuna ubishi, Vincent Kompany ni mmoja wa mabeki bora kabisa wa kati waliowahi kutokea duniani. Hali ya kuwa majeruhi wa mara kwa mara ndilo jambo linalomsumbua staa huyo na kumfanya ashindwe kutimiza majukumu yake ya uwanjani kwa ufanisi zaidi.

Lakini, jambo hilo halina maana kwamba Kompany anashindwa kufanya vizuri kwenye mambo mengine kwani, beki huyo Mbelgiji amekuwa vizuri kwenye masuala ya kielimu.

Akiwa beki mwenye medali mbili za ubingwa wa Ligi Kuu England, Kompany alijiandikisha kwenye shule ya biashara huko Manchester mwaka 2012 akichukua masomo ya Utawala wa Biashara.

Andrey Arshavin

Unamkumbuka yule mshambuliaji wa Russia? Yule staa wa zamani wa Arsenal, ambaye katika mechi moja dhidi ya Liverpool alipiga bao nne peke yake. Basi bana, yale mashuti yake ya uwanjani na ule ufundi wake wa uwanjani aliokuwa akitaka kuufanya kwa ubunifu mkubwa, unashabihiana na maisha yake mengine ya nje ya uwanja, hasa kwenye masuala ya kielimu. Jamaa sio kilaza hata kidogo, yuko vizuri.

Wakati Arsenal ikimwona kama amefeli alipokuwa kwenye kikosi chao, kumbe katika masuala ya nje ya uwanja na hasa elimu, Arshavin hakufeli. Kwa taarifa yako tu fowadi hiyo na shahada ya ubunifu wa mitindo. Mitindo yake Arshavin ni maarufu sana huko Russia na amekuwa na ubunifu wake kwenye vifaa vya kimichezo pia. Kwa sasa anaendelea kula maisha taratibu bila kokoro.