MAONI YA MHARIRI: Mtibwa Sugar, Yanga zimeonyesha mfano wa kuigwa

WAKATI dirisha la usajili likikaribia kufika ukingoni, kuna mambo machache yaliyofanyika wakati huu wa uhamisho wa wachezaji ambayo hatuna budi kujifunza na kuiga.

Katika dirisha la sasa la usajili ambalo lipo wazi tangu Juni 15, kumekuwa na mshikemshike na vituko vingi, pia limekuwa kama darasa.

Ni dirisha hili ambalo tumeshuhudia Simba ikisajili kikosi kizima pamoja na wachezaji wa akiba. Simba itakamilisha usajili wake kwa kusaini jumla ya wachezaji 13 ambao ni zaidi ya kikosi kizima. Ni jambo la kushangaza kidogo, lakini wenyewe wanasema kikosi chao kilihitaji marekebisho hayo makubwa.

Kituko kingine ambacho kimetokea katika dirisha la sasa la usajili ni kumong’onyoka kwa klabu ya Azam FC ambayo imeachia mastaa wake sita wa kikosi cha kwanza kujiunga na timu nyingine ikiwemo Simba.

Miongoni mwa wachezaji hao ni aliyekuwa kipa bora wa Ligi Kuu kwa miaka miwili mfululizo, Aishi Manula pamoja na aliyekuwa nahodha wao, John Bocco ambaye ameondoka klabuni hapo baada ya miaka 10.

Vituko hivyo pamoja na vingine vingi ni sehemu ya usajili, lakini leo tungependa kuzipongeza Yanga na Mtibwa Sugar kwa kitendo chao cha kuwapa nafasi wachezaji waliokuwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Vijana wenye umri usiozidi miaka 17, Serengeti Boys.

Mtibwa Sugar imewapandisha vijana wake watatu Kibwana Ally, Dickson Job na Nickson Kibabage katika kikosi cha wakubwa baada ya kufanya vizuri na Serengeti Boys ambayo ilishiriki mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa vijana wa umri huo nchini Gabon mapema mwaka huu.

Yanga wao wamemsaini aliyekuwa kipa wa Serengeti, Ramadhani Kabwili ambaye alifanya kazi kubwa kuanzia mechi za kufuzu katika mashindano hayo mpaka mashindano yenyewe. Ni jambo linalotia moyo sana.

Mpaka sasa hatujaona timu nyingine ambayo imefanya usajili wa nyota hao wa Serengeti Boys. Ikumbukwe, kikosi chao kilikuwa na wachezaji zaidi ya 20 hivyo tungependa kuona wanajiunga na timu nyingi zaidi za Ligi Kuu.

Wachezaji wengi wa Serengeti walikuwa na uwezo mkubwa. Nashon Naftal tayari alishapata nafasi katika kikosi cha JKT Ruvu ambacho kitashiriki Ligi Daraja la kwanza mwaka huu baada ya kushuka daraja kutoka Ligi Kuu msimu uliopita.

Nashoni alipata nafasi ya kuichezea JKT Ruvu tangu mwezi Desemba mwaka jana na kuwa mchezaji pekee wa Serengeti aliyeweza kucheza ngazi ya Ligi Kuu.

Wachezaji wengine walioonyesha uwezo mkubwa kama Ally Ng’anzi, Mukhsin Makame, Ally Msengi, Shaaban Zuberi Ada, Ally Mohammed, Assad Ally Juma na wengineo wanastahili kupata timu za Ligi Kuu pia. Wachezaji hawa wana vijapi vikubwa ambavyo vinahitaji mwendelezo.

Unapokuwa na vijana ambao wameshiriki mashindano makubwa kama haya ya Afrika ni wazi ni rahisi kuwaendeleza kwani wanakuwa wamepata darasa kubwa pamoja na hamu ya kusonga mbele.

Kilichofanywa na Mtibwa na Yanga ndicho ambacho kinapaswa kuigwa na timu nyingine za Ligi Kuu.

Azam inaweza isihangaike nao sana kutokana na ukweli wachezaji wao wawili Kabwili na Yohana Mkomola waliondolewa klabuni kwao kimizengwe.

Azam imeamua kujenga upya timu zake za vijana na kujiimarisha kwa ajili ya kuanza kuuza vipaji baadaye. Kwa sasa Azam ina timu za vijana umri chini ya miaka 11, 13, 15, 17 na 20. Ni timu pekee nchini ambayo imejijenga katika misingi hiyo.

Timu nyingine zimeshindwa kutengeneza vijana wao hivyo ni vyema zikasajili hawa ambao tayari wameonekana na uwezo wao umekubalika.

Tulikubaliana kama Taifa kwamba hii ndiyo timu ijayo ya Taifa hivyo hilo haliwezi kufanikiwa kirahisi kama wachezaji hawa hawatapata nafasi ya kucheza na kukuza vipaji vyao. Timu lazima ziwape nafasi.

Tunapenda pia kuwashauri ndugu na walezi wa wachezaji hawa, wasiwakumbatie humo nyumbani kwa kuamini tayari wamekuwa wachezaji wakubwa. Safari ya vijana hawa bado ni ndefu kwani wengi wao bado hawajacheza soka ngazi ya Ligi Kuu.

Walezi na wazazi wao wawatafutie nafasi sehemu nyingine ili waweze kupata nafasi ya kuonekana.

Ni wazi sasa watasajiliwa kwa kiasi kidogo cha fedha lakini hilo siyo la kujali sana kwani baadaye wakifanya vizuri watakuwa na mikataba minono.

Wakipata timu hata za kawaida kama Majimaji, Lipuli, Njombe Mji, Stand United na Mbao FC watakuwa wamepata fursa kubwa ya kuonekana kuliko kuwaacha tu nyumbani.

Timu nazo zipate msukumo kama ilivyo kwa Mtibwa na Yanga ambazo zimeamua kutoa nafasi hiyo. Baada ya muda watakuwa wametutengenezea wachezaji mahiri ambao watalisaidia Taifa.