Tujiandae kisaikolojia na miaka minne mingine ya Malinzi

Friday June 16 2017

 

KILA binadamu ana mtazamo wake. Kuna nyakati ambazo tunakubaliana kuelewana na nyakati nyingine tunakubaliana kutokuelewana. Siyo lazima tuwe na mawazo yanayofanana kila siku. Leo nina mawazo tofauti kidogo.

Kwa tathmini, ni dhahiri kwamba Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, ana nafasi kubwa ya kutetea nafasi yake. Hii ni tathmini tu, usinihukumu. Kuna sababu nyingi za mimi kuamini hilo kuliko kulikataa. Nianze na sababu kwa nini Malinzi ana nafasi kubwa ya kurejea TFF.

Kwanza, hadi sasa Malinzi ndiye kigogo aliyejiandaa zaidi kwa ajili ya uchaguzi. Hakuna mgombea mwingine yeyote wa nafasi hiyo ambaye amejiandaa kuliko Malinzi. Kama yupo mtaje.

Pili, Malinzi ametengeneza ukaribu mkubwa na wapiga kura kuliko mgombea mwingine yeyote. Yaani huku mtaani, watu wengi hawamtaki Malinzi, lakini wale wanaopiga kura, wengi wapo karibu naye. Kama unakataa shauri yako.

Tatu, mpaka sasa hakuna mpinzani mkubwa ambaye amejitokeza kumpa changamoto Malinzi. Kuna taarifa kwamba Ally Mayai anaweza kugombea nafasi hiyo, binafsi ninaamini kama atafanya hivyo anaweza kuwa mpinzani mkubwa wa Malinzi.

Hawa wagombea wengine ninaowasikia, wana sababu nyingi za kushindwa kuliko kushinda. Siamini kama hao wanaotajwa wanaweza kumng’oa Malinzi pale TFF. Si Athumani Nyamlani wala Crescentius Magori. Kwanza wengi wao hawajajiandaa kuwania, wanashinikizwa tu.

Sababu ya nne na ya mwisho ni kwamba Malinzi ndiye rais wa sasa wa TFF. Mara nyingi mtu anayekuwa katika ofisi, akigombea tena ana nafasi kubwa ya kushinda. Huwa inatokea mara chache mtu wa aina yake akaanguka.

Mtu aliyepo kwenye mfumo ni ngumu kumwangusha, kwa kuwa kona zote anazifahamu, labda kama kutakuwa na nguvu ya ziada kutoka nje. Hii ndiyo sababu viongozi wengi wanaongoza kwa vipindi vyote viwili. Hizi ndizo sababu chache zinazoonyesha kwamba huenda Malinzi akapata miaka mingine minne ndani ya TFF.

Je, kuna tatizo Malinzi akiongezewa muda wa kuiongoza TFF? Ndiyo, tatizo lipo, tena kubwa sana. Tatizo kubwa ni kwamba Malinzi anakwenda kulizika soka letu kabisa. Baada ya miaka minne sidhani kama tutakuwa tumepiga hatua yoyote kwenda mbele.

Binafsi, ninaamini kwamba mpaka hapa tulipofika, Malinzi ameuharibu mpira wetu kuliko kuutengeneza. Yapo machache mazuri aliyoyafanya, haina ubishi, lakini haikuwa kwa sababu ya mpira wetu, ilikuwa tu kujitengenezea mazingira ya kura. Mfano hili la Serengeti Boys kwenda Gabon kupitia mezani.

Ukisoma Ilani yake ya uchaguzi, Malinzi ametekeleza mambo mengi aliyoahidi lakini ameongeza matatizo mengi zaidi. Yaani amefanya mambo manne mazuri lakini akaharibu mengine 10. Mfano, aliahidi kuongeza mashindano mengine, akaleta Kombe la FA na kinachofanyika mnakiona.

Kwanza, fedha za wadhamini hazifiki kwenye klabu kwa wakati. Pili, mechi za FA zimekuwa ni kiza kitupu. Hakuna ratiba ya wazi. Hakuna uamuzi wa haki. Inaonekana kabisa mashindano yametengenezwa kuzibeba timu fulani.

Mwaka huu Azam na Polisi Dar walikuwa wahanga wa michuano hiyo. Polisi Dar walikata rufani, kanuni zikapindishwa kwa matakwa ya timu fulani. Azam iliishia nusu fainali kwa kuumizwa na mwamuzi. TFF ya Malinzi iko wapi? Imelala.

Ahadi nyingine ya Malinzi ilikuwa ni kuongeza waamuzi wa Tanzania kuchezesha mechi za kimataifa na pia kupandisha viwango vyao. Waamuzi wa kati wanaochezesha mechi za kimataifa kwa sasa ni wanne tu. Labda ndiyo ongezeko alilotuahidi. Kwa kipindi cha miaka yake, waamuzi hao wamebaki hao hao wanne.

Ukirejea kwenye viwango vya waamuzi wa mechi za Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza ndipo utakapoamini kwamba Malinzi akichaguliwa tena itakuwa ni majanga. Viwango vya waamuzi vinatia huruma. Msimu uliopita waamuzi karibu 20 walifungiwa.

Hapa ndipo alipotufikisha Malinzi. Hakuna anayemwogopa tena. Leo anafungiwa mwamuzi fulani, kesho anaharibu mwamuzi mwingine. Hakuna anayejali. Wamefungiwa mpaka karibu wanakwisha wote, lakini hakuna anayejadili. Pengine Malinzi anafahamu zaidi ni kwanini wanafanya hivyo.

Kwa viwango vya waamuzi wa sasa vilivyoshuka, unajiuliza hali itakuwaje miaka minne ijayo Malinzi akiwa madarakani? Kwa kweli tupo kwenye matatizo. Wazungu wanasema ‘We are in trouble’ my dia kaka.

Malinzi ameifanya Ligi Kuu kuwa ya vurugu. Msimu uliopita tumeona uchafu wa Simba na Kagera Sugar. Tumeona namna ratiba inavyopanguliwa kila siku. Mechi zinapangwa kwa kujuana na uonevu. Pata picha akichaguliwa tena tutakuwa tunakwenda wapi.

Stars aliyoikuta Malinzi na iliyopo sasa ni vitu viwili tofauti. Malinzi aliikuta Stars ikiwa moto, inapambana ndani na nje ya nchi. Ilikuwa inatunishiana misuli na timu za Morocco na Ivory Coast. Leo hii Stars inatoka sare nyumbani, tena na Lesotho. tars wakati wa Malinzi ilipigwa mabao 7-0 na Algeria, haikuwahi kutokea tangu nchi imepata uhuru. Kwa sasa timu hiyo haina mvuto tena, imeyumba kabisa. Unajiuliza Stars itakuwaje miaka minne baadaye kama Malinzi ataendelea kuwa Rais wa TFF. Tunaelekea katika janga la kitaifa au ndiyo kete ya Serengeti Boys? Kinachoumiza ni vipi mpira utaishi hadi mwaka 2021?