Hatma ya msimu wa Liverpool ni wiki hii

Tuesday May 8 2018

 

By OLLE BERGDAHL MJENGWA

MSOMAJI, Liverpool imekuwa na msimu mzuri, imefikia fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Mohamed Salah amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu England (EPL) na kocha wao Jurgen Kloop anawania tuzo ya Kocha Bora England.

Bado Salah ana nafasi kubwa ya kutwaa Kiatu cha Dhahabu katika EPL akiwa anaongoza katika ufungaji bora mpaka sasa.

Hata hivyo, Liverpool ipo katika hatari ya kupoteza kazi kubwa na mafanikio ambayo imeyapata msimu huu.

Liverpool ina lengo la kupiga hatua kubwa zaidi kila msimu. Na katika miaka inayokuja ni muhimu sana kwa klabu hiyo kuendelea kushiriki katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Ni kwa kuwa mashindano hayo yanasaidia uchumi wa klabu nyingi zinazoshiriki kutokana na kila klabu kupata fedha nyingi kila hutua inavuka katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Lakini, muhimu zaidi ni kwamba wachezaji bora duniani wanataka kucheza katika Ligi ya Mabingwa Ulaya na hivyo ni rahisi zaidi kwa klabu ambayo inashiriki katikia michuano hiyo kusajili wachezaji wenye vivango vikubwa. Sehemu kubwa ya msimu kumekuwa na ishara nyingi kwamba Liverpool itafanikiwa kunasa moja ya nafasi nne za juu katika Ligi Kuu na kufuzu kushiriki katika Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao pia.

Lakini, katika takriban mwezi mzima sasa Liverpool imeshindwa kupata matokeo katika Ligi Kuu ya England.

Wikiendi iliyopita ilifungwa na Chelsea bao 1-0 na katika mechi zake tano za mwisho imeshinda mechi moja tu. Hapa kuna swali la kujiuliza, je, Liverpool itacheza mechi yake ya mwisho katika Ligi Kuu wiki hii. Ni mechi ya nyumbani dhidi ya Brighton, itaweza kupata matokeo?

Ikishindwa kuchukua pointi tatu basi kuna uwezekano itaishia katika nafasi ya tano kama Chelsea itashinda mechi zake mbili za mwisho dhidi ya Hudersfield na Newcastle.

Hakika sababu moja ya Liverpool kupoteza pointi nyingi katika Ligi Kuu katika wiki za hivi karibuni ni kutokana na kocha wa timu hiyo kuwapumzisha wachezaji wengi katika mechi za Ligi Kuu kabla mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Lakini pia kuna ishara kwamba wachezaji wa Liverpool wamechoka. Katika mfumo wa Kloop wachezaji wote huhitaji kujituma na kukimbia sana.

Na kutokana na Liverpool kutokuwa na kikosi kipana sana wachezaji kama Salah, Sadio Mane, na Roberto Firmino wamecheza katika takriban mechi zote. Hivyo sio jambo la kushangaza sana kwamba hali yao ya kimpira imeshuka kidogo katika mechi za hivi karibuni katika Ligi Kuu.

Bila shaka Liverpool bado ina nafasi ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya hata kama itaishia katika nafasi ya tano katika Ligi Kuu kama itachukua ubingwa wa Ligi ya

Mabingwa Ulaya itakapocheza fainali dhidi ya Real Madrid, Mei 26 mwaka huu.

Kuna desturi kwamba mshindi wa mashindano hayo anafuzu moja kwa moja kushiriki katika Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu unaifuata.

Pamoja na kuwapon kwa njia hiyo, hata hivyo, bila shaka nafasi ya Liverpool kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya ni kuifunga Brighton katika mechi yake ya mwisho ni kubwa kuliko klabu hiyo kuifunga RealMadrid katika fainali ya Ligi ya Mabingwa.

Hivyo, huenda hatima ya msimu wa Liverpool ipo katika mechi yao dhidi ya Brighton wikiendi hii.