Ruby, Nandy wapishana jukwaani ZIFF

Muktasari:

  • Ruby na Nandy walitakiwa kutumbuiza jana kwenye jukwaa moja kwa nyakati tofauti, lakini ilishindikana kutokana na Nandy kutofika na matokeo yake alipanda Ruby peke yake.

Zanzibar. Wanamuziki nyota wa Bongo Fleva nchini, Hellen George ' Ruby na Faustina Charles  ‘Nandy’ usiku wa kuamkia leo Ijumaa wameshindwa kuimba kwa wakati mmoja katika tamasha la ZIFF linaloendelea katika viwanja vya Ngome Kongwe Zanzibar.
Ruby na Nandy walitakiwa kutumbuiza jana kwenye jukwaa moja kwa nyakati tofauti, lakini ilishindikana kutokana na Nandy kutofika na matokeo yake alipanda Ruby peke yake.
MCL Digital ilizungumza na uongozi wa ZIFF ambapo ulisema, ratiba ilibadilishwa hivyo Nandy atapanda jukwaani leo.
"Ni kweli kutokana na Ratiba inaonyesha inatakiwa Nandy na Ruby waimbe jana, pia Aslay na The Mafiki wataimba leo, sasa ratiba ilibadilika kwa Nandy hivyo ataungana na kina Aslay leo," alisema Daniel Nyalusi  ambaye ni Meneja wa Tamasha la ZIFF.
Hata hivyo, jana watu waliokuwa wamehudhuria katika Viwanja vya Ngome Kongwe, walionekana kuwa na Shauku kubwa ya kuona Nandy na Ruby wakitoa burudani katika steji moja.