Yanga yapiga hesabu kali Ligi ya Mabingwa

Dar es Salaam. Wakati wawakilishi  wanne wa Tanzania kwenye mashindano ya klabu Afrika wakiingia kibaruani mwishoni mwa wiki hii, Yanga itapaswa kupiga hesabu kali.
Yanga itaiwakilisha Tanzania Bara kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika sanjari na JKU ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu Zanzibar.
Simba itaungana na Zimamoto ya Zanzibar kuiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika Jumapili.
Hata hivyo, Simba na Yanga zinaweza kuathirika katika mashindano ya kimataifa endapo zitashindwa kujipanga kikamilifu.
 Timu hizo zinakabiliwa na mashindano mengine ambayo yatazilamisha kucheza idadi kubwa ya mechi ndani ya muda mfupi, jambo linaloweza kuchangia uchovu kwa wachezaji.
Yanga inaweza kupata athari zaidi kwa kuwa imekuwa ikisumbuliwa na tatizo sugu la majeruhi lililochangia kutumia kikosi chenye idadi ndogo ya wachezaji ambao watalazimika kucheza mechi mfululizo na kufa au kupona.
Yanga itacheza na St. Louis ya Shelisheli kesho Jumamosi, itakuwa na kibarua cha mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Majimaji ambayo itachezwa katikati ya wiki inayofuata jijini Dar es Salaam.
Timu hiyo italazimka kusafiri hadi Shelisheli kwa mechi ya marudiano ambayo itachezwa mwishoni mwa wiki ijayo na baada ya hapo itapumzika siku zisizozidi tatu kabla ya kwenda Mtwara kuikabili Ndanda.
Simba baada ya kuivaa Gendarmarie ya Djibout, katikati ya wiki ijayo itakwaana na Mwadui mkoani Shinyanga kabla ya kwenda Djibouti kwa mechi ya marudiano itakayochezwa mwishoni mwa wiki ijayo na baadaye itarudi kukabiliana na Mbao jijini Dar es Salaam.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa alisema wamejipanga kukabiliana na ratiba hiyo ingawa inawapa muda mfupi wa kupumzika na kutekeleza ipasavyo programu.
“Sidhani kama majeruhi wanaweza kutuzuia kutimiza tulichokipanga kama watu wanavyoamini. Timu iko imara ndio maana tunapata matokeo mazuri licha ya kuwakosa wachezaji wetu muhimu,” alisema Nsajigwa.
Kocha Msaidizi wa Simba, Masoud Djuma alisema wana kikosi kipana chenye uwezo wa kucheza idadi kubwa ya mechi mfululizo bila kutetereka.