Yanga yataka ushindi asubuhi

Muktasari:

Yanga inahitaji ushindi au sare ya aina uouote ile ili ifuzu kwenda raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambako watakutana na mshindi  baina ya El Merreik ya Sudan na Township Rollers ya Botswana.

Shelisheli. Mastaa wa Yanga kwa nyakati tofauti wameahidi kuibuka na ushindi katika mechi ya kesho ugenini dhidi ya St. Louis na kwa ujasiri zaidi wamepanga mechi hiyo kumalizika ndani ya dakika 90.

Yanga inahitaji ushindi au sare ya aina uouote ile ili ifuzu kwenda raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambako watakutana na mshindi  baina ya El Merreik ya Sudan na Township Rollers ya Botswana.

Wawakilishi hao wa Tanzania wamekuwa hawana rekodi nzuri ya upigaji penati katika siku za hivi karibuni jambo ambalo limewafanya wachezaji wake kujipanga kwa hali na mali kupata ushindi katika muda wa kawaida wa mchezo ili mechi hiyo isiamriwe kwa mikwaju ya penati.

"Sisi nia yetu ni kupata ushindi ugenini na tunawaomba Watanzani na mashabiki wa Yanga popote walipo kuwa na imani  kutuombea ili tufanikishe nia yetu.

Tumejipanga kufunga mabao ya mapema na kuyalinda ili tusijiweke kwenye mazingira magumu au kusababisha mechi iende kwenye penati. Kwa molali tuliyonayo naamini tutafanya vizuri," alisema Nadir Haroub 'Cannavaro'

Kipa Ramadhan Kabwili alisema St. Louis hawana timu ya kutisha na hadhani kama watawapa wakati mgumu.

"Ni timu ya kawaida na hata mechi ya kwanza walikuwa na bahati sisi kuwafunga bao 1-0. Naamini kwenye mchezo huu tutawamaliza mapema kwani watataka kufunguka jambo ambalo litawaumiza wao wenyewe," alisema Kabwili.