Yanga iungwe mkono kesho Taifa dhidi ya Medeama

Wachezaji wa Yanga

Muktasari:

  • Yanga ipo Kundi A katika michuano hiyo ya pili kwa ukubwa kwa ngazi ya klabu Afrika baada ya Ligi ya Mabingwa Afrika sambamba na Mo Bejaia ya Algeria na TP Mazembe ya DR Congo inayoongoza msimamo wa kundi hilo ikiwa na pointi sita.

MABINGWA wa soka nchini, Yanga ambao ni wawakilishi pekee wa Tanzania katika michuano ya kimataifa, kesho Jumamosi watashuka tena uwanjani kuvaana na timu ya Medeama ya Ghana katika mechi yake ya tatu ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga ipo Kundi A katika michuano hiyo ya pili kwa ukubwa kwa ngazi ya klabu Afrika baada ya Ligi ya Mabingwa Afrika sambamba na Mo Bejaia ya Algeria na TP Mazembe ya DR Congo inayoongoza msimamo wa kundi hilo ikiwa na pointi sita.

Katika mechi zake mbili za awali, moja ikicheza ugenini dhidi ya Mo Bejaia na nyingine ya nyumbani dhidi ya TP Mazembe, Yanga ilichezea kichapo cha bao 1-0 kila mechi na kujikuta ikiburuza mkia ikiwa haina pointi hata moja.

Medeama wanaovaana nao kesho kwenye Uwanja wa Taifa, ipo juu ya Yanga ikiwa na pointi moja katika mechi zake mbili, ikipoteza kwa Mazembe na kulazimisha suluhu kwa Bejaia ambayo inashika nafasi ya pili ikikusanya pointi nne.

Kwa kuangalia msimamo wa kundi hilo, Yanga ina kazi kubwa katika pambano la kesho li angalau ipate ushindi wake wa kwanza utakaowapa pointi tatu ambazo zitafufua matumaini yao ya kucheza hatua ya nusu fainali ikiwa ni rekodi kwao.

Tangu Yanga ianze kushiriki michuano ya kimataifa ya Afrika, rekodi ya kujivunia kwao ni kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa mwaka 1998 na mwaka huu katika Kombe la Shirikisho.

Pia, imewahi kufika robo fainali mara mbili mfululizo katika Ligi ya Mabingwa (enzi ikifahamika kama Klabu Bingwa Afrika) mwaka 1969 na 1970 kabla ya kufika hatua kama hiyo katika michuano ya Kombe la Washindi mwak 1995.

Michuano hiyo ya Kombe la Washindi iliyoasisiwa mwaka 1975 ilikuja kuunganishwa na michuano ya Kombe la CAF mwaka 2004 na kuzaliwa kwa michuano hii ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo Yanga mwaka huu imeingia hatua ya makundi.

Kwa namna yoyote ilivyo, Yanga inahitaji kushinda mechi yake ya kesho, lakini pia kuna haja kubwa kwa mashabiki wa soka ambao wamepata bahati ya kupungiziwa viingilio kutoka Sh 5,000-30,000 na kuwa Sh 3,000-10,000 tu kujitokeza kwa wingi Uwanja wa Taifa ili kuipiga tafu Yanga.

Hakuna ubishi kuwa, Yanga ndio wawakilishi pekee wa Tanzania kwa sasa katika michuano ya kimataifa, pia wanaiwakilisha Ukanda wa Afrika Mashariki, kitu ambacho Watanzania ni lazima wajivunie kwa jambo hilo bila kujali itikadi zao. Mwanaspoti inaamini kuwa umoja siku zote ni nguvu na ushindi, hivyo mashabiki wa soka waweke kando ushabiki na kujitokeza kwa wingi ili kuhakikisha wawakilishi wao wanapata ushindi mbele ya Waghana.

Ile aibu ya mashabiki kushangilia wapinzani na kuwapa nguvu haipendezi hata kama hakuna sheria inayombana mtu kufanya hivyo, kwani huwa tunawashangaza hata wageni kuona tunawapa nguvu wageni na kuwanyong’onyesha wenyeji.

Mashabiki kokote kwenye mchezo hususan wa soka kwa timu iliyo nyumbani ni sawa na mchezaji wa ziada wa kikosi cha timu wenyeji, hivyo tunahimiza mashabiki waonyeshe uzalendo kwa Watanzania wenzao ili kuhakikisha Medeama inalala.

Ni kweli ni jukumu la Yanga kuhakikisha inapambana uwanjani kusaka ushindi na kuepuka kufanya makosa.