Yanga isahauni Simba, fikirieni kimataifa

Muktasari:

  • Mashabiki hao na wanachama wa klabu hiyo walikuwa na kila sababu ya kufurahia ushindi huo kutokana na upinzani wa jadi uliozoeleka baina ya timu hizo.
  • Kabla ya mechi hiyo mashabiki wa pande hizo mbili walikuwa wakitambiana na hivyo inaeleweka wazi hali wanayokuwa nayo mashabiki wa timu inayoshindwa.

        JUZI Jumanne usiku mashabiki wa Simba walikuwa na furaha isiyo kifani baada ya timu yao kufanikiwa kuitoa Yanga katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi.

Mashabiki hao na wanachama wa klabu hiyo walikuwa na kila sababu ya kufurahia ushindi huo kutokana na upinzani wa jadi uliozoeleka baina ya timu hizo.

Kabla ya mechi hiyo mashabiki wa pande hizo mbili walikuwa wakitambiana na hivyo inaeleweka wazi hali wanayokuwa nayo mashabiki wa timu inayoshindwa.

Ni kweli kwamba kushindwa ni kubaya hasa pale unaposhindwa na mpinzani wako wa jadi ambaye kabla ya mechi hiyo kila mmoja wenu alitamba kumshinda mwenzake lakini matokeo hayo ya kushindwa si mwisho wa kila kitu katika soka.

Yanga bado wana nafasi nyingine ya kurudiana na Simba na kuonyesha ubora wao katika mechi ijayo ya Ligi Kuu Bara ambayo kwa mujibu wa ratiba ya ligi hiyo itachezwa baadaye mwezi ujao.

Hata hivyo, tunafahamu ukweli kwamba hasira za kushindwa huku haziishi kwa mashabiki tu, bali hata wachezaji na wakati mwingine viongozi hujikuta katika wakati mgumu pindi timu mojawapo inaposhindwa.

Na kwa matokeo ya juzi moja kwa moja tunaizungumzia Yanga ambayo ilitolewa kwa mikwaju ya penalti 4-2 baada ya kutofungana katika dakika 90 za kawaida.

Hatutashangaa kusikia baadhi ya viongozi na watu wenye nguvu ndani ya Yanga wakianza kunyoosheana vidole na kutafuta wachawi kutokana na matokeo hayo kwa imani kwamba walikuwa na kila sababu za kushinda mechi hiyo.

Kibaya zaidi hao ambao wana hulka ya kuwanyooshea vidole wenzao hawana ushahidi wowote wa kiufundi au wa aina yoyote ile kuthibitisha kwamba kuna mchezaji kaihujumu timu yao au kuna mapungufu ya aina yoyote.

Ukweli huu ndio unaotufanya tuwakumbushe Yanga kwamba kuna mechi nyingine dhidi ya Simba lakini pia mechi dhidi ya Simba sio mwisho wa safari yao, badala yake wana mtihani mkubwa mbele yao.

Na hapa tungependa kusikia viongozi na wanachama wa Yanga wanafikiria zaidi mtihani wao wa kimataifa katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Haipendezi na si sahihi kwa Yanga kusahau mtihani huo mkubwa na kuifikiria mechi ya Simba kwa kusaka mchawi na wakati mwingine kukurupuka na kuanza kuwalaumu baadhi ya wachezaji kwa hisia kwamba walihujumu mechi hiyo.

Hatukatai ukweli kwamba mambo ya hujuma yapo, na yamekuwa yakifanyika lakini si sahihi kuruhusu hisia kutawala katika jambo hili badala ya uhalisia.

Kuruhusu hisia zitawale jambo hilo ni mwanzo wa kuharibu kila kitu na kama Yanga watalikubali jambo hilo ni wazi kwamba mbio zao katika mashindano ya kimataifa zitaingia doa na kuwaweka katika wakati mgumu.

Tungependa kuona mechi ya Simba inakuwa kama sababu ya kuiimarisha Yanga katika mbio zao za kimataifa badala ya kuwa chanzo cha mgogoro baina ya wachezaji na viongozi hasa mgogoro wenyewe unapotokana na mambo ya hisia.

Mechi hiyo inatakiwa kuwa na changamoto kwa Yanga na kufanya jitihada zaidi ili kuweza kufanya vizuri katika michuno ya kimataifa.

Yanga inapaswa kuchukulia kwa umakini sana suala la upigaji penalti kwani hii siyo mara ya kwanza timu hiyo kutolewa katika changamoto hiyo. Inawezekana kabisa Simba imeikumbusha Yanga kuwa timu yao bado haijakomaa katika upigaji wa penalti kwani msimu wa mwaka 2014/15 Yanga ilitolewa na Aly Ahly ya Misri katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa kwa matuta. Hivyo, Kocha George Lwandamina anatakiwa kujipanga zaidi.