Yanga, Simba zikaze msuli zaidi vita vyao vya Afrika

WAWAKILISHI wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga, juzi Jumanne waliianza vibaya raundi ya kwanza kwa kufungwa nyumbani mabao 2-1 na Township Rollers ya Botswana.

Matokeo hayo yamewanyong’onyesha mashabiki wa Yanga na hata wachezaji wa klabu hiyo, kwani sasa wana kazi kubwa katika marudiano ya siku 10 zijazo huko Gaborone.

Yanga iliingia kwenye mechi hiyo ikiwa na matumaini ya kufanya vizuri, ni bahati mbaya soka huwa halitabiriki, hivyo ikapata matokeo hayo yanayoifanya kuwa na kazi ya kushinda ugenini si chini ya mabao 2-0 ili isonge mbele.

Hayo ni matokeo mabaya kwa Yanga kwenye uwanja wake wa nyumbani tangu ilipofungwa na TP Mazembe mwaka 2016, kwani rekodi zinaonyesha katika mechi za nyumbani Yanga wamekuwa wakifanya vizuri kwa muda mrefu.

Hata hivyo licha ya ugumu iliojiwekea kuelekea marudiano ya Machi 17, matokeo hayo yasiwakatishe tamaa wachezaji wa Yanga badala yake wayachukue kama changamoto kwao na kwenda kulipa kisasi.

Kitu cha kufurahisha ni kwamba kwa miaka ya karibuni, Yanga imekuwa ikicheza kwa kujiamini ikiwa ugenini, ni wajibu wa wachezaji kuhakikisha wanapata matokeo mazuri ili kusonga mbele.

Yanga inaweza kabisa kusonga mbele kama wachezaji wake wataamua kucheza kwa bidii kubwa na kujitoa kwa masilahi ya klabu yao kwa sababu kama Township imeshinda ugenini kwanini wao nao wasiweze?

La muhimu ni benchi la ufundi la Yanga chini ya kocha George Lwandamina kufanyia kazi mapungufu yaliyoonekana kwenye pambano la kwanza.

Tunaamini Lwandamina na wasaidizi wake wameona tatizo lililowaangusha juzi kwa baadhi ya wachezaji kukosa nidhamu ya uchezaji na kujisahau.

Kadhalika kuna tatizo la kukosekana kwa baadhi ya nyota wa Yanga, lakini kwa vile wapo wengine wameanza kurejea ni lazima waanze kuandaliwa kwa mchezo huo ujao.

Hata kama Yanga bado ina nafasi ya kuendelea kushiriki michuano ya Afrika kwa kuangukia Kombe la Shirikisho kama itang’olewa Ligi ya Mabingwa, bado inapaswa kupigia hesabua michuano waliyopo sasa.

Kiwango cha fedha zinazolipwa kwa klabu zinazoingia makundi ndizo zinazofanya timu nyingi za mataifa mengine kujituma vilivyo, jambo ambalo hata wachezaji wa Yanga nao wanapaswa kulifanya.

Sh 1.3 bilioni si fedha ndogo kulinganisha na Sh600 zinazotolewa Kombe la Shirikisho kama timu ikitinga makundi. Fedha hizo ni nyingi na zinaweza kutatua matatizo mengi ya kiuchumi ya Yanga.

Ndio maana tunawakumbusha wana Yanga waanze kujipanga sasa na kukomalia waitoe Township, ili wavune fedha hizo mbali na heshima watakayoweka nyota wa klabu hiyo kwa kuipeleka timu makundi ikiwa ni mara ya pili kihistoria.

Yanga ilitinga hatua hiyo mara ya kwanza na mwisho kwa Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1998 kabla ya kurudia tena katika Kombe la Shirikisho mwaka 2016, hivyo kufuzu kwao ni heshima kwa wachezaji waliopo katika kikosi cha sasa.

Nani asiyependa kuandika historia tamu kama hiyo? Ndio maana tunawahimiza wachezaji wa Yanga kwa kusema ni kweli wameumizwa na matokeo ya juzi, lakini bado wana nafasi ya kupindua meza ugenini.

Muhimu wazingatie maelekezo ya makocha wao na viongozi wajipange ili kuona kila kitu kinakuwa sawa, ili watakapoenda kurudiana na Township wawe na kiu ya kuhakikisha wanatoka na ushindi ugenini na mwishowe kuweke historia Afrika.

Mwanaspoti inawaombea kila la heri Yanga kwa maandalizi itakayofanya kwa ajili ya mechi ya marudiano ugenini ili ipate matokeo bora zaidi.

Jana usiku, nayo Simba inayocheza Kombe la Shirikisho ilikuwa na mechik dhidi ya Waarabu Al Masry ya Misri.

Kwa matokeo yoyote ambayo Wekundu wa Msimbazi hao watakuwa wameyapata, nao pia tunapenda kuwaasa kujituma zaidi kwani mechi ya marudiano ugenini nayo ni ngumu kwao lakini yenye nafasi ya kuwapeleka mbele.

Kama ilivyo kwa Watanzania wengine, Mwanaspoti nalo linapenda kuona Simba na Yanga zikisonga mbele.