Wenger amweka sokoni Sanchez kiana

Saturday January 13 2018

 

London, England. Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger ameanza kukubali kuwa Alexis Sanchez ataondoka mwezi huu wakati akijiandaa kutafuta nyota wengine wa kuziba nafasi ya Mchile huyo.

Manchester City na Manchester United zote zimeonyesha nia ya kutaka kumsajili mshambuliaji huyo, ambaye mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu, na sasa uenda akacheza mechi yake ya mwisho leo kati ya Arsenal dhidi ya Bournemouth.

Wenger amekuwa akihusishwa na kumfuata nyota wa Bordeaux, Mbrazili Malcom pamoja na Thomas Lemar wa Monaco kuziba pengo la Sanchez.

Wakati alipoulizwa kama Sanchez ataendela kubaki Arsenal kama atashindwa kumpata mrithi wake, Wenger alisema: "Umeliweka swali lako vizuri sana."

"Alexis ni mchezaji mzuri wa kiwango cha juu na kama ataondoka, itatupa wakati mgumu kupata mrithi wake kwa haraka," aliongeza Mfaransa huyo.

Kocha huyo wa Arsenal alisema: "Nimekuwa na mazungumzo mengi kuhusu yeye ni wazi watu wengi wanataka kujua baada ya kubaki muda mfupi kwa mkataba wake, lakini sijawahi kuwa na wasiwasi kuhusu weledi wake uwanjani. Alexis anachotaka ni kushinda. Unapomuona amekasirika ni kwa sababu hatujashinda."