Washelisheli waipa Yanga ushindi

Muktasari:

Katika mchezo wa kwanza Yanga kuibuka na ushindi kiduchu wa bao 1-0 nyumbani siku 10 zilizopita, wenyeji bado wanaamini wana kibarua kizito cha kupenya mbele ya mabingwa hao wa Tanzania Bara

Victoria,Shelisheli. Pamoja na kuhitaji ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Yanga ili wafuzu hatua inayofuata ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wenyeji St. Louis wameingiwa hofu ya kupata matokeo mazuri kwenye mchezo wa leo.

Katika mchezo wa kwanza Yanga kuibuka na ushindi kiduchu wa bao 1-0 nyumbani siku 10 zilizopita, wenyeji bado wanaamini wana kibarua kizito cha kupenya mbele ya mabingwa hao wa Tanzania Bara.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Soka la Shelisheli, Georges Bibi alisema siyo kazi rahisi kwao kuwatoa Yanga kama wengi wanavyofikiria na wana mlima mrefu wa kupanda ili hilo litimie.

"Nadhani sisi tuko kwenye presha kubwa kuliko Yanga kwa sababu tutatakiwa kupata ushindi wa idadi kubwa ya mabao tofauti na wenzetu ambao matokeo ya aina nyingi yanaweza kuwavusha.

Sikuwepo Tanzania kwenye mchezo wa kwanza, lakini waliokwenda waliniletea taarifa kwamba Yanga walicheza vizuri ingawa walipoteza idadi kubwa ya mabao lakini pia walikosa penalti.

“Kwa kuliangalia hilo tu unaweza kukubaliana na mimi kwamba tunakutana na wapinzani wenye ubora na uzoefu wa hali ya juu kulinganisha na sisi ambao kwa sasa ndio tumeanza kupiga hatua," alisema Bibi.