Tshishimbi, Ajibu wamgusa mzungu

KOCHA mzungu wa Township Rollers ya Botswana, Nikola Kavazovic, amechekelea timu yake kuondoka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Yanga, lakini amekiri kazi bado haijaisha huku akisema ameondoka na majina mawili ya nyota wa Jangwani.

Kocha huyo Mserbia, alisema mziki wa Ibrahim Ajibu, Obrey Chirwa na Kabamba Tshishimbi, umemgusa na anakwenda Gaborone kufanya kazi ya ziada ili nyota hao wasije wakamtibulia kwenye mchezo wa marudiano utakaopigwa Machi 17.

Kavazovic amesema umahiri wa wachezaji hao uliwasumbua vijana wake licha ya ushindi huo na sasa wanarudi kwao kujipanga upya kuwazuia ili wasilete madhara kwani, anaamini nyota hao ndio wanaoweza kupindua meza wakiwa nyumbani kwao.

Akizungumza mara baada ya pambano hilo lililopigwa juzi Jumanne Uwanja wa Taifa katika mchezo wa kwanza wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Kavazovic alisema Ajibu ni mchezaji mzuri anayeweza kumiliki na kuuchezea mpira na anayetengeneza nafasi nyingi za kufunga.

Alisema hata kutolewa kwake katika kipindi cha pili, ilikuwa nafuu kwao na kuwapa nafasi mabeki wake kuwa na uhuru na ndio maana haikuwa ajabu kupata bao la pili lililokuwa la ushindi.

Pia, alisema Tshishimbi ana uwezo wa kupiga pasi za mbali na karibu, yupo vizuri katika kukaba na aliweza kushindana na wachezaji wake kwa kiwango, ilihali Chirwa alikuwa msumbufu kwa mabeki wake na anahisi wanaweza kuwa kikwazo kwao.

“Kama nilivyopata muda wa wiki tatu kuwaangalia Yanga nitafanya hivyo kwa kuwaangalia tena vizuri Ajibu, Chirwa na Tshishimbi kwani nimewaona ni mhimili na wasumbufu, hivyo naondoka nikienda kuwatafutia dawa katika mechi ya marudiano,” alisema.

“Yanga si timu ya kuibeza kama tumeweza kupata ushindi hapa kwao, hata wao wanaweza kupata ushindi kwetu, hivyo tutajitahidi kuangalia jinsi ya kuwazuia na kupata matokeo ya kusonga mbele,” alisema Kavazovic.

WALISTAHILI KIPIGO

Kocha Msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa amekiri timu yake ilistahili kipigo walichopewa na Waswana hao kutokana na makosa kadhaa yaliyokuwa yakifanywa na vijana wake kwenye mchezo huo na hasa kuwaacha wageni wamiliki mpira watakavyo.

Nsajigwa alisema hata hivyo kuelekea mechi hiyo ya marudiano, watafanya marekebisho kupitia mechi za Ligi Kuu watakazocheza ikiwamo ya Ijumaa dhidi ya Kagera Sugar ili kuona wanakwenda jijini Gaborone kupindua meza.

“Wapinzani wetu walicheza kitimu zaidi na si uwezo wa mchezaji mmoja mmoja, walikuwa wakishambulia na kukaba wote kitimu, tulifanya makosa yaliyotupa zawadi ya kipigo. Hata hivyo, tutajipanga kurekebisha makosa,” alisema.

Yanga inahitajika kupata ushindi usiopungua mabao 2-0 kama inataka kuvuka kuingia hatua ya makundi, vinginevyo ijiandae tu kucheza play-off ya Kombe la Shirikisho Afrika ili kusaka tiketi ya makundi kwa michuano hiyo ambayo Simba wanashiriki kwa sasa.