TFF isinyamazie kabisa vitendo hivi vya kihuni

Monday January 9 2017Rais wa TFF Jamal Malinzi

Rais wa TFF Jamal Malinzi 

By Mwanaspoti

SOKA ni mchezo wa furaha, amani na urafiki, ndiyo maana mara zote Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) limekuwa likihimiza mchezo wa kiungwana (fair play).

Kuthibitisha kuwa soka sio vita au uhamasa, wachezaji wa timu zote, makocha bila kujali timu zao zimepata matokeo gani ama wametoleana lugha gani ndani ya dakika za mchezo, mara tu unapokwisha hukumbatiana na kupongezana.

Kuonyesha kuwa soka ni furaha na amani, mashabiki wa timu pinzani hata kama timu zao zinapofungwa huwezi kuona wakifikia hatua ya kuparurana ama kupigana au kufanyiana uadui ndani na nje ya uwanja.

Kama ikitokea jambo kama hilo la mashabiki, makocha ama wachezaji kufanyiana uadui, Fifa na vyama wanachama wa shirikisho hilo kwa nchi husika huchukua hatua kali za haraka.

Hata ndani ya uwanja mwamuzi huwa makini kuhakikisha hakufanyiki vitendo vyovyote vya kutaka kujengeana uadui ndiyo maana hutumia maonyo ya mdomo na wakati mwingine kadi ili kuepuka kuvuruga pambano la soka. Kitu cha kustaajabisha katika soka la Tanzania katika karne hii, bado kuna mambo ya kihuni yamekuwa yakifanywa na baadhi ya wasimamizi wa mchezo huo na mamlaka nyingine kitu kinachochafua taswira ya soka letu.

Juzi Jumamosi mkoani Iringa kumetokea tukio la aibu kwa soka la Tanzania. Katika pambano la Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kati ya wenyeji Lipuli Iringa na Mshikamano ya Dar es Salaam, kumetokea kitendo ambacho hakipaswi kunyamaziwa kwa sababu kinavuruga soka letu. Pambano hilo limedaiwa lilichezeshwa zaidi ya dakika 90 zinazohitajiwa na hata na zile za majeruhi, kwa kile kilichoelezwa kuitafutia timu wenyeji ushindi na mwamuzi kutoa penalti dakika za jioni iliyogomewa na Mshikamano.

Wachezaji hao walimvamia mwamuzi wa pambano hilo na kumpa kashkash kabla ya askari polisi waliokuwa uwanjani hapo kuingilia kati kumwokoa mwamuzi na kuwasulubu wachezaji wa Mshikamano. Picha za wachezaji kadhaa wa Mshikamano wakiwa na majeraha mbalimbali zilionekana mitandaoni na kibaya zaidi, tukio hilo ni kama lilitaka kuzimwa kwa vile hakuna mwandishi wa mkoa huo aliyeripoti tukio hilo zaidi na matokeo tu.

Mashuhuda wanadai Mshikamano waliadhibiwa kwa maagizo ya mamlaka ya mkoa huo. Mwanaspoti halina ushahidi juu ya hilo, lakini kwa kuwa wachezaji wa timu ngeni wamejeruhiwa na kukatengenezwa mazingira ya kuficha ukweli ni dalili za wazi wahusika hawawezi kukwepa lawama hata kidogo.

Kama wadau wa soka, kwanza tunalaani kitendo walichofanyiwa wachezaji wa Mshikamano mkoani Iringa, pia tunalaani tukio la wachezaji kumvamia mwamuzi hata kama walihisi walionewa, walipaswa kuwaachia kazi viongozi wao kupeleka malalamiko yao kwa TFF kuhusu uonevu waliokumbana nao. Pia tungependa kuliomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lichukue hatua kali za haraka dhidi ya tukio hilo. Vitendo kama hivi ambavyo siku za nyuma vilibatizwa jina la uzalendo ndivyo vinavyorudisha nyuma soka la Tanzania, pia vimekuwa vikichangia kwa sehemu kubwa kuzikwamisha timu zinazobebwa kwa mbeleko.

Kariakoo Lindi inakumbukwa jinsi ilivyokuwa ikisaidiwa kwa hali na mali na mamlaka za mkoa wao, kiasi timu zilizokuwa zikienda kucheza nazo mkoani humo zilikuwa zikikiona cha moto, lakini leo Kariakoo Lindi iko wapi? AFC Arusha nayo iliwahi kubebwa na wasimamizi wa Ligi Daraja la Kwanza kituo cha Arusha, leo iko wapi?

Ni kwa sababu siku zote dhuluma huwa haijengi, lakini figisu figisu hazisaidii maendeleo ya soka daima.

Ndiyo maana tunaisisitizia TFF isinyamazie uhuni uliofanyika mjini Iringa, wachukue hatua kali ili kusaidia kuepusha maafa viwanjani katika mechi za lala salama za FDL ambazo zinasakwa timu tatu za kupanda Ligi Kuu 2017-2018.

Msimu uliopita ligi hiyo ilishuhudia aibu ya upangwaji matokeo, lakini TFF ilichukua muda mrefu kutoa uamuzi kwa sababu zipo tuhuma kwamba vigogo wao walikuwa wanahusika, basi kwa hili lijisafishwe mapema.

RT angalieni msiharibu mapema

Uongozi wa Shirikisho la Riadha (RT) hauna hata miezi miwili tangu uchaguliwe na mtihani wao mkubwa uliopo mbele ni ushiriki wa Tanzania katika mashindano ya Mbio za Nyika (Cross Country) yatakayofanyika Machi.

Mashindano hayo yatakayofanyika nchini Uganda, ni kipimo cha kwanza kwa uongozi huo na lazima RT wajipange hasa katika kupata timu ya taifa itakayoiwakilisha nchini.

Majuzi Katibu Mkuu wa RT, Wilhem Gidabuday alinukuliwa kuwa mashindano ya taifa ya riadha yameahirishwa mpaka wikiendi hii, ili kutoa muda kwa mikoa kupata wanariadha wenye sifa stahiki. Hilo ni jambo zuri, lakini hofu yetu isiwe kuahirishwa kwa mashindano hayo ni kisingizio tu cha viongozi wa RT.

Kama sababu ya dhati, basi hatutarajii kuona timu ya taifa ikienda Uganda kama wasindikizaji, lazima ipigane kuweza kuliwakilisha vyema taifa na kurejea na medali ambavyo RT mpya imekuwa ikisisitiza wamekuja na mapinduzi.

Watanzania na hasa wanaofuatilia michezo ya riadha wamechoka kushuhudia wanariadha wa Tanzania kuwa wasindikizaji wa wenzao, lazima safari hii waenda Uganda na kurejea na medali ili kutuliza mioyo ya mashabiki hao.