Yanga bampa kwa bampa

Mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe (kushoto) akimtoka beki wa Mwadui FC, Iddy Mobbi wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana. Yanga ilishinda mabao 2-0. Picha na Omary Fungo

MASHABIKI wa Yanga jana walikuwa na furaha ya ajabu Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam baada ya timu yao kufanikiwa kukamata usukani wa Ligi Kuu Bara kutokana na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mwadui ya Shinyanga.

Wakirejea mistari ya kibao kinachotamba kwa sasa nchini cha msanii Darassa kiitwacho Muziki, mashabiki walikuwa wakiimba’ “blah blah blah hatutaki kusikia sio Simba, sio Chui sio Mamba soka letu linatosha kujigamba na hatuna maneno ya kwenye kanga kazi juu ya kazi yaani Bumper to Bumper...” Mashabiki hao waligeuza mistari ya wimbo huo wa Darassa baada ya mabao mawili kutoka kwa Mzambia, Obrey Chirwa kuirejesha kileleni Yanga baada ya miezi kadhaa kupitia nafasi hiyo ikishikiliwa na watani zao Simba.

Simba walijiweka kwenye hatari ya kuachia kiti hicho juzi Jumamosi walipokubali kipigo cha bao 1-0 toka kwa Azam waliopo nafasi ya tatu na Yanga jana Jumapili haikufanya ajizi kwa kupata ushindi huo muhumu.

Chirwa ambaye alikuwa majeruhi kwa muda mrefu aliifungia Yanga mabao hayo katika kipindi cha pili kwenye dakika za 69 na 83 yaliyowafanya mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara kufikisha pointi 46 na kuipiku Simba iliyosaliwa na pointi 45.

Chirwa alifunga bao la kwanza kwa mguu wa kulia akimalizia mpira uliotemwa na kipa Shaaban Kado aliyeokoa shuti la Simon Msuva kabla ya kufunga la pili akimalizia pasi ya kichwa cha Thabani Kamusoko.

Katika pambano hilo Mwadui inayonolewa na Kocha Msaidizi wa zamani wa Taifa Stars, Ali Bushiri ‘Benitez’, ilionyesha ushindani mkubwa kipindi cha kwanza kwa kuwazuia Yanga kupata angalau bao moja, huku wenyewe wakikosa mabao kadhaa ya wazi na kutoa dalili kwamba Yanga ingetoka uwanjani bila bao.

Mabadiliko yaliyofanywa na Kocha George Lwandamina kwa kuwatoa Deus Kaseke na Haruna Niyonzima na kuwaingiza Emmanuel Martin na Chirwa yaliisaidia Yanga kuongeza mashambulizi yake na kujipatia mabao hayo mawili.

Baada ya kufungwa bao la pili Mwadui iliamua kuwatoa Yasin Mustafa na Salim Khamis na kuwaingiza Kanoni na Joseph Kimwaga hata hivyo mabadiliko hayo hayakuweza kusaidia kitu na kujikuta wakitoka Uwanja wa Taifa kinyonge kwa kipigo cha mabao 2-0.

Katika mchezo huo mwamuzi msaidizi Haji Mwalukuta alilazimika kutibiwa na daktari wa Yanga dakika ya 71 baada ya kushikwa na misuli hali iliyosababisha mchezo huo kusimama kwa muda kabla ya kuendelea tena.

Kwenye pambano jingine la ligi hiyo Majimaji ya Songea ikiwa ugenini ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji wa Ndanda FC kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaoni mjini Mtwara.

Ligi hiyo itaendelea tena leo kwa michezo miwili, Mtibwa Sugar itaavana na Kagera Sugar mjini Bukoba wakati Stand United itaialika JKT Ruvu.

YANGA: Dida, Abdul, Mwinyi, Cannavaro, Yondani, Zulu, Msuva, Kamusoko, Tambwe/Makapu, Niyonzima/Martin  na Kaseke/Chirwa

MWADUI: Kado, Chollo, Malika, Mobby, Mustafa/ Kanoni, Awadh, Kabunda/ Luhende, Razack, Nonga, Seseme na Khamis/Kimwaga