Wachezaji kodi lazima hakuna jinsi

Muktasari:

  • Ni miaka miwili sasa imepita tangu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) itangaze kwamba wachezaji wanapaswa kulipa kodi (PAYE) lakini klabu zilishindwa kutekeleza agizo hilo mpaka baada ya kutolewa semina kwa viongozi wa klabu hizo.

SERIKALI ya Rais John Pombe Magufuli huwezi kuikimbia wala kuikwepa kirahisi rahisi na sasa imejikita kuhakikisha inakusanya kodi kwa watu wote wanaokwepa kulipa kodi hiyo na mwaka huu wachezaji kutoka klabu za Ligi Kuu Bara watalipa kodi kama wafanyakazi wengine wa mashirika ama serikalini pasipo kukwepa.

Ni miaka miwili sasa imepita tangu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) itangaze kwamba wachezaji wanapaswa kulipa kodi (PAYE) lakini klabu zilishindwa kutekeleza agizo hilo mpaka baada ya kutolewa semina kwa viongozi wa klabu hizo.

Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Huduma kwa Walipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo ameliambia Mwanaspoti kuwa Januari mwaka huu walikutana na viongozi hao na kuwapa semina kwani ni wajibu wa kila mfanyakazi kulipa kodi na tayari utekelezaji ulikwishaanza mara moja.

“Tulitoa elimu juu ya ulipwaji kodi hiyo, nadhani elimu ilieleweka kwani utekelezaji ulianza kufanyika. Hao ni wafanyakazi kama ilivyo kwa wafanyakazi wengine ambao wanalipa kodi, hiyo ni sheria ya nchi hivyo hakuna mfanyakazi ambaye hapaswi kulipa kodi.

“Mtu yeyote anayefanyakazi na kulipwa mshahara ajue kuwa ni lazima alipe kodi, hawa wanamichezo walishindwa kulipa miaka ya nyuma huenda hawakuelewa, hivi sasa kila mtu atalipa, maadamu tulitoa mwongozo kwa viongozi wao, iwe mchezaji wa ndani ama wa kigeni ili mradi tu ni mfanyakazi,” alisema.

Mwanaspoti inafahamu tangu Januari hadi Juni kila mchezaji alikuwa akikatwa 11% lakini kuanzia Julai imeelezwa kuwa itakatwa 9% kutokana na punguzo la serikali.