Singida United yalamba mkataba SpotiPesa

Muktasari:

Hafla ya kusaini mkataba huo imefanyika leo (Jumanne) kwenye hoteli ya Kempiski jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na watendaji wa Stand United na SpotiPesa.

Dar es Salaam. Klabu ya Singida United imeingia mkataba wa udhamini wa mwaka mmoja na Kampuni ya SpotiPesa ya Kenya wenye thamani ya Sh.250 Milioni za Tanzania.

Hafla ya kusaini mkataba huo imefanyika leo (Jumanne) kwenye hoteli ya Kempiski jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na watendaji wa Stand United na SpotiPesa.

Akizungumza wakati wa kusaini mkataba huo, Ofisa Utawala wa SpotiPesa Tanzania, Tarimba Abbas alisema hatua ya kampuni yake kuingia mkataba na Singida United inalenga kukuza soka hapa nchini.

"Timu hii imeonyesha mwelekeo mpya katika soka laetu, tumebaini mipango yao ni kuwa Leicester City ya Tanzania na ndio maana tumevutiwa kuwasapoti,"alisema Tarimba na kuongeza kuwa mkataba huo pia utahusisha bonasi na zawadi kwa wachezaji ikiwa timu hiyo itafanya vizuri msimu ujao.

Katibu Mkuu wa Singida United, Abdulrahman Sima alisema mkataba huo umekuja wakati muafaka.

"Tumepokea mkataba kwa mikono miwili, Singida tumedhamiria kubadilisha fikra za watanzania kupitia mchezo wa soka,"alisema Sima.