Simba hawataki ujinga, ila huyu Tambwe

Muktasari:

Yanga ambayo imetwaa taji la Ligi Kuu Bara kwa misimu miwili mfululizo, imekuwa ikibebwa na ubora wa mastraika wake wa kati na pembeni kutokana na uwezo mkubwa wa kufunga jambo ambalo Simba wamelishtukia na kulifanyia kazi.


SIMBA ilinyanyaswa na Yanga kwa misimu miwili mfululizo, lakini sasa imeshtukia silaha kubwa za watani wao hao na kutengeneza nguzo tano imara ili kubeba taji la Ligi Kuu msimu huu. Pia imejipanga kuhakikisha inaifunga Yanga wikiendi hii.

Yanga ambayo imetwaa taji la Ligi Kuu Bara kwa misimu miwili mfululizo, imekuwa ikibebwa na ubora wa mastraika wake wa kati na pembeni kutokana na uwezo mkubwa wa kufunga jambo ambalo Simba wamelishtukia na kulifanyia kazi.

Katika misimu hiyo miwili ambayo Yanga imetwaa ubingwa staa wao pia aliibuka mfungaji bora ambapo mwaka jana alikuwa ni Saimon Msuva na mwaka huu alichukua Amissi Tambwe, jambo ambapo pia Simba wamelishutukia na wameanza kumtengeneza mmoja wa washambuliaji wao ili aweze kuwa mfungaji bora msimu huu.

Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja alisema waligundua timu yao msimu uliopita ilishindwa kufanya vizuri kutokana na kumtegemea mtu mmoja ama wawili na sasa wameongeza nguvu na hawamtegemei tena mtu mmoja kupata matokeo.

“Simba ya msimu huu inaweza kupata matokeo kupitia kwa mchezaji yeyote, mfano kwenye mchezo na Majimaji uliona walioanza walishindwa kufanya vizuri na waliotoka benchi wakaibeba timu,” alisema Mayanja. “Hata washambuliaji wetu wa kati wasipofunga bado tuna uwezo mkubwa wa kupata mabao kupitia kwa washambuliaji wengine, tazama mchezo wa Majimaji mabao yamefungwa na Kichuya (Shiza) na Mnyate (Jamal), hao wanacheza pembeni,” alifafanua kocha huyo wa zamani wa Kagera Sugar.

 

HUKU KICHUYA,

KULE TWAMBWE

Tathmini imeonyesha mabao 12 ya Simba msimu huu yamefungwa na wachezaji watano tofauti ambapo, Kichuya ndiye anaongoza akiwa amefunga mabao manne ikiwemo bao pekee la ushindi dhidi ya Azam.

Laudit Mavugo ni wa pili akiwa amefunga mabao matatu wakati Ibrahim Ajibu na Jamal Mnyate wanafuatia wakiwa na mabao mawili kila mmoja huku straika ngongoti Blagnon Frederic akiwa na bao moja.

Hata hivyo, kwa upande wa Yanga kabla ya mchezo wa jana wachezaji watano pia walikuwa wamehusika katika mabao yao nane ya msimu huu. Tambwe ndiye anaongoza akiwa amefunga mabao matatu na kufuatiwa na Kaseke mwenye mabao mawili huku Donald Ngoma, Juma Mahadhi na Msuva wakiwa wamefunga bao moja kila mmoja.

Mayanja alisema tayari wameanza kulifanyia kazi suala la uchoyo katika safu yao ya ushambuliaji kutokana na baadhi ya wachezaji kuwa wabinafsi wakifika eneo la mwisho kwa kutaka wafunge wao tu.

“Tumeliona hilo tatizo, kuna baadhi ya washambuliaji hawajali sana matokeo ya timu, wanataka wafunge wao tu kitu ambacho sio kizuri, tunapambana kulitatua hilo tatizo mapema.

Tunataka Simba icheze soka safi la kuvutia huku ikionyesha uwezo kwenye pasi za mabao ili tufunge mengi zaidi,” alisema Mayanja.