Rooney akomaa Man United

Muktasari:

  • Mwanzoni mwa wiki hii, Mourinho alisema kwamba hana uhakika iwapo nahodha huyo, Rooney ataendelea kuwapo Manchester United  wakati kukiwa na tetesi za uhamisho wake kwenda China kipindi cha dirisha dogo la usajili kabla halijafungwa mwishoni mwa mwezi huu. Pia, alisisitiza kwamba kamwe hawezi kumuuza mchezaji mwenye rekodi nzuri ya kufunga mabao kwenye klabu hiyo.

London, England. Mshambuliaji wa Manchester United, Wayne Rooney amekataa ofa ya kwenda kukipiga China, huku akimaliza uvumi uliokuwa umesambaa kwenye vyombo vya habari  na mitandao kuhusu kuhamia kwenye Ligi Kuu ya nchi hiyo.

Nahodha huyo wa Manchester United alihusishwa na kuhama kwenye klabu hiyo baada ya kuwapo tetesi kwamba hana uhusiano mzuri na kocha Jose Mourinho.

Mwanzoni mwa wiki hii, Mourinho alisema kwamba hana uhakika iwapo nahodha huyo, Rooney ataendelea kuwapo Manchester United  wakati kukiwa na tetesi za uhamisho wake kwenda China kipindi cha dirisha dogo la usajili kabla halijafungwa mwishoni mwa mwezi huu. Pia, alisisitiza kwamba kamwe hawezi kumuuza mchezaji mwenye rekodi nzuri ya kufunga mabao kwenye klabu hiyo.

Hata hivyo Rooney amethibitisha kwamba licha ya kupokea ofa kutoka sehemu mbalimbali hana matarajio ya kuondoka kwenye klabu kipindi cha msimu ambacho timu hiyo inapambana kuwapo kwenye nafasi nne za juu.

“Licha ya ofa ambazo nimeletewa kutoka klabu nyingi, jambo ambalo nalifurahia, lakini nataka kumalizia msimu huu nikiwa na Manchester United,” alisema mchezaji huyo kupitia taarifa rasmi iliyowekwa kwenye tovuti ya kalbu hiyo.

Alisema, “Ninatarajia kucheza kwa bidii ili kuisaidia timu kufikia mafanikio ya kuwapo kwenye nafasi nne za juu. Klabu ipo kwenye kipindi kigumu na mimi nataka niwe sehemu ya mafanikio.”

Rooney ameanza mechi nane tu za Ligi Kuu England akiwa chini ya kocha Mourinho huku chaguo lake la kwanza wakiwa ni Zlatan Ibrahimovic, Anthony Martial, Marcus Rashford, Juan Mata  na Henrikh Mkhitaryan katika nafasi za ushambuliaji.

Rooney (31) hajacheza tangu timu hiyoalipoingia kipindi cha pili timu hiyo ilipotoka suluhu ya bila kufungana katika mchezo wake dhidi ya Hull City Februari Mosi. Hata hivyo, amekuwa akisumbuliwa na maumivu kwa wiki tatu sasa kutokana na kuwa majeruhi.

Kocha wa Tianjin Quanjian, Fabio Cannavaro  alisema kwamba timu hiyo imeshindwa kumpa nafasi mshambuliaji huyo wa Manchester United jambo linalosababisha kutoonyesha uwepo wake kwenye timu.

Rooney mwenye mabao matano na asisti 10 kwenye mashindano yote aliyoshhiriki alimfurahisha mkongwe  Bobby Charton kutokana na  faulo aliyopiga kwenye mchezo dhidi ya Stoke Cityna anatarajiwa kucheza katika mchezo wa fainali kesho dhidi ya Southampton kwenye Uwanja wa Wembley kutokana na kuumia kwa Mkhitaryan and Michael Carrick.