Nditi wa Chelsea anatia huruma

Mtanzania Adam Nditi aliyekuwa akikipiga katika timu ya vijana ya Chelsea

Muktasari:

Nditi alisajiliwa na Chelsea mwaka 2009 wakati huo akiwa na miaka 15 na kujiunga na academia ya klabu hiyo ambayo aliichezea kwa miaka mitano na kuanza kuibua matumaini mapya hasa kwa mashabiki wa Tanzania kabla ya kutemwa mwaka 2014.

UNAMKUMBUKA yule Mtanzania Adam Nditi aliyekuwa akikipiga katika timu ya vijana ya Chelsea? Kwa sasa anatia huruma baada ya kujiunga na klabu ya Farnborough inayoshiriki mashindano ya mchangani.

Nditi alisajiliwa na Chelsea mwaka 2009 wakati huo akiwa na miaka 15 na kujiunga na academia ya klabu hiyo ambayo aliichezea kwa miaka mitano na kuanza kuibua matumaini mapya hasa kwa mashabiki wa Tanzania kabla ya kutemwa mwaka 2014.

Nyota huyo mzaliwa wa Zanzibar ni ndugu wa damu wa kiungo wa Mtibwa Sugar, Shaban Nditi na nyaraka za uhamisho wake kutoka Zanzibar mwaka 2009 zinaonyesha kuwa aliruhusiwa kuondoka nchini na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Hata hivyo klabu yake ya sasa ya Farnborough inashiriki Ligi ya Kusini mwa England ambayo inashirikisha timu za ridhaa na ambazo si profesheno kamili jambo ambalo linaonyesha kuwa Mtanzania huyo ameporomoka kwa kiwango kikubwa na majaliwa yake katika soka la kiwango cha juu yanabaki kuwa njia panda.

Nditi ambaye anacheza nafasi ya beki kuna wakati alikuwa akipigiwa upatu wa kuitwa katika timu ya Tanznaia Taifa Stars lakini kumekuwa na ugumu hasa baada ya kupotea kutoka Chelsea na kushuka hadi katika timu za madaraja hayo ya chini.