Morgan ashinda mashindano ya Baiskeli

Muktasari:

Mshindi wa mbio hizo kwa upande wa wanaume aliyejinyakulia kitita cha Sh 200,000, Morgan alisema kuwa kuwa siku zote haogopi kushindwa ndio siri yake ya kushinda michuano hiyo.

Arusha: Mwendesha Baiskeli Thomas Morgan kutoka Habari Node ameshinda mashindano ya Baiskeli ya km 120 yaliyofanyika mwishoni mwa wiki Mkoani Arusha.

Mashindano hayo yaliyoanza Mnara wa Sanaa kuelekea Wilayani Monduli na kumalizikia Uwanja wa Mpira wa Sheikh Amri Abeid ilishuhudiwa Muingereza Morgan akitumia saa 2:58:25, huku nafasi ya pili ikienda kwa Richard Laizer aliyetumia saa 2:59:39, na nafasi ya tatu ikienda kwa Denis Julius aliyetumia saa 3:00:15.

Mshindi wa mbio hizo kwa upande wa wanaume aliyejinyakulia kitita cha Sh 200,000, Morgan alisema kuwa kuwa siku zote haogopi kushindwa ndio siri yake ya kushinda michuano hiyo.

“Mwezi uliopita nilikuwa Afrika Kusini kushiriki mbio za JOBERG 2C zilizofanyika katika jiji la Johannesburg yaliyokuwa na umbali wa zaidi ya km 1,000 na yalifanyika kwa siku tisa mfululizo na nilifanikiwa kushika nafasi ya 15” alisema Morgan

Aliongeza Tanzania kuna vipaji vya aina nyingi katika michezo, tatizo hakuna anayeviibua na kuviendeleza kama wanavyofanya nchi nyingine zilizoendelea kwenye michezo.

Kwa upande wa wanawake waliokimbia km 70, Habibu Mathias aliibuka mshindi, akifuatwa na Lauresi Luzuba na Sophia Hadson akishika nafasi ya tatu.

Mwenyekiti wa Klabu ya Arusha (ACC), Mosses Andrew alisema mashindano hayo yameshirikisha mikoa minne ya Kilimanjaro, Manyara, Mwanza na wenyeji Arusha huku Dar es salaam walifika lakini hawakushiriki.

“Mkoa wa Mbeya walithibitisha ushiriki wao, lakini hawakutokea kwenye mashindano na hawajatoa sababu ya kutofika kwao maana mara ya mwisho tunaongea nao walituambia wapo njiani kuja Arusha, na Dar es Salaam wamewasili hadi Arusha lakini hawakushiriki”