Mghana awatingisha Juuko na Bokungu Msimbazi

Muktasari:

  • Ujio wa mchezaji huyo unawaumiza vichwa viongozi wa Simba huku wachezaji wawili ambao ni Juuko Murshid na Janvier Bokungu wakiwa matumbo joto.
  • Habari za ndani zinadai kwamba Simba inafikiria kumchomoa mmoja wa mabeki hao ili kumpa nafasi Agyei atoe changamoto kwa Vincent Angban. Ingawa baadhi wanapendekeza Mussa Ndusha ambaye mzunguko wa kwanza hakucheza mkataba wake usitishwe kutokana na umuhimu wa Bokungu na Juuko kwenye ulinzi.

INYESHE au liwake, Kipa Mghana Daniel Agyei, aliyetua nchini mchana wa jana Jumatano lazima asaini Simba kabla ya wikiendi ijayo.

Ujio wa mchezaji huyo unawaumiza vichwa viongozi wa Simba huku wachezaji wawili ambao ni Juuko Murshid na Janvier Bokungu wakiwa matumbo joto.

Habari za ndani zinadai kwamba Simba inafikiria kumchomoa mmoja wa mabeki hao ili kumpa nafasi Agyei atoe changamoto kwa Vincent Angban. Ingawa baadhi wanapendekeza Mussa Ndusha ambaye mzunguko wa kwanza hakucheza mkataba wake usitishwe kutokana na umuhimu wa Bokungu na Juuko kwenye ulinzi.

Habari zinadai kwamba uwezekano wa Ndusha au Bokungu kutoka bado ni mkubwa kutokana na harakati za kumnasa beki wa kulia wa Prisons, Salum Kimenya.

Katika hatua nyingine, Mama wa Kimenya, Asia Kimenya ametoa la moyoni kwamba klabu kubwa nchini zina tabia ya ‘kuua’ vipaji vya wachezaji hivyo anahofia pia mwanaye akitua Simba anaweza kupotea japokuwa amedai wamemuhakikishia kumtunza kama anavyotaka.

Hofu ya mama huyo ni kuwa mwanaye ambaye ni mwajiriwa wa Jeshi la Magereza nchini anaweza kupoteza ajira na kwenda Simba ambako akicheza na kushindwa kutimiza malengo ya klabu ataanza kukaa benchi au jukwaani kabisa na baadaye kuonekana hafai na kutemwa.

Simba inawania saini ya Kimenya kwa mkataba wa Sh 25 milioni kwa miaka miwili pesa ambayo beki huyo pamoja na mama yake wameigomea, wakihofia kuharibu kazi yake mambo yatakapokuwa magumu ndani ya kikosi hicho huku akiwa amepoteza ajira yake. Wao wamependekeza ofa ya Sh 40 milioni kutoka Sh 50 milioni ya awali.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Urambo, Tabora, Asia alisema: “Simba walinipigia wakidai wanamuhitaji Kimenya na walisema watarudi tena baada ya kuwaambia kile tunachokihitaji, kwanza ni pesa ya usajili lakini wasijemchukuwa mwanangu na kumkalisha benchi mwisho wa siku akaharibu maisha yake kwani atakuwa ameacha kazi. Niliwaambia mwanangu nataka acheze sio kwamba akiharibu kidogo ambapo ni kawaida kwa binadamu basi wamvuruge.”

“Bado hawajapiga tena hivyo tunasubiri wapige na Kimenya anapaswa kurudi kazini kwake akaendelee na kazi. Pesa yao ni ndogo kwani wanasema bajeti yao ni ndogo pia ndiyo maana wanataka kumpa Sh 25 milioni hapo anatakiwa ailipe na Prisons kwani anakwenda kuvunja mkataba, hawezi kuondoka Prisons kwa kiasi hicho cha pesa. Wakiongeza kile tulichowaambia sitakuwa na kinyongo na atakwenda kucheza Simba,” alisema Asia.

Hii ni mara ya tatu kwa Simba kumuhitaji Kimenya lakini wamekuwa wakishindwa kupata saini yake kutokana na ofa ndogo wanayompa huku akiwa amebakiza mkataba wa miezi sita ndani ya timu ambao ni nje ya ajira yake.