Kocha wa maana aondoka Dar

Kocha Bernandro Taraves.

Muktasari:

Simba ilikuwa imecheza mechi 13 za Ligi Kuu zikiwamo sita mfululizo ikishinda, ilikumbana na kipigo hicho kwa Lyon kwenye Uwanja wa Uhuru kabla ya kwenda kuongezewa maumivu na Tanzania Prisons Mbeya kwa kufungwa mabao 2-1.

KOCHA Bernandro Taraves ndiye aliyekuwa wa kwanza kumtibulia rekodi Kocha Joseph Omog, baada ya timu yake ya African Lyon kuifunga Simba bao 1-0 kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara.

Simba ilikuwa imecheza mechi 13 za Ligi Kuu zikiwamo sita mfululizo ikishinda, ilikumbana na kipigo hicho kwa Lyon kwenye Uwanja wa Uhuru kabla ya kwenda kuongezewa maumivu na Tanzania Prisons Mbeya kwa kufungwa mabao 2-1.

Sasa ni kwamba Kocha huyo Mreno, amesepa zake na kuiacha Lyon wakati klabu hiyo ikiwa kwenye sakata dhidi ya nyota wake watatu kutoka Uganda, ambao wamezinguana na mabosi wa klabu hiyo.

Mreno Taraves ameamua kuitema timu hiyo bila kutarajiwa baada ya kuiongoza katika duru la kwanza na kumaliza katika nafasi 11 ikiwa na pointi 17.

Uongozi wa Lyon umethibitisha kutimika kwa kocha huyo wakati sakata lao na Waganda, Hood Mayanja, William Otong na Tito Okello likiwa bado halijapatiwa ufumbuzi baada ya pande hizo kutifuatana kwelikweli.

Mkurugenzi wa Lyon, Rahim Kangezi ‘Zamunda’, alikiri kuwa ni kweli kocha huyo ameondoka katika klabu yao na amepata timu nyingine kwao Ureno, ambayo ina maslahi zaidi na kwamba wameridhia kuondoka kwake na kumpa baraka zote.

“Ni kweli alitutaarifu kuwa anahitaji kuondoka, awali ilitupa changamoto ila alituambia pia amepata timu kubwa zaidi yetu hivyo, anatuomba aweze kuondoka tukaona kama hilo limekaa vyema kwa upande wake tukambariki aende,” alisema Zamunda.

Aliongeza kuwa kocha huyo alitua kuwasaidia katika duru la kwanza, ila hawakuwa na mkataba naye mrefu ni makubaliano yaliyokuwepo pande mbili tu.

Aliongeza kuwa kwa sasa Lyon itakuwa chini ya Kocha Charles Otieno, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Ufundi wa klabu hiyo.

Katika taarifa yake Tavares aliandika katika ukurasa wake wa mtandao jinsi anavyosijikia vibaya kuiacha Lyon, lakini akiwa hana jinsi, huku akiisifia Tanzania kuwa ni moja ya nchi bomba na kuahidi atarejea tena kujua kufundisha soka kama mambo yakienda ndivyo sivyo huko anakokwenda.