Kila shabiki Yanga anadaiwa buku

Muktasari:

  • Tathmini ya soka la Tanzania inaonyesha kwamba klabu za Simba na Yanga zinagawana mashabiki wa mchezo huo nchini huku timu nyingine zikipata watu wasiofikia hata asilimia tano kutokana na umaarufu na ukongwe wa timu hizo mbili.

KILA shabiki wa klabu ya Yanga popote alipo Tanzania ajue anadaiwa kiasi cha Sh 1,100 ili kufuta madeni yote ya klabu hiyo na kuiacha kwenye mikono salama.

Kwa mujibu wa taarifa ya madeni ya Yanga iliyotolewa Septemba mwaka jana, klabu hiyo inadaiwa kiasi cha fedha kinachofikia Sh11.6 bilioni lakini kumbe kwa idadi ya mashabiki wake nchini ni fedha ya mboga tu ambayo wakiamua kupiga harambee ya kuikusanya mkoa kwa mkoa hata wiki haiishi itakuwa imeshapatikana na chenji inabaki.

Tathmini ya soka la Tanzania inaonyesha kwamba klabu za Simba na Yanga zinagawana mashabiki wa mchezo huo nchini huku timu nyingine zikipata watu wasiofikia hata asilimia tano kutokana na umaarufu na ukongwe wa timu hizo mbili.

Hadi kufikia mwaka 2015 idadi ya Watanzania ilikadirwa kuwa milioni 53 ambapo idadi ya watu wenye umri kati ya miaka 18-64 ni milioni 22.7, umri ambao watu ndiyo wanakuwa na mapenzi halisi ya soka. Hata hivyo idadi hiyo inatajwa kuongezeka kwa sasa.

Hii inamaanisha kwamba Simba na Yanga zinagawana idadi hiyo ya mashabiki ambapo Yanga itakuwa na mashabiki wanaofikia milioni 11 sawa na Simba huku idadi ya watu milioni moja ikitajwa kuwa ni mashabiki wa timu nyingine ama watu ambao hawapendi soka kabisa.

Kwa mantiki hiyo ni kwamba kwa deni la Sh11.6 bilioni, mashabiki hao milioni 11 wa Yanga wakichanga kiasi cha Sh1,100 tu wanaweza kulipa kiasi chote hicho na fedha ikabaki lakini ugumu unabaki kwa namna ya kuwaleta pamoja ili walipe. Kiuhalisia Sh1,100 haitoshi kununua msosi wa kawaida kwa Mamantilie kwa sasa labda ulielie sana.

Katika deni hilo la Yanga, aliyekuwa Mwenyekiti wao Yusuf Manji anadai kiasi kinachofikia Sh5.4 bilioni fedha ambayo mashabiki hao wakiamua kujitoa kwa moyo mmoja kwa kutoa tu Sh500 watakuwa wamemalizana naye.

Manji alibwaga manyanga mapema wiki hii ikiwa ni miaka mitano tangu alipochanguliwa kwa mara ya kwanza kuiongoza klabu hiyo.

WANACHAMA MZIGO

Kwa mujibu wa Katiba ya Yanga, watu wenye dhamana ya klabu ni wanachama ambao idadi yao inatajwa kuwa kati ya 15,000 na 20,000.

Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa alikiri kwa sasa wanafanya uhakiki wa wanachama kufahamu idadi yao kamili.

“Bado hatujawa na idadi kamili lakini tayari tumewasiliana na matawi ili kuona tunapata idadi hiyo, wapo pia waliojiunga kwa njia ya benki,” alisema.

Takwimu ambazo Mwanaspoti  imezikusanya kutoka kwenye matawi, kwa Dar es Salaam pekee, Yanga ina matawi 100 ya wanachama ambapo kila tawi lina watu wasiopungua 100, hivyo  wapo zaidi ya 10,000.

Licha ya idadi hiyo kubwa, wanachama hai hawazidi 15,000 na hao ndiyo wenye mamlaka ya kuamua klabu hiyo ijiendeshe kwa mfumo gani, ai iweje.

Hesabu zinaonyesha kwamba kwa Wanachama 15,000 kila mmoja atapaswa kulipa kiasi cha Sh 600,000 ili kuweza kufuta madeni ambayo yanawazunguka fedha ambazo inaonekana kuwa ni ngumu.