Kichuya awalaza njaa mastaa Yanga

Muktasari:

  • Nyota wa Yanga ndio wanaoumia zaidi kwani wamejikuta wakilazimika kulala njaa kutokana na mabao mawili, la  Laudit Mavugo lililotokana na krosi pasi ya Kichuya na lile lililofungwa kiufundi na Kichuya mwenyewe likiwa la ushindi.

KAMA kuna mtu ambaye wana Yanga wanamlaani kimya kimya, basi ni Shiza Kichuya, winga aliyepeleka maafa Jangwani kwa kuhusika kwake na mabao mawili yaliyoizamisha Yanga katika pambano la juzi la watani wa jadi.

Mpaka jana Jumapili mchana, huwezi kuamini lakini ni kweli kuwa, mashabiki wa Yanga na hata wachezaji walikuwa hawajui kipi kilichowatokea Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam hata wakalala mabao 2-1 mbele ya watani zao Simba.

Nyota wa Yanga ndio wanaoumia zaidi kwani wamejikuta wakilazimika kulala njaa kutokana na mabao mawili, la  Laudit Mavugo lililotokana na krosi pasi ya Kichuya na lile lililofungwa kiufundi na Kichuya mwenyewe likiwa la ushindi.

Kabla ya mchezo huo, vigogo wa Yanga walikutana na wachezaji wa timu hiyo na kuwapa ahadi ya kuwapatia Sh. 30 milioni endapo wataifunga Simba na wakati wa mapumziko Yanga ikiwa mbele kwa bao 1-0 la mkwaju wa penalti ya Simon Msuva walipewa ujumbe wa kuongezewa Sh 20 milioni.

Hata hivyo bwana, baada ya Kichuya kuingia uwanjani kumpokea Nouvalt Lufunga katika kipindi cha pili na winga huyo kufanya mautundu yake, alitibua kila kitu kwani ahadi zote mbili walizopewa vijana wa Jangwani ziliyeyuka.

Krosi pasi tamu aliyoituma kwa Mavugo na kumfanya Mrundi huyo kufunga bao lake la kwanza dhidi ya Yanga tangu atue kutoka kwao, kisha kuwahadaa mabeki wa Yanga na kufungabao la kideoni dakika ya 81, yalizima ndoto za mastaa hao wa Yanga, ambao sasa wanalazimika kupiga miayo bila kupenda.

“Ilikuwa tupate fedha nyingi sana, lakini ndiyo hivyo tujilaumu wenyewe kwa kitu kilichotokea unajua awali tuliahidiwa kupewa Sh 30 milioni kama  tungeshinda,” alisema mmoja wa mabeki wa Yanga.

“Tulipokuwa mapuziko tuliongezewa ahadi nyingine kuwa, kama tukikomaa na ushindi huo au kuongeza mabao zaidi zingeongezwa Sh 20 milioni katika ahadi ya kwanza, lakini kilichotokea tumuachie Mungu inaumiza sana,” alisema beki huyo kwa sauti ya kukata tamaa, huku wenzake wakiimanisha vichwa chini.

Yanga ilipoteza mechi yake ya tatu msimu huu na ya kwanza tangu mwaka juzi dhidi ya Simba katika Ligi Kuu Bara baada ya kulala mabao 2-1 na kusababisha pengo la pointi baina yao na watani kufikia tano kwa sasa, japo ina mechi moja mkononi. Yanga itashuka dimbani keshokutwa kuvaana na Ruvu Shooting kabla ya kuifuata Mtibwa Sugar Jumapili mjini Morogoro.