Heh! MO amzidi maarifa Manji

MANJI

Muktasari:

  • Makamu Mwenyekiti wa Kundi la Friends of Simba, Mulamu Ng’ambi aliliambia Mwanaspoti kuwa kama mabadiliko yakikubali MO awekeze Sh20 bilioni kwa asilimia 51 ya hisa, hizo asilimia nyingine zikiuzwa Simba itapiga mkwanja wa maana ambao unaweza kuwekezwa na kuongeza kipato klabuni hapo

SIMBA imeanza mchakato wa kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo kutoka ule wa wanachama unaotumika sasa kwenda mfumo wa hisa na sasa imebainika kuwa mchakato huo ukikamilika Simba itakuwa si ya kufananishwa tena na Yanga.

Bilionea Mohammed Dewji tayari ametangaza nia ya kuwekeza Sh20 bilioni kwa asilimia 51 ya hisa na fedha hizo zitawekezwa na kuzalisha faida ya Sh3.5 bilioni kwa mwaka halafu atajazia tena Sh2 bilioni ili timu hiyo iweze kuwa na bajeti ya Sh5.5 bilioni lakini kumbe hiyo ni kwa kuanzia tu kwani mauzo ya asimilia 49 za hisa zilizosalia yakifanyika Simba itakuwa inaichungulia TP Mazembe na kuondoka kabisa katika daraja la Yanga ambayo inataka kukodishwa na tajiri Yusuf Manji.

Makamu Mwenyekiti wa Kundi la Friends of Simba, Mulamu Ng’ambi aliliambia Mwanaspoti kuwa kama mabadiliko yakikubali MO awekeze Sh20 bilioni kwa asilimia 51 ya hisa, hizo asilimia nyingine zikiuzwa Simba itapiga mkwanja wa maana ambao unaweza kuwekezwa na kuongeza kipato klabuni hapo.

“Unajua kuna watu bado hawajaelewa vizuri, huu mfumo wa hisa unahusisha mambo mengi na kubwa ni kutafuta thamani ya Simba ili kuweza kuzipa thamani hisa, kama MO anataka kuweka bilioni 20 kwa asilimia 51, inamaanisha kuwa asilimia 49 zinaweza kuwa na thamani ya Sh18 bilioni ama zaidi,” alisema.

“Mfano kama Simba ikiamua kuuza tu, hapo asilimia 20 nyingine ya hisa inaweza kupata fedha nyingine nje ya zile Sh20 bilioni za MO, hizi sasa zinaweza kutumika katika uwekezaji mwingine, mfano katika biashara ama chochote na faida yake ndiyo itaamuliwa ifanyie nini klabuni,” alifafanua.

Mulamu alisema kama baadaye Simba itafuzu katika hatua za juu za mashindano ya Afrika, inaweza kuongeza bajeti yake kwa kuwa ina fedha ilizowekeza tofauti na sasa na italazimika kutumia fedha za michango.

“Mfano kama ikitokea tunacheza nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika kwa miaka miwili mfululizo, inamaanisha mahitaji ya timu yatakuwa makubwa na bajeti itahitajika kubwa, hiyo fedha kuipata itakuwa ni rahisi kwa kuwa tayari tumewekeza fedha nyingi zinazozalisha faida,” alifafanua.

THAMANI YA SIMBA PASUA KICHWA

Katika hatua nyingine, Mulamu alisema suala gumu zaidi kwa sasa ni kupata thamani halisi ya Simba kwani katika mapato na matumizi inajiendesha kwa hasara na thamani yake itaonyesha ni sifuri. Bosi huyo aliongeza kuwa kutafuta thamani pia kwa kutumia mali za Simba nalo ni janga kwa kuwa ina majengo mawili tu pale Kariakoo na eneo inalojenga uwanja pale Bunju.

“Thamani inaweza kutafutwa kwa kuangalia mapato na matumizi lakini kwa sasa timu inajiendesha kwa hasara, huko tutaingia chaka. Kama tutatumia mali za klabu bado thamani itakuwa chini kwa kuwa klabu haina mali nyingi, bado tunatazama namna nyingine sahihi,” alisema.