Hebu sikia huyu Omog alichowaambia Simba

Kocha wa Simba, Joseph Omog.

Muktasari:

Omog ambaye aliwapa Azam FC ubingwa pekee mwaka 2013 na sasa anataka kufanya maajabu kwa Simba iliyoukosa ufalme huo kwa misimu minne mfululizo, hakutaka kuwafananisha Wekundu hao na klabu za Ulaya, lakini akasisitiza mashabiki wenyewe ndiyo watatoa majibu.

LICHA ya kikosi cha Simba kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu Bara, Mcameroon wao, Joseph Omog ametamka mbona hapo bado kabisa, ndiyo kwanza asilimia 60 ya kile anachokitaka na atakapofanikiwa kwenye 90 mashabiki watapagawa zaidi na pengine huenda Yanga wasiende hata uwanjani.

Omog ambaye aliwapa Azam FC ubingwa pekee mwaka 2013 na sasa anataka kufanya maajabu kwa Simba iliyoukosa ufalme huo kwa misimu minne mfululizo, hakutaka kuwafananisha Wekundu hao na klabu za Ulaya, lakini akasisitiza mashabiki wenyewe ndiyo watatoa majibu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Omog ambaye si msemaji sana alisema wanashinda mechi sasa hivi kwa sababu wachezaji wanafuata maelekezo na mbinu za mchezo, lakini kwa mtazamo wake, ndiyo kwanza wanaanza kukaribia ubora anaoutaka yeye.

“Nataka kuwa na kikosi bora na imara kwa sasa bado kabisa na kama kufanikiwa ni kwa asilimia 60 tu na kama tutasogea na tukafika angalau kwenye asilimia 90 ninayoitaka mimi Simba itakuwa habari nyingine na hata wewe utaona mabadiliko. Sasa mechi tunashinda lakini kushinda na ubora ni kitu tofauti pale zinatumika mbinu zaidi lakini tutakaposogea na kufikia ninapopataka mambo yatakuwa rahisi sana na mashabiki wenyewe ndiyo watasema,”alisema Omog ambaye kikosi chake kinaongoza ligi na pointi 23.

“Lakini kufika hapo lazima nguvu itumike zaidi, kila mchezaji akili yake iwe inafikiria ushindi tu na siyo kitu kingine na kwa sasa tatizo kubwa ambalo linasumbua ni timu kupoteza mipira, kwani kupoteza mipira au nafasi katika kufunga tunakuwa tunajitengenezea hatari wenyewe,”alifafanua Omog ambaye amewataka mashabiki wasimbeze Laudit Mavugo kwavile yeye ndiye anayeshinda naye mazoezini na anajua nini kinakuja, wawe na subira.

Simba inacheza na Mbao leo Alhamisi katika mechi ya ligi kuu na baada ya hapo itakwenda mikoani kucheza na Toto African, Mwadui na Stand United. Lakini itakaporudi Dar es Salaam kwenye mechi yao ya kwanza Yanga itakuwa na kocha mpya jukwaani huku Hans Pluijm akikusanya kilicho chake.